< Mathayo 1 >

1 Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:
Yesu Kristo alikuwa mzawa wa Daudi, mzawa wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake:
2 Abrahamu akamzaa Isaki, Isaki akamzaa Yakobo, Yakobo akawazaa Yuda na ndugu zake,
Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake,
3 Yuda akawazaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari, Peresi akamzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Aramu,
Yuda alimzaa Faresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Faresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami,
4 Aramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni,
Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni,
5 Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu, Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu, Obedi akamzaa Yese,
Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu). Boazi na Ruthi walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese,
6 Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme. Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria.
naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa mke wa Uria).
7 Solomoni akamzaa Rehoboamu, Rehoboamu akamzaa Abiya, Abiya akamzaa Asa,
Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa,
8 Asa akamzaa Yehoshafati, Yehoshafati akamzaa Yoramu, Yoramu akamzaa Uzia,
Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia,
9 Uzia akamzaa Yothamu, Yothamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hezekia,
Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia,
10 Hezekia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia,
Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia,
11 wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.
Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni.
12 Baada ya uhamisho wa Babeli: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli akamzaa Zerubabeli,
Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishomi Babuloni: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerobabeli,
13 Zerubabeli akamzaa Abiudi, Abiudi akamzaa Eliakimu, Eliakimu akamzaa Azori,
Zerobabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori,
14 Azori akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Akimu, Akimu akamzaa Eliudi,
Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi,
15 Eliudi akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo,
Eliudi alimzaa Eleazeri, Eleazeri alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo,
16 naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.
Yakobo alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.
17 Hivyo, kulikuwepo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.
Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.
18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.
Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri.
20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, “Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.”
22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema:
Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:
23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”
“Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli” (maana yake, “Mungu yu pamoja nasi”).
24 Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake.
Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani.
25 Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.
Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.

< Mathayo 1 >