< Mathayo 23 >
1 Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake:
2 “Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose,
3 hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri.
4 Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.
5 “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao.
6 Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi.
7 Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’
8 “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu.
9 Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni.
10 Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo.
11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu.
12 Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.
13 “Lakini ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya Ufalme wa Mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [
14 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo hukumu yenu itakuwa kuu zaidi.]
15 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja mwongofu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa jehanamu mara mbili kuliko ninyi! (Geenna )
16 “Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’
17 Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?
18 Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’
19 Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu?
20 Kwa hiyo, mtu aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake.
21 Naye mtu aapaye kwa Hekalu, huapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake.
22 Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketiye juu ya kiti hicho.
23 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo.
24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!
25 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na kutokuwa na kiasi.
26 Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia.
27 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu.
28 Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.
29 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki.
30 Nanyi mwasema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu, tusingalikuwa tumeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’
31 Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii.
32 Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!
33 “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu? (Geenna )
34 Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine.
35 Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu.
36 Amin, nawaambia, haya yote yatakuja juu ya kizazi hiki.
37 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!
38 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa.
39 Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa mpaka mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana.’”