< Mathayo 27 >

1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua.
Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua.
2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.
Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.
3 Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.
Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha.
4 Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.” Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”
Akawaambia, “Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe.” Lakini wao wakasema, “Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako.”
5 Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.
Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.
6 Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.”
Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, “Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu.”
7 Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni.
Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.
8 Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo.
Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.
9 Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli,
Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: “Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei,
10 wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”
wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.”
11 Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?” Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”
Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamwambia, “Wewe umesema.”
12 Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno.
Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.
13 Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?”
Hivyo Pilato akamwuliza, “Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?”
14 Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.
Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.
15 Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu.
Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.
16 Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba.
Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba.
17 Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?”
Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, “Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwae Kristo?”
18 Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.
Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.
19 Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: “Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”
20 Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe.
Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.
21 Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?” Wakajibu, “Baraba.”
Mkuu wa mkoa akawauliza, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?” Wakamjibu, “Baraba!”
22 Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?” Wakajibu wote, “Msulubishe!”
Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!”
23 Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?” Wao wakazidi kupaaza sauti: “Asulubiwe!”
24 Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”
Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.”
25 Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”
Watu wote wakasema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”
26 Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe.
27 Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.
Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.
28 Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha
Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.
29 wakasokota taji ya miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”
Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!”
30 Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena.
Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.
31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.
Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
32 Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.
Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.
33 Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).
Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, “Mahali pa Fuvu la kichwa,”
34 Hapo wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa.
wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.
35 Walipokwisha kumsulubisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”]
Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
36 Kisha wakaketi, wakamchunga.
Wakaketi, wakawa wanamchunga.
37 Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.
Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.”
38 Wanyangʼanyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto.
Wanyang'anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.
39 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao
Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema,
40 na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”
“Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!”
41 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki wakisema,
Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema,
42 “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, nasi tutamwamini.
“Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini.
43 Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’”
Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.”
44 Hata wale wanyangʼanyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.
Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.
45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote.
Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza.
46 Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”
47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.”
Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Eliya.”
48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe.
Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.
49 Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”
Wengine wakasema, “Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.”
50 Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.
Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.
51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka.
Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;
52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa.
makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;
53 Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.
nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.
54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
55 Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake.
Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.
56 Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.
Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.
57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.
Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.
58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe.
Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe.
59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi,
Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani,
60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake.
akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.
61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwepo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.
Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.
62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato
Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,
63 na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’
Wakasema, “Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, Baada ya siku tatu nitafufuka.
64 Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”
Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali.”
65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.”
Pilato akawaambia, “Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo.”
66 Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.
Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.

< Mathayo 27 >