< Mathayo 11 >
1 Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.
Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.
2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake
Yohane mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake,
3 ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”
wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?”
4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona:
Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona:
5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.
vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema.
6 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”
Heri mtu yule asiyekuwa na mashaka nami.”
7 Wale wanafunzi wa Yohana walipokuwa wanaondoka, Yesu akaanza kusema na makutano kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?
Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?
8 Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme.
Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumtazama mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme.
9 Basi mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.
Basi, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.
10 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa: “‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako.’
“Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: Tazama, hapa namtuma mjumbe wangu, asema Bwana, akutangulie na kukutayarishia njia yako.
11 Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji. Lakini aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni ni mkuu kuliko Yohana.
Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye.
12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa, Ufalme wa Mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka.
Tangu wakati wa Yohane mbatizaji mpaka leo hii, Ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu.
13 Kwa maana manabii wote na Sheria walitabiri mpaka wakati wa Yohana.
Mafundisho yote ya manabii na sheria yalibashiri juu ya nyakati hizi.
14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Eliya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja.
Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Eliya ambaye angekuja.
15 Yeye aliye na masikio, na asikie.
Mwenye masikio na asikie!
16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,
“Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine:
17 “‘Tuliwapigia filimbi, lakini hamkucheza; tuliwaimbia nyimbo za maombolezo, lakini hamkuomboleza.’
Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza; tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!
18 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’
Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: Amepagawa na pepo.
19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.”’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”
Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: Mtazameni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wahalifu! Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake.”
20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu.
Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kubadili nia zao mbaya:
21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.
“Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia na kujipaka majivu zamani, ili kuonyesha kwamba wametubu.
22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.
Hata hivyo nawaambieni, Siku ya hukumu, ninyi mtapata adhabu kubwa kuliko Tiro na Sidoni.
23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwepo hadi leo. (Hadēs )
Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka Kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. (Hadēs )
24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”
Lakini nawaambieni, Siku ya hukumu itakuwa nafuu zaidi kwa watu wa Sodoma, kuliko kwako wewe.”
25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo.
Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima mambo haya, ukawafumbulia watoto wadogo.
26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
Naam Baba, ndivyo ilivyokupendeza.
27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.
“Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumjulisha.
28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu.
30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”
Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”