< Mathayo 20 >

1 “Kwa maana Ufalme wa Mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri ili kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu.
“Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.
2 Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinarimoja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.
Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu.
3 “Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi.
Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.
4 Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’
Akawaambia, Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.
5 Kwa hiyo wakaenda. “Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo.
Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.
6 Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’
Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
7 “Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’ “Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’
Wakamjibu: Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Yeye akawaambia, Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.
8 “Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’
“Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.
9 “Wale vibarua walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakaja na kila mmoja wao akapokea dinari moja.
Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja.
10 Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja.
Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.
11 Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba,
Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung'unikia yule bwana.
12 wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’
Wakasema, Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?
13 “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja?
“Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja?
14 Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe.
Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
15 Je, sina haki yangu kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’
Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?”
16 “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
17 Basi Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua kando wale wanafunzi wake kumi na wawili na kuwaambia,
Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,
18 “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Nao watamhukumu kifo
“Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe.
19 na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”
Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.”
20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.
Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.
21 Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”
Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.”
22 Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakajibu, “Tunaweza.”
Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.”
23 Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”
Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.”
24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili.
Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.
25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao.
Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao.
26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu,
Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;
27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu:
na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.
28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
29 Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata.
Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.
30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: “Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”
Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: “Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”
Wakamjibu, “Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.”
34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.
Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.

< Mathayo 20 >