< Mathayo 8 >
1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata.
Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata.
2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”
Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia akisema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!”
3 Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.
Yesu akanyosha mkono wake, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika.” Mara huyo mtu akapona ukoma wake.
4 Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Mose, ili kuwa ushuhuda kwao.”
Kisha Yesu akamwambia, “Sikiliza, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”
5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada,
Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, ofisa mmoja Mroma alimwendea, akamsihi
6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”
akisema, “Mheshimiwa, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.”
7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”
Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.”
8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
Huyo ofisa akamwambia, “Mheshimiwa, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.
9 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, Nenda! naye huenda; na mwingine, Njoo! naye huja; na mtumishi wangu, Fanya kitu hiki! naye hufanya.”
10 Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii.
Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli aliye na imani kama hii.
11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni.
Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa mbinguni.
12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”
Lakini wale ambao wangalipaswa kuwa katika Ufalme huo watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.”
13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.
Kisha Yesu akamwambia huyo ofisa Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile.
14 Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa.
Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali.
15 Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.
Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia.
16 Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote.
Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa.
17 Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba: “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na alichukua magonjwa yetu.”
Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameondoa udhaifu wetu, ameyachukua magonjwa yetu.”
18 Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ngʼambo ya ziwa.
Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ng'ambo ya ziwa.
19 Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.”
Mwalimu mmoja wa Sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote uendako.”
20 Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.”
21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.”
22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”
Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.”
23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata.
Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye.
24 Ghafula, kukainuka dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi.
Ghafla, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu alikuwa amelala usingizi.
25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”
Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!”
26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.
Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akazikemea pepo na mawimbi; kukawa shwari kabisa.
27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”
Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na mawimbi vinamtii!”
28 Walipofika ngʼambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile.
Yesu alifika katika nchi ya Wagerasi, ng'ambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita katika njia hiyo.
29 Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”
Nao wakaanza kupiga kelele, “Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?”
30 Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha.
Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa.
31 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.”
Basi, hao pepo wakamsihi, “Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale.”
32 Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji.
Yesu akawaambia, “Haya, nendeni.” Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa maji.
33 Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.
Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa.
34 Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.
Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.