< Mathayo 16 >

1 Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.
Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba afanye ishara itokayo mbinguni.
2 Yesu akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’
Lakini Yesu akawajibu, “Wakati wa jioni ukifika ninyi husema: Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!
3 Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati.
Na alfajiri mwasema: Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda! Basi, ninyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.
4 Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.
Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara yoyote isipokuwa tu ile ya Yona.” Basi, akawaacha, akaenda zake.
5 Wanafunzi wake walipofika ngʼambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate.
Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate.
6 Yesu akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”
Yesu akawaambia, “Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”
7 Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”
Lakini wao wakawa wanajadiliana: “Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate.”
8 Yesu, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate?
Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate?
9 Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?
Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu elfu tano? Je, mlijaza vikapu vingapi vya makombo?
10 Au ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?
Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu elfu nne, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?
11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
Inawezekanaje hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”
12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
13 Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”
Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?”
14 Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yohana Mbatizaji; wengine husema ni Eliya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”
Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.”
15 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
Yesu akawauliza, “Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni.
Yesu akasema, “Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana si binadamu aliyekufunulia ukweli huu, ila Baba yangu aliye mbinguni.
18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kulishinda. (Hadēs g86)
Nami nakwambia: wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala kifo chenyewe hakitaweza kulishinda. (Hadēs g86)
19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.”
Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni.”
20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
21 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.
Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake: “Ni lazima mimi niende Yerusalemu, na huko nikapate mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Nitauawa, na siku ya tatu nitafufuliwa.”
22 Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”
Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: “Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!”
23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, “Ondoka mbele yangu Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya mungu bali ni ya kibinadamu!”
24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza;
26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?
lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake?
27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.
Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.
28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”
Kweli nawaambieni, wako wengine papahapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika Ufalme wake.”

< Mathayo 16 >