< Mathayo 7 >
1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa.
“Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;
2 Kwa maana jinsi unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa, na kwa kipimo kile upimiacho, ndicho utakachopimiwa.
kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.
3 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?
Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?
4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako,’ wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?
Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?
5 Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.
Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako.
6 “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu; wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyagakanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.
“Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.
7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.
“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa.
9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe?
Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?
10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka?
Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?
11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?
Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.
12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.
“Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo.
“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.
14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.
Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali.
“Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma?
Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!
17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.
Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema.
19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni.
20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.
Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.
21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
“Si kila aniambiaye, Bwana, Bwana, ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’
Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.
23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
Hapo nitawaambia: Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.
24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba.
“Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.
25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba.
Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.
26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga.
“Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.
27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”
Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa.”
28 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake,
Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.
29 kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.
Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.