< Hesabu 12 >

1 Miriamu na Aroni walianza kuzungumza dhidi ya Mose kwa sababu ya mke wake Mkushi, kwa kuwa alikuwa ameoa Mkushi.
Kisha Miriamu na Haruni wakasema kinyume na Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi ambaye alikuwa amemwoa.
2 Waliuliza, “Je, Bwana amesema kupitia Mose peke yake? Je, hajasema kutupitia sisi pia?” Naye Bwana akasikia hili.
Walisema. “Hivi BWANA amesema na Musa tu? Ni kweli hajawahi kusema nasi pia? Sasa BWANA akasikia kile walichokuwa wanaongea. Sasa
3 (Basi Mose alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine yeyote katika uso wa dunia.)
Musa alikuwa mtu mpole sana, mpole kuliko mtu yeyote duniani.
4 Ghafula Bwana akawaambia Mose, Aroni na Miriamu, “Njooni katika Hema la Kukutania, ninyi nyote watatu.” Kwa hiyo wote watatu wakaenda.
Wakati huo, BWANA akanena na Musa, Haruni na Miriamu: “tokeni nje ninyi watatu kwenye hema ya kukutania.” kwa hiyo wale watatu wakatokanje.
5 Kisha Bwana akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye ingilio la Hema, akawaita Aroni na Miriamu. Wakati wote wawili waliposogea mbele,
Kisha BWANA akashuka katika nguzo ya wingu. Akasimama kwenye lango la hema na akamwita Haruni na Miriamu. wote wakaja mbele.
6 Bwana akasema, “Sikilizeni maneno yangu: “Akiwapo nabii wa Bwana miongoni mwenu, nitajifunua kwake kwa maono, nitanena naye katika ndoto.
BWANA akasema, “Sasa sikilizeni maneo yangu, Nabii wangu anapokuwa nanyi, Mimi nitajifunua kwake kwa maono na kusema naye katika ndoto.
7 Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Mose; yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.
Lakini si hivyo kwa mtumishi wangu Musa. Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.
8 Kwake nitanena naye uso kwa uso, waziwazi wala si kwa mafumbo; yeye ataona umbo la Bwana. Kwa nini basi ninyi hamkuogopa kuzungumza kinyume cha mtumishi wangu Mose?”
Mimi huongea na Musa moja kwa moja, si kwa maono wala mafumbo. Yeye huniona umbo langu. Kwa hiyo, kwa nini hamuogoopi kumnenea kinyume, mtumishi wangu Musa?”
9 Hasira ya Bwana ikawaka dhidi yao, akawaacha.
Hasira ya BWANA ikawawakia, kisha akawaacha.
10 Wakati hilo wingu liliinuka kutoka juu ya Hema, Miriamu akawa tayari ana ukoma, mweupe kama theluji. Aroni akamgeukia, akaona ana ukoma.
Lile wingu likainuka juu ya hema, Miriamu akapata ukoma ghafla - akawa mweupe kama theluji. Naye Haruni alipogeuka kumwona Miriamu, akamwona amepata ukoma.
11 Kisha Aroni akamwambia Mose, “Tafadhali, bwana wangu, usituhesabie dhambi hii ambayo tumeifanya kwa upumbavu.
Haruni akamwambia Musa, “Bwana wangu, usituadhibu kwa uovu wetu huu. Tumenena katka upumbuvu, na tumetenda dhambi.
12 Usimwache awe kama mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa mfu, ambaye nusu ya mwili wake imeharibika hapo atokapo katika tumbo la mama yake.”
Tafadhali nakuomba usimwache akawa kama mtoto mchanga aliyekufa ambaye nusu ya nyama yake imeoza tangu kuzaliwa”
13 Hivyo Mose akamlilia Bwana akisema, “Ee Mungu, nakuomba umponye!”
Kwa hiyo Musa akamwomba BWANA, akasema, “Mungu ninakusihi umponye tafadhali.”
14 Bwana akamjibu Mose, “Je, kama baba yake angemtemea usoni, asingeona aibu kwa siku saba? Mfungie nje ya kambi kwa siku saba; baada ya hapo anaweza kurudishwa kambini.”
BWANA akamwambia Musa, “kama baba yake angemtemea usoni angepata aibu kwa muda wa siku saba. Umfungie nje ya kambi kwa muda wa siku saba. Kisha umrejeshe ndani tena.”
15 Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba, nao watu hawakuendelea na safari mpaka aliporudishwa kambini.
Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba. Watu hawakusafiri mpaka aliporudi kambini.
16 Baada ya hayo, watu waliondoka Haserothi, wakapiga kambi katika Jangwa la Parani.
Kisha watu wakasafiri kutoka Hazeroti na kuweka kambi kwenye jangwa la Parani.

< Hesabu 12 >