< Nehemia 11 >
1 Basi viongozi wa watu walikaa Yerusalemu, nao watu wale wengine walipiga kura ili kuleta mtu mmoja kati ya watu kumi aje kuishi Yerusalemu, mji mtakatifu, nao wengine tisa waliobaki wakae katika miji yao wenyewe.
2 Watu waliwasifu wale wote waliojitolea kuishi Yerusalemu.
3 Hawa ndio viongozi wa majimbo waliokuja kuishi Yerusalemu (baadhi ya Waisraeli, makuhani, Walawi, watumishi wa Hekalu, na wazao wa watumishi wa Solomoni waliendelea kuishi katika miji ya Yuda, kila mmoja katika milki yake mwenyewe katika miji mbalimbali,
4 ambapo watu wengine kutoka Yuda na Benyamini waliishi Yerusalemu). Kutoka wazao wa Yuda: Athaya mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli, mzao wa Peresi.
5 Naye Maaseya mwana wa Baruku, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, mzao wa Mshiloni.
6 Wazao wa Peresi walioishi Yerusalemu walikuwa 468, watu wenye uwezo.
7 Kutoka wazao wa Benyamini: Salu mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseya, mwana wa Ithieli, mwana wa Yeshaya
8 na wafuasi wake, Gabai na Salai watu 928.
9 Yoeli mwana wa Zikri alikuwa afisa wao mkuu, naye Yuda mwana wa Hasenua alikuwa msimamizi juu ya Mtaa wa Pili katika mji.
10 Kutoka makuhani: Yedaya, mwana wa Yoyaribu, Yakini,
11 Seraya mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, msimamizi katika nyumba ya Mungu,
12 pamoja na wenzao waliofanya kazi hekaluni: watu 822. Adaya mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amsi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya,
13 na wenzao, waliokuwa viongozi wa jamaa: watu 242. Amashisai mwana wa Azareli, mwana wa Azai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri,
14 na wenzao waliokuwa wenye uwezo: watu 128. Afisa wao mkuu alikuwa Zabdieli mwana wa Hagedolimu.
15 Kutoka Walawi: Shemaya mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, mwana wa Buni;
16 Shabethai na Yozabadi, viongozi wawili wa Walawi, ambao walisimamia kazi za nje za nyumba ya Mungu;
17 Matania mwana wa Mika, mwana wa Zabdi, mwana wa Asafu, kiongozi aliyeongoza kutoa shukrani na maombi; Bakbukia aliyekuwa msaidizi wake kati ya wenzake; na Abda mwana wa Shamua, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni.
18 Jumla ya Walawi waliokaa katika mji mtakatifu walikuwa watu 284.
19 Mabawabu: Akubu, Talmoni na wenzao, waliolinda malango: watu 172.
20 Waisraeli waliosalia, pamoja na makuhani na Walawi, walikuwa katika miji yote ya Yuda, kila mmoja katika urithi wa baba yake.
21 Watumishi wa Hekalu waliishi katika kilima cha Ofeli. Siha na Gishpa walikuwa wasimamizi wao.
22 Afisa mkuu wa Walawi huko Yerusalemu alikuwa Uzi mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika. Uzi alikuwa mmoja wa wazao wa Asafu, waliokuwa waimbaji wenye kuwajibika kwa ajili ya huduma ya nyumba ya Mungu.
23 Waimbaji walikuwa chini ya amri za mfalme, ambazo pia ziliratibu shughuli zao za kila siku.
24 Pethahia mwana wa Meshezabeli, mmoja wa wazao wa Zera mwana wa Yuda, alikuwa mwakilishi wa mfalme katika mambo yote kuhusu mahusiano na watu.
25 Kuhusu vijiji na mashamba yake, baadhi ya watu wa Yuda waliishi Kiriath-Arba na makazi yaliyokizunguka, katika Diboni na makazi yake, katika Yekabzeeli na vijiji vyake,
26 katika Yeshua, katika Molada, katika Beth-Peleti,
27 katika Hasar-Shuali, katika Beer-Sheba na makazi yake,
28 katika Siklagi, katika Mekona na makazi yake,
29 katika En-Rimoni, katika Sora, katika Yarmuthi,
30 Zanoa, Adulamu na vijiji vyake, katika Lakishi na mashamba yake, na katika Azeka na makazi yake. Hivyo walikuwa wakiishi kuanzia Beer-Sheba mpaka Bonde la Hinomu.
31 Wazao wa Wabenyamini kutoka Geba waliishi Mikmashi, Aiya, Betheli na makazi yake,
32 katika Anathothi, Nobu na Anania,
33 katika Hazori, Rama na Gitaimu,
34 katika Hadidi, Seboimu na Nebalati,
35 katika Lodi na Ono, na katika Bonde la Mafundi.
36 Baadhi ya makundi ya Walawi wa Yuda waliishi huko Benyamini.