< Mika 7 >

1 Taabu gani hii niliyo nayo! Nimefanana na yule akusanyaye matunda ya kiangazi, aokotaye masazo baada ya kuvunwa shamba la mizabibu; hakuna kishada chenye matunda ya kula, hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.
Ole wangu! Kwangu mimi ni kama msimu wa mavuno ulipokwisha, na pia makombo ya mavuno ya zabibu kwenye shamba la mizabibu: Hakuna tena kishamba cha matunda kinachoonekana, hakuna matini ya malimbuka ambayo ninayoyatamani.
2 Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi; hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki. Watu wote wanavizia kumwaga damu, kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.
Watu waaminifu wamepotelea kutoka kwenye nchi, hakuna mtu mwadilifu katika wanadamu wote. Wote hudanganya katika kusubiri kumwaga damu; kila mtu humuwinda ndugu yake mwenyewe kwa wavu.
3 Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya, mtawala anadai zawadi, hakimu anapokea rushwa, wenye nguvu wanaamuru wanachotaka: wote wanafanya shauri baya pamoja.
Mikono yao ni mizuri mno kwa kufanya madhara. watawala huuliza pesa, hakimu yuko tayari kwa rushwa, na mtu mwenye nguvu anawaambia wengine kile anachokitaka kujipatia. Hivyo ndivyo waundavyo kwa pamoja.
4 Aliye mwema kupita wote kati yao ni kama mchongoma, anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao ni mbaya kuliko uzio wa miiba. Siku ya walinzi wako imewadia, siku atakayokutembelea Mungu. Sasa ni wakati wao wa kuchanganyikiwa.
Mtu bora kwao ni kama mitemba, mwadilifu sana ni kama mche wa miba. Imefika siku iliyosemwa nyuma na walinzi wako, siku ya hukumu. Sasa ni mda wa machafuko.
5 Usimtumaini jirani; usiweke matumaini kwa rafiki. Hata kwa yule alalaye kifuani mwako uwe mwangalifu kwa maneno yako.
Msimwamini kila jirani; msimuweke kiongozi katika rafiki yeyote. Kuweni makini kuhusiana na kile msemacho hata kwa mwanamke ambaye adanganyaye kwenye mikono yenu.
6 Kwa kuwa mwana humdharau baba yake, naye binti huinuka dhidi ya mama yake, mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake: adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.
Kwa kuwa mwana humfedhehesha baba yake, binti huinuka kushindana na mama yake, na mke wa mwana wa kiume hushindana na mama mkwe wake. Adui wa watu ni watu wa nyumba yake mwenyewe.
7 Lakini mimi, namtazama Bwana kwa matumaini, namngoja Mungu Mwokozi wangu; Mungu wangu atanisikia mimi.
Lakini kama kwangu mimi, nitamtazama Yahwe. Nitamsubiri Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu ataniskia.
8 Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu! Ingawa nimeanguka, nitainuka. Japo ninaketi gizani, Bwana atakuwa nuru yangu.
Usifurahi juu yangu, adui yangu. Niangukapo, nitainuka. Wakati nitakapokuwa nimekaa katika giza, Yahwe atakuwa mwanga kwangu.
9 Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake, nitabeba ghadhabu ya Bwana, mpaka atakaponitetea shauri langu na kuithibitisha haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaiona haki yake.
Kwasababu nimetenda dhambi dhidi ya Yahwe, nitachukua ghadhabu yake hata aniteteapo kosa langu, na kutekeleza hukumu kwa ajili yangu. Atanileta kwenye nuru, na nitamwona akiniokoa kwenye haki yake.
10 Kisha adui yangu ataliona naye atafunikwa na aibu, yule aliyeniambia, “Yu wapi Bwana Mungu wako?” Macho yangu yataona kuanguka kwake, hata sasa atakanyagwa chini ya mguu kama tope barabarani.
Kisha adui yangu atakapoliona hilo, na aibu itamfunika yule aliyeniambia, “Yahwe Mungu wako yuko wapi?” macho yangu yatamtazama; atakanyagwa chini kama tope kwenye mitaa.
11 Siku ya kujenga kuta zako itawadia, siku ya kupanua mipaka yako.
Siku ya ya kujenga kuta zako zitafika; siku hiyo mipaka itasogezwa mbali sana.
12 Siku hiyo watu watakuja kwako kutoka Ashuru na miji ya Misri, hata kutoka Misri hadi Frati na kutoka bahari hadi bahari na kutoka mlima hadi mlima.
Siku hiyo watu watakuja kwako, kutoka Ashuru na miji katika Misri, kutoka Misri hata mto mkubwa, kutoka bahari kwenda bahari, na kutoka mlima kwenda mlima.
13 Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao.
Hizo nchi zitakuwa zimejitenga kwasababu ya watu ambao wanaishi huko sasa, kwasababu ya tunda la matendo yao.
14 Wachunge watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, ambalo linaishi peke yake msituni, katika nchi ya malisho yenye rutuba. Waache walishe katika Bashani na Gileadi kama ilivyokuwa siku za kale.
Chunga watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako. Wanaishi wenyewe kwenye msitu, katikati ya msitu. Wachunge katika Bashani na Gileadi kama siku za zamani.
15 “Kama siku zile mlipotoka Misri, nitawaonyesha maajabu yangu.”
Kama katika siku wakati mlipotoka nje ya nchi ya Misri, nitawaonyesha maajabu.
16 Mataifa yataona na kuaibika, waliondolewa nguvu zao zote. Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao na masikio yao yatakuwa na uziwi.
Mataifa yataona na kuwa na aibu ya nguvu zao zote. Wataweka mikono yao kwenye midomo yao; masikio yao yatakuwa kiziwi.
17 Wataramba mavumbi kama nyoka, kama viumbe vitambaavyo juu ya ardhi. Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka; watamgeukia Bwana Mungu wetu kwa hofu nao watakuogopa.
Watalamba vumbi kama nyoka, kama viumbe vitaambavyo juu ya nchi. Watatoka nje kwenye maficho kwa hofu; watakuja kwako kwa hofu, Yahwe Mungu wetu, na wataogopa kwa sababu yako.
18 Ni nani Mungu kama wewe, ambaye anaachilia dhambi na kusamehe makosa ya mabaki ya urithi wake? Wewe huwi na hasira milele, bali unafurahia kuonyesha rehema.
Ni nani aliye Mungu kama wewe, wewe uchukuaye dhambi, wewe upitaye juu ya kosa la mabaki ya mrithi wako? Hutunzi hasira yako milele, kwa sababu unapenda kutuonyesha agano lako la aminifu.
19 Utatuhurumia tena, utazikanyaga dhambi zetu chini ya nyayo zako, na kutupa maovu yetu yote katika vilindi vya bahari.
Tena utakuwa na huruma juu yetu; utayakanyaga maovu chini ya miguu yako. Utazitupa dhambi zetu zote kwenye vilindi vya bahari.
20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo, nawe utamwonyesha Abrahamu rehema, kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu siku za kale.
Utampatia ukweli Yakobo na agano aminifu kwa Abrahamu, ulipoapa kwa babu zetu katika siku za kale.

< Mika 7 >