< Nehemia 9 >

1 Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa nguo za gunia na kujitia mavumbi vichwani mwao.
Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo huo watu wa Israeli walikusanyika, nao walikuwa wamefunga, nao walikuwa wamevaa magunia, nao wakaweka vumbi juu ya vichwa vyao.
2 Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao.
Wazao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Walisimama na kukiri dhambi zao wenyewe na matendo maovu ya baba zao.
3 Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Bwana Mungu wao kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu Bwana Mungu wao.
Walisimama mahali pao, na robo ya siku walisoma kutoka Kitabu cha Sheria ya Bwana Mungu wao. Na robo nyingine ya siku walikiri na kuinama mbele ya Bwana Mungu wao.
4 Walawi wafuatao walikuwa wamesimama kwenye ngazi: Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Hawa walimlilia Bwana Mungu wao kwa sauti kubwa.
Walawi, Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebaniya, Buni, Sherebia, Bani na Kenani, walisimama juu ya ngazi, wakamwita Bwana, Mungu wao kwa sauti kubwa.
5 Nao Walawi Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabnea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakasema: “Simameni mkamsifu Bwana Mungu wenu, yeye ambaye ni Mungu tangu milele hata milele. “Libarikiwe jina lake tukufu, litukuzwe juu ya baraka zote na sifa.
Ndipo Walawi, na Yeshua, na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethalia, wakasema, “Simameni, mkamsifu Bwana, Mungu wenu, milele na milele.” “Libarikiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.
6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.
Wewe ni Bwana. Wewe peke yako. Wewe umefanya mbinguni, mbingu za juu, na malaika wote wa vita vita, na dunia na kila kitu kilicho juu yake, na bahari na vyote vilivyomo. Unawapa wote uzima, na majeshi ya malaika wanakusujudia.
7 “Wewe ni Bwana Mungu uliyemchagua Abramu na kumtoa kutoka Uru ya Wakaldayo, nawe ukamwita Abrahamu.
Wewe ndiwe Bwana, Mungu aliyemchagua Abramu, akamtoa kutoka Uri wa Wakaldayo, akamwita Ibrahimu.
8 Uliona kuwa moyo wake ni mwaminifu kwako, nawe ukafanya Agano naye kuwapa wazao wake nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi. Umetimiza ahadi yako kwa sababu wewe ni mwenye haki.
Uliona moyo wake ulikuwa mkamilifu mbele yako, nawe ukafanya pamoja naye agano la kuwapa wazao wake nchi ya Wakanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Perizi, na Myebusi, na Wagirgashi. Umeweka ahadi yako kwa sababu wewe ni mwenye haki.
9 “Uliona mateso ya baba zetu huko Misri, ukasikia kilio chao huko Bahari ya Shamu.
Uliona shida ya baba zetu Misri na ukasikia kilio chao kando ya bahari ya shamu.
10 Ulituma ishara za miujiza na maajabu dhidi ya Farao, dhidi ya maafisa wake wote na watu wote wa nchi yake, kwa kuwa ulifahamu jinsi Wamisri walivyowafanyia ufidhuli. Ukajifanyia jina linalodumu hadi leo.
Wewe ulifanya ishara na maajabu juu ya Farao, na watumishi wake wote, na watu wote wa nchi yake, kwa maana ulijua kwamba Wamisri walifanya kwa kujivunia. Lakini ulijifanyia jina ambalo linasimama hadi siku leo.
11 Ukagawa bahari mbele yao, ili waweze kupita katikati yake penye nchi kavu, lakini uliwatupa Wamisri waliowafuatilia katika vilindi, kama jiwe kwenye maji mengi.
Ukagawanya bahari mbele yao, wakavuka katikati ya bahari juu ya nchi kavu; na ukawatupa wale waliowa ndani ya kina, kama jiwe ndani ya maji ya kina.
12 Mchana uliwaongoza kwa nguzo ya wingu, na usiku kwa nguzo ya moto kuwamulikia njia iliyowapasa kuiendea.
Wewe uliwaongoza kwa nguzo ya wingu wakati wa mchana, na kwa nguzo ya moto wakati wa usiku, ili kuwamulikia njiani waweze kutembea katika nuru yake.
13 “Ulishuka katika Mlima Sinai, ukanena nao kutoka mbinguni. Uliwapa masharti na sheria zile ambazo ni za kweli na haki, pia amri na maagizo mazuri.
Ulishuka juu ya Mlima Sinai ukazungumza nao kutoka mbinguni ukawapa amri za haki na sheria za kweli, amri nzuri na maagizo.
14 Uliwafahamisha Sabato yako takatifu na ukawapa amri, maagizo na sheria kupitia mtumishi wako Mose.
Uliwajulisha sabato yako takatifu, ukawapa amri, maagizo, na sheria kupitia Musa mtumishi wako.
15 Katika njaa yao uliwapa mkate kutoka mbinguni, na katika kiu yao uliwatolea maji kutoka kwenye mwamba. Uliwaambia waingie na kuimiliki nchi ambayo ulikuwa umeapa kuwapa kwa mkono ulioinuliwa.
Uliwapa chakula kutoka mbinguni kwa ajili ya njaa yao, na maji kutoka mwamba kwa kiu yao, ukawaambia waende kuimiliki nchi uliyowaapa kwa kiapo kuwapa.
16 “Lakini wao, baba zetu, wakawa na kiburi na shingo ngumu, nao hawakutii maagizo yako.
Lakini wao na baba zetu walifanya uasi, nao walikuwa wakaidi, wala hawakuzitii amri zako.
17 Wakakataa kusikiliza na kushindwa kukumbuka miujiza uliyoifanya miongoni mwao. Wakawa na shingo ngumu, na katika uasi wao wakamchagua kiongozi ili warudi kwenye utumwa wao. Lakini wewe ni Mungu mwenye kusamehe, mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo. Kwa hiyo hukuwaacha,
Walikataa kusikiliza, na hawakufikiri juu ya maajabu uliyofanya kati yao, lakini wakawa wakaidi, na katika uasi wao waliweka kiongozi ili wairudie hali ya utumwa. Lakini wewe ni Mungu ambaye amejaa msamaha, mwenye rehema na huruma, si mwepesi wa hasira, na wingi katika upendo thabiti. Wewe haukuwaacha.
18 hata wakati walijitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu na kusema, ‘Huyu ni mungu wenu, aliyewapandisha kutoka nchi ya Misri,’ au walipofanya makufuru makubwa.
Wala hukuwaacha hata walipokwisha kutoa ndama katika chuma kilichochomwa na kusema, “Huyu ndio Mungu wenu aliyekuleta kutoka Misri,” wakati walipopotoka sana.
19 “Kwa sababu ya huruma zako kuu hukuwaacha jangwani. Wakati wa mchana ile nguzo ya wingu haikukoma kuwaongoza katika njia yao, wala nguzo ya moto haikuacha kuwamulikia usiku njia iliyowapasa kuiendea.
Wewe, kwa huruma yako, hukuwaacha katika jangwa. Nguzo ya wingu iliyowangoza njiani haikuwaacha wakati wa mchana, wala nguzo ya moto usiku iliwaangazia barabara ambayo walipaswa kutembea.
20 Uliwapa Roho wako mwema ili kuwafundisha. Hukuwanyima mana yako vinywani mwao, nawe ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.
Uliwapa Roho wako mzuri kuwafundisha, na mana yako haukuwanyima kinywani mwao, na ukawapa maji kwa kiu yao.
21 Kwa miaka arobaini uliwatunza jangwani. Hawakukosa chochote, na nguo zao hazikuchakaa wala miguu yao haikuvimba.
Kwa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, na hawakukosa chochote. Nguo zao hazikuchakaa na miguu yao haikuvimba.
22 “Uliwapa falme na mataifa, ukiwagawia hata mipaka ya mbali. Wakaimiliki nchi ya Sihoni mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani.
Uliwapa falme na watu, na ukawapa ardhi katika kila kona ya mbali. Basi wakaimiliki nchi ya Sihoni mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani.
23 Uliwafanya wana wao kuwa wengi kama nyota za angani, nawe ukawaleta katika nchi ambayo uliwaambia baba zao kuingia na kuimiliki.
Uliwafanya watoto wao kuwa wengi kama nyota za mbinguni, na ukawaingiza katika nchi. Uliwaambia baba zao waingie na kumiliki.
24 Wana wao wakaingia na kuimiliki nchi. Uliwatiisha Wakanaani mbele yao, walioishi katika nchi, ukawatia Wakanaani mikononi mwao, pamoja na wafalme wao na watu wa nchi, wawafanyie kama wapendavyo.
Basi watu wakaingia, wakaimiliki nchi, ukawashinda wenyeji wa nchi hiyo, Wakanaani. Ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao na watu wa nchi, ili Israeli afanye nao kama walivyotaka.
25 Wakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
Wao waliteka miji yenye nguvu na nchi yenye ustawi, nao wakachukua nyumba zenye vitu vyote vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu na miti ya mizeituni, na miti ya matunda mengi. Kwa hiyo walikula na wakashiba na wakatosheka, na wakafurahi kwa wema wako.
26 “Lakini hawakukutii nao wakaasi dhidi yako, wakatupa sheria zako nyuma yao. Wakawaua manabii wako, waliowaonya ili wakurudie, na wakafanya makufuru makubwa.
Basi hawakukutii na wakawaasi. Walitupa sheria yako nyuma ya migongo yao. Waliwaua manabii wako waliowaonya wakurudie wewe, nao wakafanya ukatili mkubwa.
27 Hivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Kutoka mbinguni uliwasikia, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa waokozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.
Kwa hiyo ukawatia mikononi mwa adui zao, aliyewatesa. Na wakati wa mateso yao, walikulilia na wewe uliwasikia kutoka mbinguni na mara nyingi ukawaokoa katika mikono ya adui zao, kwa sababu ya huruma zako nyingi.
28 “Lakini mara walipokuwa na raha, wakafanya maovu tena machoni pako. Kisha ukawaacha mikononi mwa adui zao, nao wakawatawala. Walipokulilia tena, ukasikia kutoka mbinguni, na kwa huruma zako ukawaokoa kila mara.
Lakini baada ya kupumzika, wakafanya mabaya tena mbele yako, nawe ukawaacha mikononi mwa adui zao, kwa hiyo adui zao wakatawala juu yao. Hata walipokurudia na kukulilia, ukasikia kutoka mbinguni, mara nyingi ukawaokoa kwa sababu ya huruma yako.
29 “Ukawaonya warudi katika sheria yako, lakini wakawa na kiburi na hawakutii amri zako. Wakatenda dhambi dhidi ya maagizo yako ambayo kwayo mtu ataishi kama akiyatii. Kwa ukaidi wakakugeuzia kisogo, wakawa na shingo ngumu na wakakataa kusikiliza.
Uliwaonya ili wapate kurudi kwenye sheria yako. Hata hivyo walifanya kiburi na hawakusikiliza amri zako. Walifanya dhambi dhidi ya amri zako ambazo humpa uzima mtu yeyote anayezitii. Hawakuzitii, hawakuzitenda na walikataa kuzisikiliza.
30 Kwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao. Kwa njia ya Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani.
Kwa miaka mingi ukachukiliana nao na kuwaonya kwa Roho wako kwa njia ya manabii wako. Hata hivyo hawakusikiliza. Kwa hiyo ukawatia mikononi mwa watu wa jirani.
31 Lakini kwa rehema zako kuu hukuwakomesha wala kuwaacha, kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na rehema.
Lakini kwa huruma zako kubwa hukuwakomesha kabisa, au kuwaacha, kwa maana wewe ni Mungu mwenye rehema na mwenye huruma.
32 “Basi sasa, Ee Mungu wetu, uliye mkuu, mwenye nguvu na Mungu wa kuogofya, mwenye kushika agano lake la upendo, usiache taabu hizi zote zionekane kuwa kitu kidogo mbele za macho yako, taabu hizi zilizotupata, juu ya wafalme wetu na viongozi, juu ya makuhani wetu na manabii, juu ya baba zetu na watu wako wote, tangu siku za wafalme wa Ashuru hadi leo.
Basi, Mungu wetu, Mungu wetu mkuu, mwenye nguvu na mwenye kutisha, unayeweka agano lako na upendo wako, shida zote zilizotupata sisi, wafalme wetu, wakuu wetu, na makuhani wetu, na manabii wetu, na baba zetu, na watu wako wote tangu siku za wafalme wa Ashuru mpaka leo usizihesabu kuwa ni kidogo.
33 Katika hayo yote yaliyotupata, umekuwa mwenye haki, na umetenda kwa uaminifu, wakati sisi tumetenda mabaya.
Wewe ni mwenye haki katika yote yaliyotupata, kwa kuwa umetenda kwa uaminifu, na tumefanya uovu.
34 Wafalme wetu, viongozi wetu, makuhani wetu na baba zetu hawakufuata sheria yako. Hawakuzingatia amri zako wala maonyo uliyowapa.
Wafalme wetu, wakuu wetu, makuhani wetu, na baba zetu hawakuishika sheria yako, wala hawakuzingatia amri zako au shuhuda zako ulizowashuhudia.
35 Hata walipokuwa wangali katika ufalme wao, wakiufurahia wema wako mkuu katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa, hawakukutumikia wala kugeuka kutoka njia zao mbaya.
Hata katika ufalme wao wenyewe, wakati walifurahia wema wako kwao, katika nchi kubwa na yenye mazao uliyoweka mbele yao, hawakukutumikia au kuacha njia zao mbaya.
36 “Lakini tazama, sisi ni watumwa leo, watumwa katika nchi uliyowapa baba zetu ili wapate kula matunda yake na vitu vingine vizuri inayozalisha.
Sasa sisi ni watumwa katika nchi uliyowapa baba zetu kufurahia matunda yake na zawadi zake nzuri, na tazama, sisi ni watumwa!
37 Kwa sababu ya dhambi zetu, mavuno yake mengi huenda kwa wafalme uliowaweka watutawale. Wanatawala juu ya miili yetu na mifugo yetu kama wapendavyo. Tuko katika dhiki kuu.
Mavuno mazuri kutoka nchi yetu huenda kwa wafalme uliowaweka juu yetu kwa sababu ya dhambi zetu. Watawala juu ya miili yetu na juu ya mifugo kama wanavyopenda. Tuna shida kubwa.
38 “Kwa sababu ya haya yote, tunajifunga katika mapatano, na kuyaandika, nao viongozi wetu, Walawi wetu na makuhani wetu wanatia mihuri yao.”
Kwa sababu ya yote haya, tunafanya agano thabiti kwa kuandika. Kwenye hati iliyofungwa ni majina ya wakuu wetu, Walawi, na makuhani.”

< Nehemia 9 >