< Mathayo 24 >

1 Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu.
Yesu alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonyesha majengo ya Hekalu.
2 Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
Yesu akawaambia, “Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.”
3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?” (aiōn g165)
Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, “Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?” (aiōn g165)
4 Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye.
Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’nao watawadanganya wengi.
Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: Mimi ndiye Kristo, nao watawapotosha watu wengi.
6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado.
Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado.
7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.
Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.
8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.
9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu.
“Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa ajili ya jina langu.
10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana.
Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.
11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi.
Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.
12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa,
Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.
13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka.
14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.
Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.
15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu),
“Basi, mtakapoona Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),
16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.
hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.
17 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba.
Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake.
18 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.
Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.
19 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!
Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!
20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato.
Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato!
21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe.
Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena.
22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa.
Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa.
23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki.
“Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: Kristo yuko hapa au Yuko pale, msimsadiki.
24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa.
Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu.
25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.
Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati.
26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki.
Basi, wakiwaambieni, Tazameni, yuko jangwani, msiende huko; au, Tazameni, amejificha ndani, msisadiki;
27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.
Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.
29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile, “‘jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’
“Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.
30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.
Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.
31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.
Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.
32 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
“Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
33 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.
Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.
34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.
35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
36 “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.
“Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye ajuaye.
37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.
38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina.
Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.
39 Nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.
Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.
40 Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
42 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu.
Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.
43 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa.
Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.
Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”
45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa?
Yesu akaendelea kusema, “Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.
47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.
Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote.
48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’
Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: Bwana wangu anakawia kurudi,
49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi.
kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi,
50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua.
bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua.
51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.
Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.

< Mathayo 24 >