< Hesabu 11 >

1 Basi watu wakalalamika kwa habari ya taabu zao masikioni mwa Bwana, naye alipowasikia, hasira yake ikawaka. Ndipo moto kutoka kwa Bwana ukawaka miongoni mwao na kuteketeza baadhi ya viunga vya kambi.
Sasa watu wakanung'unika juu ya matatizo yao wakati BWANA alipokuwa akiwasikiliza. BWANA akawasikia watu naye akakasirika. Moto kutoka kwa BWANA ukashuka na ukawaka kati yao na kuteketeza baadhi ya kambi kwenye pembe zake.
2 Watu walipomlilia Mose, akamwomba Bwana, nao moto ukazimika.
Ndipo watu wakamwita Musa kwa nguvu, Naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukazimika.
3 Hivyo mahali pale pakaitwa Tabera, kwa sababu moto kutoka kwa Bwana uliwaka miongoni mwao.
Mahali pale paliitwa Tabera, kwa sababu moto wa BWANA uliwaka kati yao.
4 Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule!
Baadhi ya wageni wakaanza kuweka kambi zao pamoja na wana wa wa Israeli. Walitaka kula chakula kizuri. Kisha wana wa Israeli walipoanza kulia wakisema, “Ni nani atakayetupatia nyama za kula?
5 Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu.
Tunakumbuka samaki tulizokula bure kule Misri, yale matango, na matikiti maji, na mboga na vitunguu na vitunguu saumu.
6 Lakini sasa tumepoteza hamu ya chakula; hatuoni kitu kingine chochote isipokuwa hii mana!”
Na sasa hatuna hamu ya kula, kwa sababu tunaona mana tu.
7 Mana ilifanana kama mbegu za giligilani, nayo ilikuwa na rangi ya manjano iliyopauka.
Mana ilifanana na punje ya mtama. ilionekana kama bedola.
8 Hao watu walikwenda kukusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia ya mkono au kuitwanga kwenye vinu. Waliipika vyunguni au kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama kitu kilichotengenezwa kwa mafuta ya zeituni.
watu wakazunguka kisha wakakusanyika. Wakaisaga, wakaitwanga kwa vinu, wakaitokosa nyunguni, na kuitengeneza mikate. radha yake ilikuwa kama mafuta mapya ya mizeituni.
9 Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, pia mana ilianguka pamoja nao.
Na umande ulipoanguka kambini usiku ule, na mana ilianguka pia.
10 Mose akasikia watu wa kila jamaa wakilia, kila mmoja kwenye mlango wa hema lake. Bwana akakasirika mno, naye Mose akafadhaika.
Musa akawasikia watu wakilia katika familia zao, na kila mtu alikuwa kwenye lango la hema yake. BWANA alikasirika sana, na mbele ya macho ya Musa malalamiko yao yalikuwa mabaya.
11 Akamuuliza Bwana, “Kwa nini umeleta taabu hii juu ya mtumishi wako? Nimekufanyia nini cha kukuchukiza hata ukaweka mzigo huu wa watu hawa wote juu yangu?
Musa akasema na BWANA, “Kwa nini umemtendea mtumishi wako vibaya namna hiyo? kwa nini hujapendezwa na mimi? unanifanya kubeba mizigo ya hawa watu.
12 Je, watu hawa wote mimi ndiye niliyewatungisha mimba? Je, ni mimi niliyewazaa? Kwa nini unaniambia niwachukue mikononi mwangu, kama vile mlezi abebavyo mtoto mchanga, hadi kwenye nchi uliyowaahidi baba zao?
Je, mimi ndiye niliyewatungia mimba hawa watu? Mimi ndiye niliyewazaa kiasi kwamba unaniambia, “wabebe kwa ukaribu vifuani mwako kama baba abebavyo mtoto wake? Je, nitawabeba mpaka kwenye nchi ambayo uliwaahidi mababu zao kuwapa?
13 Nitapata wapi nyama kwa ajili ya watu wote hawa? Wanaendelea kunililia wakisema, ‘Tupe nyama tule!’
Naweza kupata wapi nyama za kuwapa watu wote hawa? Wanalia mbele zangu na wanasema, 'tupe nyama tule.'
14 Mimi siwezi kuwabeba watu hawa wote peke yangu, mzigo ni mzito sana kwangu.
Mimi peke yangu siwezi kuwabeba watu wote hawa. Ni wengi sana kwangu.
15 Kama hivi ndivyo unavyonitendea, uniue sasa hivi, yaani kama nimepata kibali machoni pako, wala usiniache nione maangamizi yangu mwenyewe.”
Kwa vile unanitendea hivi, basi uniue, na kama wewe ni mpole kwangu, basi niondolee mzigo huu.”
16 Bwana akamwambia Mose: “Niletee wazee sabini wa Israeli, unaowafahamu kama viongozi na maafisa miongoni mwa watu. Walete katika Hema la Kukutania, ili waweze kusimama huko pamoja nawe.
BWANA akamwambia Musa, “Niletee wazee sabini miongoni mwa Waisraeli. Hakikisha ni wazee na viongozi wa watu. Uwalete kwenye hema ya kukutania wasimame pamoja na wewe.
17 Nami nitashuka na kusema nawe huko. Nami nitachukua sehemu ya Roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao. Watakusaidia kubeba mzigo wa watu hao ili usije ukaubeba peke yako.
Nami nitashuka niseme nawe mahali pale. Nitatoa sehemu ya roho iliyo ndani yako na kuwapatia wao. Nao watabeba mzigo wa watu pamoja nawe. na hautaubeba peke yako.
18 “Waambie hao watu: ‘Jiwekeni wakfu wenyewe kwa ajili ya kesho, wakati mtakapokula nyama. Bwana aliwasikia mlipolia, mkisema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tulikuwa na hali nzuri zaidi katika nchi ya Misri!” Sasa Bwana atawapa nyama, nanyi mtaila.
Waambie watu, 'Jitakaseni ninyi wenyewe, kwa kuwa kesho mtakuala nyama, kwa kuwa mmelia na BWANA amesikia, “Mlipokuwa mkisema kuwa nani atakayetupa nyama tule? Kule Misri tulikula chakula kizuri!” Kwa hiyo BWANA atawapeni nyama, nanyi mtakula nyama.
19 Hamtaila kwa siku moja tu, au siku mbili, au tano, kumi au siku ishirini,
Hamtakula nyama kwa siku moja tu, au siku mbili, au siku tano, au siku kumi, au siku ishirini,
20 bali kwa mwezi mzima mpaka iwatokee puani, nanyi mtaichukia kabisa, kwa kuwa mmemkataa Bwana, ambaye yupo miongoni mwenu, nanyi mmelia mbele zake, mkisema, “Hivi kwa nini tulitoka Misri?”’”
Lakini mtakula nyama kwa mwezi mmoja mpaka zitakapowatokea puani. Mpaka zitawakinai kwa sababu mmemkataa BWANA ambaye yuko kati yenu. Mmelia mbele yake. mmesema, “Kwa nini tulitoka Misri?””
21 Lakini Mose alisema, “Mimi niko hapa miongoni mwa watu 600,000 wanaotembea kwa miguu, nawe umesema, ‘Nitawapa nyama ya kula kwa mwezi mzima!’
Kisha Musa akasema, “Mimi nina watu 600, 000, na wewe umesema, “Nitawapa nyama mle kwa mwezi mmoja,'
22 Je, wangeweza kupata nyama ya kuwatosha hata kama makundi ya kondoo na ya ngʼombe yangechinjwa kwa ajili yao? Je, wangetosheka hata kama samaki wote wa baharini wangevuliwa kwa ajili yao?”
Je, tutayachinja haya makundi ya ng'ombe na kondoo ili kuwatosheleza?”
23 Bwana akamjibu Mose, “Je, mkono wa Bwana ni mfupi sana? Sasa utaona kama jambo nililolisema litatimizwa kwa ajili yako au la.”
BWANA akasema na Musa, “Je mkono wangu ni mfupi? Sasa utaona kama maneno yangu ni ya kweli ama sivyo.
24 Kwa hiyo Mose akatoka na kuwaambia watu lile ambalo Bwana alikuwa amesema. Akawakusanya wazee wao sabini, akawasimamisha kuzunguka Hema.
Musa alitoka nje kwenda kuwaambia watu maneno ya BWANA. Aliwakusanya wazee sabini wa watu na kuwaweka kuizunguka hema.
25 Kisha Bwana akashuka katika wingu na kunena na Mose, naye akachukua sehemu ya Roho iliyokuwa juu ya Mose na kuiweka juu ya wale wazee sabini. Roho aliposhuka juu yao, wakatoa unabii, lakini hawakufanya hivyo tena.
BWANA akashuka chini katika wingu akaongea na Musa. BWANA akachukua sehemu ya roho iliyokuwa kwa Musa na kuiweka kwa wale wazee sabini. Roho alipowashukia, wakaanza kutoa unabii, lakini ilitokea kwenye tukio hilo tu na haikujirudia tena.
26 Lakini, watu wawili, ambao majina yao ni Eldadi na Medadi, walibaki kambini. Walikuwa wameorodheshwa miongoni mwa wale wazee sabini, lakini hawakutoka kwenda kwenye Hema. Lakini Roho pia alishuka juu yao, nao wakatabiri huko kambini.
Watu wawili waitwao Elidadi na Medadi walibaki kambini. Lakini Roho aliwashukia pia. Majina yao yalikuwa yameandikwa kwenye orodha lakini walikuwa hawajaenda hemani. Hata hivyo nao walitoa unabii wakiwa kambini.
27 Mwanaume mmoja kijana alikimbia na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”
Kijana mmoja huko kambini alikimbia akaenda kumwambia Musa, “Elidadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”
28 Yoshua mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akajibu akasema, “Mose bwana wangu, wanyamazishe!”
Joshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Musa, ambaye ni miongoni mwa wale aliowachagua akamwambia Musa, “Bwana wangu Musa, wazuie.”
29 Lakini Mose akajibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Ningetamani watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kwamba Bwana angeweka Roho yake juu yao!”
Musa akamwambia, “una wivu kwa niaba yangu? Natamani kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kwamba angeweka Roho yake juu yao wote!”
30 Ndipo Mose na wale wazee wa Israeli wakarudi kambini.
Kisha Musa na wale wazee wakarudi kambini.
31 Kisha ukatokea upepo kutoka kwa Bwana, nao ukawaletea kware kutoka baharini. Ukawaangusha kwenye eneo lote linalozunguka kambi na kujaa ardhini kimo cha mita moja hivi kutoka ardhini kwenye eneo la umbali wa mwendo wa siku moja kila upande.
Kisha upepo ukavuma kutoka kwa BWANA ukaja na kware kutokea baharini. Wakaanguka karibu na kambi, kiasi cha umbali wa safari ya siku moja upande huu na umbali wa siku moja upande mwingine. Wale kware wakaizunguka kambi kiasi cha mita moja toka uso wa dunia.
32 Mchana kutwa na usiku kucha pamoja na siku nzima iliyofuata watu walitoka kwenda kuokota kware. Hakuna mtu yeyote aliyekusanya chini ya homeri kumi. Kisha wakazianika kuzunguka kambi yote.
Watu wakawakusanya hao kware kwa bidii mchana huo wote na usiku huo wote, na mchana wote uliofuatia. Hakuna aliyekusanya pungufu ya mita mbili za uajazo. Wakawaanika kweye ardhi yote hapo kambini.
33 Lakini walipokuwa wakila nyama, ilipokuwa ingali kati ya meno yao na kabla hawajamaliza kula, hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya watu, naye akawapiga kwa tauni.
Wakati ile nyama ikiwa bado iko kwenye meno yao, wakiwa bado wanatafuna, BWANA akawakasirikia. Akwapiga watu wale kwa gonjwa kubwa sana.
34 Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Kibroth-Hataava, kwa sababu huko ndiko walipowazika watu ambao walitamani sana chakula kingine.
Mahali pale paliitwa Kibroti Hataava, kwa sababu pale walizika watu waliotamani nyama.
35 Kutoka Kibroth-Hataava watu wakasafiri mpaka Haserothi na kukaa huko.
Kutoka Kibroti Hataava watu wakasafiri hadi Hazeroti, ambapo walipumzika.

< Hesabu 11 >