< Marko 7 >

1 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Yesu.
Mafarisayo na baadhi ya waandishi ambao walikuwa wametokea Yerusalemu walikusanyika kumzunguka yeye.
2 Wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani, bila kunawa kama ilivyotakiwa na sheria ya dini ya Wayahudi.
Na waliona kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikula mkate kwa mikono najisi; ambayo haikuoshwa.
3 (Kwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao.
(kwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali mpaka wameosha mikono yao vizuri; wanashikilia utamaduni wa wazee. Wakati
4 Wanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi nyingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.)
Mafarisayo wanaporudi kutoka mahali pa soko, hawali mpaka wameoga kwanza. Na kuna sheria zingine ambazo wanazifuata kabisa, ikiwa ni pamoja na kuosha vikombe, masufuria, vyombo vya shaba, na hata viti vinavyotumika wakati wa chakula.)
5 Kwa hiyo wale Mafarisayo na walimu wa sheria wakamuuliza Yesu, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?”
Mafarisayo na waandishi walimuuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawaishi kulingana na tamaduni za wazee, kwani wanakula mkate pasipo kunawa mikono?”
6 Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa: “‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami.
Lakini yeye aliwaambia, “Isaya alitabiri vizuri kuhusu ninyi wanafiki, aliandika, 'Watu hawa wananiheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali na mimi.
7 Huniabudu bure, nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’
Wananifanyia ibaada zisizo na maana, wakifundisha sheria za wanadamu kama mapokeo yao.'
8 Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.”
Mmeiacha sheria ya Mungu na kushikilia kwa wepesi tamaduni za wanadamu.”
9 Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu!
Na akasema kwao, “Mmeikataa amri ya Mungu kwa urahisi ili kwamba mtunze tamaduni zenu!
10 Kwa mfano, Mose alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’
Kwa kuwa Musa alisema, 'mheshimu baba yako na mama yako,' na 'Yeye asemaye mabaya juu ya baba yake au mama yake hakika atakufa.'
11 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu),
Lakini mnasema, 'kama mtu akisema kwa baba yake au mama, “Msaada wowote ambao mngepokea kutoka kwangu ni hazina ya Hekalu,”' (hiyo ni kusema kwamba, 'imetolewa kwa Mungu')
12 basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake.
hivyo haumruhusu kufanya jambo lolote kwa ajili ya baba au mama yake.
13 Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.”
Mnaifanya amri ya Mungu kuwa bure kwa kuleta tamaduni zenu. Na mambo mengi ya jinsi hiyo mnayoyafanya.”
14 Yesu akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili.
Aliwaita makutano tena na kuwaambia, “Mnisikilize mimi, ninyi nyote, na mnielewe.
15 Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [
Hakuna chochote kutoka nje ya mtu ambacho chaweza kumchafua mtu kiingiapo kwake. Bali ni kile kimtokacho mtu ndicho kimchafuacho.
16 Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”
(Zingatia: mstari huu, “kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia, na asikie” haumo kwenye nakala za kale).
17 Akiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule.
Yesu alipowaacha makutano na kuingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu mfano huo.
18 Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi?
Yesu akasema, “Na ninyi pia bado hamjaelewa? Hamuoni kwamba chochote kimuingiacho mtu hakiwezi kumchafua,
19 Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)
kwa sababu hakiwezi kwenda kwenye moyo wake, lakini kinaingia katika tumbo lake na kisha kinapita kwenda chooni.” Kwa maelezo haya Yesu alivifanya vyakula vyote kuwa safi.
20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.
Alisema, “Ni kile ambacho kinamtoka mtu ndicho kimchafuacho.
21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi,
Kwa kuwa hutoka ndani ya mtu, nje ya moyo, hutoka mawazo maovu, zinaa, wizi, mauaji,
22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu.
uasherati, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, kujamiiana, wivu, kashfa, majivuno, ujinga.
23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”
Maovu haya yote yanatoka ndani, ndiyo yale yamchafuayo mtu.”
24 Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha.
Aliamka kutoka pale na kuondoka kwenda katika mkoa wa Tiro na Sidoni. Aliingia ndani na hakutaka mtu yeyote ajue kuwa alikuwa hapo, lakini haikuwezekana kumficha.
25 Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake.
Lakini ghafla mwanamke, ambaye mtoto wake mdogo alikuwa na roho mchafu, alisikia habari zake, akaja, na akaanguka miguuni pake.
26 Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu.
Mwanamke huyo alikuwa Myunani, wa kabila la Kifoeniki. Alimsihi yeye amfukuze pepo kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
Yesu akamwambia mwanamke, “Waache watoto walishwe kwanza, kwa kuwa sio sawa kuuchukua mkate wa watoto na kuwatupia mbwa.”
28 Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.”
Lakini mwanamke akamjibu na kusema, “Ndiyo Bwana, hata mbwa chini ya meza hula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.”
Akamwambia, “Kwa kuwa umesema hivi, uko huru kwenda. Pepo ameshamtoka binti yako.”
30 Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.
Mwanamke alirudi nyumbani kwake na akamkuta binti yake amelala kitandani, na pepo alikuwa amemtoka.
31 Kisha Yesu akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli.
Yesu alitoka tena nje ya mkoa wa Tiro na kupitia Sidoni kuelekea Bahari ya Galilaya mpaka kanda ya Dikapolisi.
32 Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu na amponye.
Na wakamletea mtu aliyekuwa kiziwi na alikuwa hawezi kuzungumza vizuri, walimsihi Yesu aweke mikono juu yake.
33 Baadaye Yesu akampeleka yule kiziwi kando mbali na watu, Yesu akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu.
Alimtoa nje ya kusanyiko kwa siri, na akaweka vidole vyake kwenye masikio yake, na baada ya kutema mate, aligusa ulimi wake.
34 Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akavuta hewa ndani kwa nguvu akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”)
Alitazama juu mbinguni, akahema na kumwambia, “Efata,” hiyo ni kusema “funguka!”
35 Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.
Na muda ule ule masikio yakafunguka, na kilichokuwa kimezuia ulimi kiliharibiwa na akaweza kuongea vizuri.
36 Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowazuia, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii.
Na aliwaamuru wasimwambie mtu yeyote. Lakini kadri alivyowaamuru, ndivyo walivyotangaza habari hizo kwa wingi.
37 Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”
Hakika walishangazwa, na kusema, “Amefanya kila kitu vizuri. Hata amewafanya viziwi kusikia na mabubu kuongea.”

< Marko 7 >