< Mathayo 23 >
1 Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake:
Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake,
2 “Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose,
“Walimu wa Sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua Sheria ya Mose.
3 hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri.
Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri.
4 Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.
Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba.
5 “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao.
Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya Sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao.
6 Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi.
Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi.
7 Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’
Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: Mwalimu.
8 “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu.
Lakini ninyi msiitwe kamwe Mwalimu, maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu.
9 Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni.
Wala msimwite mtu yeyote Baba hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu aliye mbinguni.
10 Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo.
Wala msiitwe Viongozi, maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo.
11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.
Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu.
12 Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.
Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.
13 “Lakini ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya Ufalme wa Mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [
“Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa Ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Ninyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie.
14 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo hukumu yenu itakuwa kuu zaidi.]
Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali.
15 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja mwongofu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa jehanamu mara mbili kuliko ninyi! (Geenna )
“Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko ninyi wenyewe. (Geenna )
16 “Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’
“Ole wenu viongozi vipofu! Ninyi mwasema ati mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, kiapo hicho kinamshika.
17 Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?
Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: dhahabu au Hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?
18 Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’
Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.
19 Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu?
Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?
20 Kwa hiyo, mtu aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake.
Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake.
21 Naye mtu aapaye kwa Hekalu, huapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake.
Na anayeapa kwa Hekalu ameapa kwa hilo Hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake.
22 Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketiye juu ya kiti hicho.
Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.
23 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo.
Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu zaka, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya Sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndiyo hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.
24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!
Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia!
25 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na kutokuwa na kiasi.
“Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyang'anyi na uchoyo.
26 Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia.
Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia.
27 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu.
“Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu.
28 Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
Hali kadhalika ninyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
29 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki.
“Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema.
30 Nanyi mwasema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu, tusingalikuwa tumeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’
Mwasema: Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!
31 Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii.
Hivyo mnathibitisha ninyi wenyewe kwamba ninyi ni watoto wa watu waliowaua manabii.
32 Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!
Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza!
33 “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu? (Geenna )
Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu? (Geenna )
34 Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine.
Ndiyo maana mimi ninawapelekea ninyi manabii, watu wenye hekima na walimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji.
35 Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu.
Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kuuawa kwa Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka kuuawa kwa Zakariya, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua Hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu.
36 Amin, nawaambia, haya yote yatakuja juu ya kizazi hiki.
Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya.
37 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!
“Yerusalemu, Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka.
38 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa.
Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame.
39 Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa mpaka mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana.’”
Nakwambia kweli, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana.”