< Mathayo 28 >

1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.
Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi.
2 Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia.
Ghafla kutatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia.
3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.
Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.
4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.
Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa.
5 Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.
Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, “Ninyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.
6 Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa.
Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala.
7 Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’”
Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni.”
8 Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo.
Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake.
9 Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu.
Mara, Yesu akakutana nao, akawasalimu: “Salamu.” Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake.
10 Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”
Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona.”
11 Wakati wale wanawake walikuwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia.
Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia.
12 Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha
Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha
13 wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’
wakisema, “Ninyi mtasema hivi: Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.
14 Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.”
Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa ninyi hamtapata matatizo.”
15 Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo.
Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.
16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza.
Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagiza Yesu.
17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka.
Walipomwona, wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka.
18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
Yesu akaja karibu, akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu,
Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu; mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.” (aiōn g165)
Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati.” (aiōn g165)

< Mathayo 28 >