< Mathayo 12 >
1 Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala.
Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake.
2 Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”
Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, “Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato.”
3 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa?
Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?
4 Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao.
Yeye aliingia katika Nyumba ya Mungu pamoja na wenzake, wakala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao.
5 Au hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia?
Au je, hamjasoma katika Sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja Sheria Hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia?
6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa.
Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko Hekalu.
7 Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia,
Kama tu mngejua maana ya maneno haya: Nataka huruma wala si dhabihu, hamngewahukumu watu wasio na hatia.
8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
Maana Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato.”
9 Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao,
Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao.
10 na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”
Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, “Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?” Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki.
11 Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa?
Lakini Yesu akawaambia, “Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato?
12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”
Mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”
13 Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine.
Kisha akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine.
14 Lakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua.
Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu.
15 Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wagonjwa wao wote,
Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote,
16 akiwakataza wasiseme yeye ni nani.
akawaamuru wasiwaambie watu habari zake,
17 Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema:
ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie:
18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa.
“Hapa ni mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka Roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote.
19 Hatagombana wala hatapiga kelele, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.
Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani.
20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya haki ishinde.
Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale.
21 Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.”
Katika jina lake mataifa yatakuwa na tumaini.”
22 Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona.
Hapo watu wakamletea Yesu kipofu mmoja ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata, akaweza kusema na kuona.
23 Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”
Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, “Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?”
24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”
Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, “Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.”
25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama.
Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka.
26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama?
Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje?
27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.
Ninyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu ninyi.
28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.
Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.
29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.
“Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang'anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang'anya mali yake.
30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.
“Yeyote asiyejiunga nami, anapingana nami; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.
31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu.
32 Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao. (aiōn )
Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao. (aiōn )
33 “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake.
“Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mema; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake.
34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake.
Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali ninyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni.
35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake.
Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya.
36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena.
“Basi, nawaambieni, Siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema.
37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
Maana kwa maneno yako, utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako, utahukumiwa kuwa na hatia.”
38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”
Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”
39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona.
Naye akawajibu, “Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara; hamtapewa ishara nyingine, ila tu ile ishara ya nabii Yona.
40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumikwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana.
Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha.
41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
Watu wa Ninewi watatokea siku ya hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona!
42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”
Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Solomoni.
43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati.
“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzika asipate.
44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri.
Hapo hujisemea: Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka. Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa,
45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”
huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu.”
46 Wakati alikuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye.
Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye.
47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”
Basi, mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe.”
48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?”
Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, “Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni kina nani?”
49 Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu!
Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu!
50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”
Maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”