< Mathayo 9 >

1 Yesu akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao.
Yesu akaingia kwenye boti, akavuka na akafika kwenye mji alipokuwa anaishi.
2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”
Tazama, wakamletea mtu aliyepooza amelazwa kwenye godoro. alipooiona imani yao, Yesu akamwambia mtu aliyepooza, “Mwanangu, uwe na furaha, Dhambi zako zimesamehewa”
3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”
Tazama, Baadhi ya walimu wa sheria wakasemezana wao kwa wao, “Huyu mtu anakufuru”
4 Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu?
Yesu akatambua mawazo yao na kusema, “Kwa nini mnawaza maovu moyoni mwenu?
5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’?
Kipi kilicho rahisi kusema, 'Dhambi zako zimesamehewa' au kusema, 'Simama na utembee?'
6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
Lakini mtambue ya kwamba Mwana wa Adamu anao uwezo wa kusamehe dhambi...” aliyasema haya kwa yule aliyepooza, “Simama, chukua godoro lako, na uende nyumbani kwako”
7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake.
Ndipo yule mtu akasimama na kuondoka kwenda nyumbani kwake.
8 Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama haya kwa wanadamu.
Makutano walipoona hayo, walishangaa na kumsifu Mungu, ambaye amewapa uwezo huo watu.
9 Yesu alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akaondoka, akamfuata.
Na Yesu alipokuwa akipita kutoka hapo, alimwona mtu ambaye aliitwa kwa jina la Mathayo, ambaye alikuwa amekaa sehemu ya watoza ushuru. Naye akamwambia, “Nifuate mimi” Naye akasimama na kumfuata.
10 Yesu alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake.
Na Yesu alipoketi ili ale chakula ndani ya nyumba, wakaja watoza ushuru wengi na watu waovu wakashiriki chakula pamoja na Yesu na wanafunzi wake.
11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
Ndipo Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi “Kwa nini mwalimu wenu anakula chakula pamoja na watoza ushuru na watu waovu?”
12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu.
Yesu aliposikia hayo, naye alisema “Watu walio na afya nzuri hawahitaji mganga, isipokuwa wale walio wagonjwa.
13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Inawapasa muende mkajifunze maana yake, “Ninapenda rehema na siyo dhabihu” Kwa kuwa nilikuja, si kwa wenye haki kutubu, lakini kwa wenye dhambi.
14 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakaja na kumuuliza Yesu, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
Ndipo wanafunzi wa Yohana wakaja kwake na kusema, “Kwa nini sisi na mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
15 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.
Yesu akawaambia, Je wasindikizaji wa arusi wanaweza kuwa na huzuni pindi Bwana arusi anapokuwa pamoja nao? Lakini siku zinakuja ambapo Bwana arusi atachukuliwa kutoka kwao, na ndipo watakapofunga.
16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi.
Hakuna mtu anayeweka kipande cha nguo mpya kwenye nguo ya zamani, kiraka kitatatuliwa kutoka kwenye nguo na mpasuko mkubwa utatokea.
17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”
Hakuna watu wanaoweka mvinyo mpya katika chombo cha mvinyo wa zamani, ikiwa watafanya, ngozi itachanika, mvinyo utatoweka na ngozi itaharibika. Badala yake, huweka mvinyo mpya katika ngozi mpya na vyote vitakuwa salama.
18 Yesu alipokuwa akiwaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye atakuwa hai.”
Wakati Yesu alipokuwa akiwaambia mambo hayo, tazama, afisa akaja akasujudu mbele yake, Naye akasema, “Binti yangu amefariki punde, lakini njoo na uweke mkono wako juu yake na yeye ataishi tena.
19 Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.
Ndipo Yesu akasimama na kumfuata na wanafunzi wake pia.
20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake,
Tazama, mwanamke ambaye alikuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja karibu na Yesu na akagusa sehemu ya pindo la vazi lake.
21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”
Kwa kuwa alisema, “Endapo nitagusa vazi lake, nami nitapata uponyaji.”
22 Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.
Yesu akageuka na kumtazama na kumwambia. “Binti, jipe moyo, imani yako imekufanya upone,” Na muda huo huo mwanamke akapata uponyaji muda huo.
23 Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele,
Na Yesu alipofika kwenye nyumba ya afisa, naye aliwaona wapiga tarumbeta na umati wa watu ulikuwa ukipiga kelele.
24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka.
Naye akasema, “Tokeni hapa, kwa kuwa binti hajafa, bali amelala. Lakini wao walicheka na kumkebehi.
25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka.
Na wale watu walipotolewa nje, naye akaingia chumbani na kumshika mkono na msichana akaamka.
26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.
Na habari hizi zikaenea katika mji mzima.
27 Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
Ndipo Yesu alipokuwa akipita kutoka pale, wanaume wawili vipofu wakamfuata. Waliendelea kupaza sauti wakisema, “Tunaomba uturehemu, Mwana wa Daudi.”
28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?” Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”
Pindi Yesu apokuwa amefika kwenye nyumba, wale vipofu wakaja kwake. Yesu akawaambia, “Mnaamini kwamba ninaweza kutenda?” Nao wakamwambia “Ndiyo, Bwana”
29 Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.”
Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema “Na ifanyike hivyo kwenu kama imani yenu ilivyo”
30 Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.”
Na macho yao yakafumbuka. Ndipo Yesu akasisitiza akawaamuru na kusema “Angalieni mtu yeyote asifahamu kuhusu jambo hili.”
31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.
Lakini watu hawa wawili wakaondoka na kutangaza habari hizi sehemu zote za mji.
32 Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu.
Ndipo wale wanaume wawili walipokuwa wakienda zao, Tazama, mtu mmoja bubu aliyepagawa na pepo akaletwa kwa Yesu.
33 Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”
Na pepo walipomtoka, yule mtu bubu akaanza kuongea. Umati ukashangazwa na kusema “Hii haijawahi kutokea katika Israel.
34 Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”
Lakini mafarisayo walikuwa wakisema “Kwa wakuu wa pepo, anawafukuza mapepo”
35 Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi.
Yesu akaenda kwenye miji yote na vijiji. Naye akaendelea kufundisha katika masinagogi, akihubiri injili ya ufalme, na kuponya magonjwa ya kila aina na udhaifu wa aina zote.
36 Alipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji.
Wakati alipotazama umati, naye aliwaonea huruma, kwa sababu walisumbuka na kuvunjika moyo. Walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji.
37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache.
Naye akawaambia wanafunzi wake. “Mavuno ni mengi, lakini wafanya kazi ni wachache.
38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”
Hivyo basi upesi mwombeni Bwana wa mavuno, ili kwamba atume wafanya kazi katika mavuno yake.”

< Mathayo 9 >