< Mathayo 10 >
1 Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, naye akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu, ili waweze kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.
Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili pamoja na kuwapa mamlaka juu ya pepo wachafu, kuwakemea na kuwafukuza na kuponya aina zote za maladhi na aina zote za magonjwa.
2 Haya ndiyo majina ya hao mitume kumi na wawili: wa kwanza, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye;
Majina ya mitume kumi na wawili ni haya. La kwanza simeoni (ambaye pia anaitwa Petro), na Andrea kaka yake, Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana kaka yake:
3 Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo;
Philipo, na Bartelemayo, Thomaso, na Mathayo mtoza ushuru, Yakobo mwana wa Alfayo, na Tadeo,
4 Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.
Simoni mkananayo, na Yuda iskariote, ambaye alimsaliti.
5 Hawa kumi na wawili, Yesu aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria.
Hawa kumi na wawili Yesu aliwatuma. Naye aliwaelekeza akisema “Msiende sehemu wanakoishi wamataifa na msiingie kwenye miji ya wasamalia.
6 Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea.
Badala yake, mwende kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israel.
7 Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’
Na mnapokwenda, hubirini na kusema, ufalme wa mbinguni umekaribia.'
8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure.
Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma na fukuzeni pepo. Mmepokea bure, toeni bure.
9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu.
Msichue dhahabu, almasi au shaba kwenye pochi zenu.
10 Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtendakazi anastahili posho yake.
Usichukue mkoba katika safari yenu, au nguo za ziada, viatu au fimbo, kwa kuwa mfanyakazi anastahili chakula chake.
11 “Mji wowote au kijiji chochote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake mpaka mtakapoondoka.
Mji wowote au kijiji mtakachoingia, tafuteni ambaye anastahili na mkae pale mpaka mtakapoondoka.
12 Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani.
Mtakapoingia katika nyumba salimieni,
13 Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi.
endapo nyumba inastahili, amani yenu ibaki pale, lakini kama nyumba haistahili, amani yenu iondoke pamoja nanyi.
14 Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo.
Na kwa wale wasiowapokea ninyi au kusikiliza maneno yenu, wakati mnaondoka kwenye nyumba au mji huo, jipanguseni mavumbi ya nyayo zenu mahali hapo.
15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.
Kweli ninawaambia, itakuwa ya kustahimili zaidi miji ya Sodoma na Gomorah siku ya hukumu kuliko mji huo.
16 “Tazama, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.
Angalia, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu, kwa hiyo iweni na werevu kama nyoka na wapole kama njiwa.
17 “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao.
Muwe waangalifu na watu, watawapeleka kwenye mabaraza, na watawapiga kwenye masinagogi.
18 Nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa.
Na mtaletwa mbele ya wakuu na wafalme kwa ajili yangu, kama ushuhuda kwao na kwa mataifa.
19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo.
Pindi watakapowashutumu, msiwe na wasiwasi jinsi gani au nini cha kuongea, kwa kuwa kitu cha kusema mtapewa kwa wakati huo.
20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.
Kwa kuwa sio ninyi mtakaoongea, lakini Roho wa Baba yenu ataongea ndani yenu.
21 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe.
Ndugu atamwinukia ndugu yake kumwua, na baba kwa mtoto wake. Watoto watainuka dhidi ya wazazi, na kuwasababishia kifo.
22 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
Nanyi mtachukiwa na kila mtu kwa sababu ya jina langu. Lakini yeyote atakayevumilia mpaka mwisho mtu huyo ataokolewa.
23 Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.
Pindi wanapowatesa katika mji huu, kimbilieni mji unaofuata, kwa kweli ninawaambia, hamtakuwa mmekwenda kwenye miji yote ya Israeli kabla ya mwana wa Adam hajarudi.
24 “Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake.
Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumwa aliye juu ya Bwana wake.
25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake!
Inatosha kwa mwanafunzi kwamba awe kama mwalimu wake, na mtumishi kama Bwana wake. Ikiwa wamemwita Bwana wa nyumba Belzabuli, ni kwa kiasi gani zaidi watawakashifu wa nyumba yake!
26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana.
Hivyo basi msiwahofu wao, kwa kuwa hakuna jambo ambalo halitafunuliwa, na hakuna lililofichika ambalo halitajulikana.
27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinongʼonwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba.
Kile ninachowaambia gizani, mkiseme nuruni, na mnachokisikia kwa ulaini masikioni mwenu, mkitangaze mkiwa juu ya nyumba.
28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. (Geenna )
Msiwaogope wale ambao wanaua mwili lakini hawana uwezo wa kuua roho. Badala yake, mwogopeni yule ambaye awezaye kuangamiza mwili na roho kule kuzimu. (Geenna )
29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua.
Je kasuku wawili hawauzwi kwa senti ndogo? Hata hivyo hakuna anayeweza kuanguka chini bila Baba yenu kufahamu.
30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa.
Lakini hata idadi ya nywele zenu zimehesabiwa.
31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
Msiwe na hofu, kwa kuwa mnathamani zaidi kuliko kasuku wengi.
32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Hivyo basi kila mmoja atakaye nikiri mbele za watu, nami pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
33 Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”
Lakini yeye atakaye nikana mbele za watu, nami pia nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.
34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga.
Msifikiri kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani, lakini upanga.
35 Kwa maana nimekuja kumfitini “‘mtu na babaye, binti na mamaye, mkwe na mama mkwe wake;
Kwa kuwa nilikuja kumweka mtu apingane na baba yake, na binti dhidi ya mama yake, na mkwe dhidi ya mama mkwe wake.
36 nao adui za mtu watakuwa ni wale watu wa nyumbani kwake.’
Adui wa mtu watakuwa wale wa nyumbani mwake.
37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu.
Yeye ambaye anampenda baba au mama zaidi kuliko mimi huyo hanistahili. Na yeye anayempenda kijana au binti zaidi kuliko mimi huyo hanistahili.
38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu.
Yeye ambaye hatabeba msalaba na kunifuata mimi hanistahili.
39 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.
Yeye atakayetafuta maisha atayapoteza. Lakini yeye atakayepoteza maisha kwa ajili yangu atayapata.
40 “Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma.
Yeye atakayewakaribisha amenikaribisha mimi, na yeye atakayenikaribisha mimi amemkaribisha yeye aliyenituma mimi.
41 Mtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki.
Na yeye atakayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii atapokea thawabu ya nabii. Na yeye atakayemkaribisha mwenye haki kwa sababu ni mtu wa haki atapokea thawabu ya mtu wa haki.
42 Kama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”
Yeyote atakayempatia mmoja wa wadogo hawa, hata kikombe cha maji ya kunywa ya baridi, kwa sababu yeye ni mwanafunzi, kweli ninawaambia, yeye hawezi kukosa kwa njia yeyote thawabu yake.”