< Hesabu 15 >

1 Bwana akamwambia Mose,
Kisha BWANA akanena na Musa, akasema,
2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Baada ya ninyi kuingia katika nchi ninayowapa kama nyumbani,
“Sema na wana wa Israeli uwaambie, 'Mtakapoingia katka nchi ambayo mtaishi, ambayo BWANA atawapa,
3 nanyi mkitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto, kutoka makundi ya ngʼombe au kondoo, kama harufu nzuri inayompendeza Bwana, ikiwa ni sadaka za kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum ama sadaka ya hiari au sadaka ya sikukuu zenu,
mtatakiwa kuandaa sadaka kwa moto kwa BWANA, sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya kukamilisha kiapo au sadaka ya hiari, au sadaka katika sikukuu zenu, ili kutoa harufu nzuri kwa BWANA ya ng'ombe au ya kondoo.
4 ndipo yeye aletaye sadaka yake ataiweka mbele za Bwana sadaka ya nafaka, sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta.
Utamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya sadaka ya unga mwembamba uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta.
5 Pamoja na kila mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, andaa robo ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji.
Na tena mtatoa pamoja na sadaka ya kuteketezwa, au kwa sadaka ya divai robo ya hini ya sadaka ya vinywaji kwa kila mwanakondoo.
6 “‘Pamoja na kondoo dume andaa sadaka ya nafaka ya sehemu mbili za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na theluthi moja ya hini ya mafuta,
Kama unatoa sadaka ya kondoo dume, utaandaa sadaka ya unga ya sehemu za kumi mbili za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na sehemu ya tatu ya hini ya divai.
7 na theluthi moja ya hini ya divai kama sadaka ya kinywaji. Vitoe kama harufu nzuri inayompendeza Bwana.
Kwa sadaka ya kinywaji, mtatoa sehemu ya tatu ya hini ya divai ambayo itatoa harufu nzuri kwa BWANA.
8 “‘Unapoandaa fahali mchanga kama sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum au sadaka ya amani kwa Bwana,
Utakapoandaa fahari kwa ajiliy a sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya kutimiza kiapo, au sadaka ya amani kwa BWANA,
9 leta pamoja na huyo fahali sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efa uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.
Ndipo utakapotoa sadaka ya fahari pamoja na sadaka ya unga ya sehemu za kumi tatu za unga mwembamba uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.
10 Pia utaleta nusu ya hini ya divai kama sadaka ya kinywaji. Itakuwa sadaka iliyoteketezwa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana.
Mtatoa sadaka ya kinywaji nusu ya hini ya divai, sadaka iloyotengenezwa kwa moto ili kufanya harufu nzuri kwa BWANA.
11 Kila fahali au kondoo dume, kila mwana-kondoo au mbuzi mchanga, atatayarishwa kwa njia hii.
Itafanyika hivi kwa kila fahari, kwa kila kondoo dume, na kila mwanakondoo dume au mbuzi mchanga.
12 Fanyeni hivi kwa ajili ya kila mmoja, kwa kadiri ya wingi wa mtakavyoandaa.
Kila sdaka utakayoindaa na kuitoa itafanyika kama ilivyoanishwa hapa.
13 “‘Kila mmoja ambaye ni mzawa ni lazima afanye vitu hivi kwa njia hii hapo aletapo sadaka ya kuteketezwa kwa moto kama harufu nzuri inayompendeza Bwana.
Wazawa wote wa Israeli watafanya mambo haya kwa utaratibu huu, yeyote atakayeleta sadaka iliyotengenezwa kwa moto, ili kufanya harufu nzuri kwa BWANA.
14 Kwa vizazi vijavyo, wakati wowote mgeni au mtu mwingine yeyote anayeishi miongoni mwenu aletapo sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana, ni lazima afanye sawasawa kabisa na jinsi mnavyofanya ninyi.
Na kama kuna mgeni anayeishi kati yenu, au yeyote atakayeishi na watu wa vizazi vyenu vyote, lazima atengeneze sadaka iliytoengenezwa kwa moto, ili kutoa harufu nzuri kwa BWANA. Atafanya kama mnavyofanya.
15 Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hii ni amri ya kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele za Bwana:
Kutakuwa na sheria hiyo hiyo kwa watu wote na kwa mgeni anayeishi kati yenu, sheria ya kudumu kwa watu wote wa uzao wako. Ninyi mlivyo, ndivyo atakavyokuwa mgeni aliyeishi kati yenu. Atafanya kama mnavyofanya mbele ya BWANA.
16 Sheria hizo hizo na masharti hayo hayo hayo, yatawahusu ninyi na mgeni aishiye miongoni mwenu.’”
Sheria na amri hiyohiyo ndiyo itakayotumika kwa mgeni anayeishi kati yenu.”
17 Bwana akamwambia Mose,
Tena BWANA akanena na Musa, akasema,
18 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapeleka
“Nena wana wa Israeli uwaambie, 'mtakapofika katika nchi ninayowapeleka,
19 nanyi mkala chakula cha nchi hiyo, toeni sehemu ya chakula hicho kama sadaka kwa Bwana.
mtakapokula chakula kinachozalishwa katika nchi hiyo, mtatoa sadaka ya kunipendeza mimi.
20 Toeni andazi kutoka kwa malimbuko ya chakula chenu kitokacho katika ardhi, na mkitoe kama sadaka kutoka sakafu ya kupuria nafaka.
Kutoka kwenye mikate yenu ya kwanza mtatoa mkate wa kuinuliwa kama sadaka iliyoinuliwa kutoka mahali pa kupuria nafaka. Mtaiinua kwa jinsi hii.
21 Kwa vizazi vyote vijavyo hamna budi kutoa sadaka hii kwa Bwana kutoka kwa malimbuko ya unga wenu.
Watu wa uzao wako wote wtanitolea sadaka ya kuinuliwa kutoka kwenye unga wenu wa kwanza.
22 “‘Basi kama pasipo kukusudia umeshindwa kushika mojawapo katika amri hizi ambazo Bwana alimpa Mose,
Wakati mwingine mtafanya dhambi pasipo kukusudia, Kama hamtatii amri zote hizi ambazo nimemwambia Musa
23 amri yoyote ya Bwana kwenu kupitia Mose, tangu siku ile Bwana alipowapa na inaendelea hadi vizazi vyote vijavyo;
-kila kitu ambacho nimewaamuru kupitia Musa kuanzia siku ambayo nilianza kuwaamuru na kuendelea kwa watu wote wa uzao wako.
24 ikiwa hili limefanyika pasipo kukusudia bila jumuiya kuwa na habari nalo, basi jumuiya yote itatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa ikiwa harufu nzuri inayompendeza Bwana, pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji zilizoamriwa kwayo, na mbuzi dume kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
Kwa swala la dhambi isiyokusudiwa ambayo watu wote hawaijui, basi watu wote watatoa fahari mchanga sadaka ya kuteketezwa ili kufanya harufu nzuri kwa BWANA. Pamoja na haya yote, lazima itengenezwe sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji, kama ilivyoagaizwa katika amri, na beberu mmoja kuwa sadaka ya dhambi.
25 Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Kiisraeli, nao watasamehewa, kwa kuwa haikuwa makusudi nao wamemletea Bwana sadaka iliyoteketezwa kwa moto na sadaka ya dhambi kwa ajili ya kosa lao.
Kuhani atafanya sadaka upatanisho kwa watu wote wa Israeli. Watasemehewa kwa sababu dhambi haikukusudiwa. Wametoa sadaka yao, sadaka iliyotengenezwa kwa moto kwa ajili yangu. Wameleta sadaka yao kwangu iliyotengenezwa kwa moto. Wameleta sadaka yao ya uovu mbele yangu kwa ajili ya kosa lao.
26 Jumuiya yote ya Kiisraeli pamoja na wageni waishio miongoni mwao watasamehewa, kwa sababu watu wote walihusika katika kosa lile lisilokusudiwa.
Ndipo watu wote wa Israeli watasamehewa, pia wageni wote wanaoishi kati yao, kwa sababu watu wote walitenda dhambi pasipo kukusudia.
27 “‘Lakini kama mtu mmoja peke yake akitenda dhambi pasipo kukusudia, ni lazima alete mbuzi mke wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
Kama mtu atatenda dhambi bila kukusudia, atatoa mbuzi jike wa umri wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya dhambi.
28 Kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya yule aliyekosa kwa kufanya dhambi pasipo kukusudia, upatanisho utakapofanywa kwa ajili yake, atasamehewa.
Naye kuhani atafanya upatanisho kwa BWANA kwa ajili ya mtu yule aliyefanya dhambi pasipo kukusudia. Yule mtu atasamehewa baada ya upatanisho kufanyika.
29 Sheria hiyo moja itamhusu kila mmoja ambaye ametenda dhambi pasipo kukusudia, awe Mwisraeli mzawa ama mgeni.
Mtakuwa na sheria hiyohiyo kwa mtu yeyote anayefanya dhambi hiyo pasipo kukusudia, sheria hiyohiyo hata kwa mzawa wa Isreli na kwa wageni wanaoishi kati yao.
30 “‘Lakini yeyote ambaye amefanya dhambi kwa dharau awe mzawa au mgeni, anamkufuru Bwana, naye mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
Lakini mtu afanyaye chochote kwa KUkusudia, awe mzawa au mgeni, ananikufuru mimi. Huyo mtu ataondolewa kati ya watu wake.
31 Kwa sababu amelidharau neno la Bwana na kuvunja amri zake, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali; hatia yake inabaki juu yake.’”
Kwa sababu atakuwa amedharau neno langu na amevunja neno amri yangu, mtu huyo ataondolewa kabisa. Dhambi yake itakuwa juu yake.'”
32 Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato.
Wakati wana wa Israeli walipokuwa katika jangwa, wakamuona mwanamume akikusanya kuni sikiu ya Sabato.
33 Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Mose, Aroni na kusanyiko lote,
Wale waliomwona wakamleta kwa Musa, Haruni na kwa watu wote.
34 nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini.
Wakamweka kifungoni kwa sababu ilikuwa haijaamuliwa atakachotendewa.
35 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima limpige mawe nje ya kambi.”
Kisha BWANA akanena na Musa, “Yule mwanamume lazima auawe. Watu wote lazima wampige kwa mawe nje ya kambi.”
36 Hivyo kusanyiko likamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kama Bwana alivyomwamuru Mose.
Kwa hiyo watu wote wakamtoa nje ya kambi nao wakampiga kwa mawe mpaka akafa kama vile BWANA alivyokuwa amemwamuru Musa.
37 Bwana akamwambia Mose,
BWANA akanena na Musa tena, akasema,
38 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo.
“Waambie wana wa Israeli na uwaamuru wajifanyie vishada wavining'inize katika mapindo ya mavazi yao, wavining'ineze katika ncha zote kwa nyuzi za rangi ya samawi. Watu wote watafanya hivi kwa watu wote wa kizazi chote.
39 Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Bwana, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu.
Huu utakuwa ukumbusho maalumu kwenu, kila mtakapovitazama, mtakumbuka amri zangu, na kuzishika ili kwamba msije mkatangatanga katika mioyo na macho yenu na kuwa waasherati wa hayo.
40 Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu.
Fanyeni hivi ili kwamba mweze kukumbuka na kutii amri zangu zote, na ili kwamba mpate kuwa watakatifu, waliotunzwa kwa ajili yangu, Mungu wenu.
41 Mimi Ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi Ndimi Bwana Mungu wenu.’”
Mimi ndimi BWANA Mungu wenu niliyekutoa toka nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu.”

< Hesabu 15 >