< Hesabu 15 >
1 Bwana akamwambia Mose,
2 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Baada ya ninyi kuingia katika nchi ninayowapa kama nyumbani,
3 nanyi mkitoa sadaka za kuteketezwa kwa moto, kutoka makundi ya ngʼombe au kondoo, kama harufu nzuri inayompendeza Bwana, ikiwa ni sadaka za kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum ama sadaka ya hiari au sadaka ya sikukuu zenu,
4 ndipo yeye aletaye sadaka yake ataiweka mbele za Bwana sadaka ya nafaka, sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta.
5 Pamoja na kila mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, andaa robo ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji.
6 “‘Pamoja na kondoo dume andaa sadaka ya nafaka ya sehemu mbili za kumi za efa za unga laini uliochanganywa na theluthi moja ya hini ya mafuta,
7 na theluthi moja ya hini ya divai kama sadaka ya kinywaji. Vitoe kama harufu nzuri inayompendeza Bwana.
8 “‘Unapoandaa fahali mchanga kama sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, kwa ajili ya nadhiri maalum au sadaka ya amani kwa Bwana,
9 leta pamoja na huyo fahali sadaka ya nafaka ya unga laini sehemu tatu za kumi za efa uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.
10 Pia utaleta nusu ya hini ya divai kama sadaka ya kinywaji. Itakuwa sadaka iliyoteketezwa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana.
11 Kila fahali au kondoo dume, kila mwana-kondoo au mbuzi mchanga, atatayarishwa kwa njia hii.
12 Fanyeni hivi kwa ajili ya kila mmoja, kwa kadiri ya wingi wa mtakavyoandaa.
13 “‘Kila mmoja ambaye ni mzawa ni lazima afanye vitu hivi kwa njia hii hapo aletapo sadaka ya kuteketezwa kwa moto kama harufu nzuri inayompendeza Bwana.
14 Kwa vizazi vijavyo, wakati wowote mgeni au mtu mwingine yeyote anayeishi miongoni mwenu aletapo sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu nzuri ya kumpendeza Bwana, ni lazima afanye sawasawa kabisa na jinsi mnavyofanya ninyi.
15 Jumuiya itakuwa na sheria hizo hizo kwenu na kwa mgeni aishiye miongoni mwenu; hii ni amri ya kudumu kwa vizazi vijavyo. Ninyi na mgeni mtakuwa sawa mbele za Bwana:
16 Sheria hizo hizo na masharti hayo hayo hayo, yatawahusu ninyi na mgeni aishiye miongoni mwenu.’”
17 Bwana akamwambia Mose,
18 “Sema na Waisraeli na uwaambie: ‘Mtakapoingia katika nchi ninayowapeleka
19 nanyi mkala chakula cha nchi hiyo, toeni sehemu ya chakula hicho kama sadaka kwa Bwana.
20 Toeni andazi kutoka kwa malimbuko ya chakula chenu kitokacho katika ardhi, na mkitoe kama sadaka kutoka sakafu ya kupuria nafaka.
21 Kwa vizazi vyote vijavyo hamna budi kutoa sadaka hii kwa Bwana kutoka kwa malimbuko ya unga wenu.
22 “‘Basi kama pasipo kukusudia umeshindwa kushika mojawapo katika amri hizi ambazo Bwana alimpa Mose,
23 amri yoyote ya Bwana kwenu kupitia Mose, tangu siku ile Bwana alipowapa na inaendelea hadi vizazi vyote vijavyo;
24 ikiwa hili limefanyika pasipo kukusudia bila jumuiya kuwa na habari nalo, basi jumuiya yote itatoa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa ikiwa harufu nzuri inayompendeza Bwana, pamoja na sadaka ya nafaka na ya kinywaji zilizoamriwa kwayo, na mbuzi dume kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
25 Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Kiisraeli, nao watasamehewa, kwa kuwa haikuwa makusudi nao wamemletea Bwana sadaka iliyoteketezwa kwa moto na sadaka ya dhambi kwa ajili ya kosa lao.
26 Jumuiya yote ya Kiisraeli pamoja na wageni waishio miongoni mwao watasamehewa, kwa sababu watu wote walihusika katika kosa lile lisilokusudiwa.
27 “‘Lakini kama mtu mmoja peke yake akitenda dhambi pasipo kukusudia, ni lazima alete mbuzi mke wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
28 Kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya yule aliyekosa kwa kufanya dhambi pasipo kukusudia, upatanisho utakapofanywa kwa ajili yake, atasamehewa.
29 Sheria hiyo moja itamhusu kila mmoja ambaye ametenda dhambi pasipo kukusudia, awe Mwisraeli mzawa ama mgeni.
30 “‘Lakini yeyote ambaye amefanya dhambi kwa dharau awe mzawa au mgeni, anamkufuru Bwana, naye mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
31 Kwa sababu amelidharau neno la Bwana na kuvunja amri zake, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali; hatia yake inabaki juu yake.’”
32 Waisraeli walipokuwa jangwani, mtu mmoja alikutwa akikusanya kuni siku ya Sabato.
33 Wale waliomkuta akikusanya kuni wakamleta kwa Mose, Aroni na kusanyiko lote,
34 nao wakamweka kifungoni, kwa sababu haikufahamika kwa wazi kwamba afanyiwe nini.
35 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Huyo mtu ni lazima afe. Kusanyiko lote lazima limpige mawe nje ya kambi.”
36 Hivyo kusanyiko likamtoa nje ya kambi na kumpiga mawe hadi akafa, kama Bwana alivyomwamuru Mose.
37 Bwana akamwambia Mose,
38 “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo.
39 Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Bwana, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu.
40 Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu.
41 Mimi Ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa Misri niwe Mungu wenu. Mimi Ndimi Bwana Mungu wenu.’”