< Nahumu 1 >

1 Neno alilosema Mungu kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu, Mwelkoshi.
Maono kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono ya Nahumu, Mwelkoshi.
2 Bwana ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi; Bwana hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu. Bwana hulipiza kisasi juu ya watesi wake, naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.
Yehova ni Mungu mwenye wivu na analipa kisasi; Yehova hulipa kisasi na amejaa ghadhabu; Yohova analipiza kisasi kwa adui zake, na huiendeleza hasira yake kwa adui zake.
3 Bwana si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu, Bwana hataacha kuadhibu wenye hatia. Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni vumbi la miguu yake.
Yehova ni mwenye nguvu nyingi na mpole wa hasira; hatakuwa na namna ya kuacha kuwahesabia hatia adui zake. Yehova hufanya njia yake kwenye upepo wa kisulisuli na dhoruba, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake.
4 Anakemea bahari na kuikausha, anafanya mito yote kukauka. Bashani na Karmeli zinanyauka na maua ya Lebanoni hukauka.
Huikemea bahari na kuifanya ikauke; hukausha mito yote. Bashani ni dhaifu, na Karmeli pia; maua ya Lebanoni ni dhaifu.
5 Milima hutikisika mbele yake na vilima huyeyuka. Nchi hutetemeka mbele yake, dunia na wote waishio ndani yake.
Milima hutetema kwenye uwepo wake, na vilima huyeyuka; dunia huanguka mbele zake, kabisa, dunia na watu wote wanaoishi ndani yake.
6 Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu? Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali? Ghadhabu yake imemiminwa kama moto, na miamba inapasuka mbele zake.
Ni nani anaweza kusimama mbele ya ghadhabu yake? Nani anaweza kuzuia ukali wa hasira yake? Ghadhabu yake imemwagwa kama moto, na miamba ameibomoa mbalimbali.
7 Bwana ni Mwema, kimbilio wakati wa taabu. Huwatunza wale wanaomtegemea,
Yehova ni mwema, boma katika siku ya taabu; na yeye ni mwaminifu kwa wale wanaomkimbilia.
8 lakini kwa mafuriko makubwa, ataangamiza Ninawi; atafuatilia adui zake hadi gizani.
Lakini atafanya mwisho wa adui zake kwa mafuriko ya kutisha; atawawinda kwenye giza.
9 Shauri baya lolote wapangalo dhidi ya Bwana yeye atalikomesha; taabu haitatokea mara ya pili.
Watu wanapanga nini dhidi ya Yehova? Yeye atakomesha; taabu haitainuka mara ya pili.
10 Watasongwa katikati ya miiba na kulewa kwa mvinyo wao. Watateketezwa kama mabua makavu.
Maana watakuwa wamevurugika kama michongoma; wataloweshwa katika kinywaji chao mwenyewe; wataharibiwa kabisa kwa moto kama mashina ya mabua.
11 Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja, ambaye anapanga shauri baya dhidi ya Bwana na kushauri uovu.
Mtu mmoja aliinuka miongoni mwenu, Ninawi, aliyepanga ubaya dhidi ya Yehova, mtu ambaye aliimarisha uovu.
12 Hili ndilo asemalo Bwana: “Ingawa wana muungano nao ni wengi sana, watakatiliwa mbali na kuangamia. Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda, sitakutesa tena.
Hivi ndivyo anavyosema Yehova, “Hata kama wananguvu zao timilifu na idadi timilifu, hata hivyo watanyolewa, watu wao hawatakuwepo tena. Bali wewe, Yuda: Ingawa nimekutesa, sitakutesa tena.
13 Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako, nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”
Sasa nitaivunja ile nira ya watu kutoka kwako; nitaikata minyororo yako.
14 Hii ndiyo amri Bwana aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi: “Hutakuwa na wazao watakaoendeleza jina lako. Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kuyeyusha ambazo zipo katika hekalu la miungu yenu. Nitaandaa kaburi lako, kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”
Yehova ametoa amri juu yako, Ninawi: “Hakutakuwa na kizazi tena chenye kubeba jina lako. Nitazizuia sanamu zilizochongwa na kuziondoa sanamu za chuma kutoka kwenye nyumba za miungu yenu. Nitachimba makaburi yenu, kwa kudharauliwa kwenu.”
15 Tazama, huko juu milimani, miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema, ambaye anatangaza amani! Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako, nawe utimize nadhiri zako. Waovu hawatakuvamia tena; wataangamizwa kabisa.
Tazama, juu ya milima kuna miguu ya mtu aletaye habari njema, anayetangaza amani! Sherehekeeni sikukuu zenu, Yuda, na tunzeni nadhiri zenu, kwa maana mwovu hatawavamia tena; ameondolewa kabisa.

< Nahumu 1 >