< Marko 3 >

1 Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na huko palikuwa na mtu aliyepooza mkono.
Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza.
2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.
Humo baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya sabato ili wapate kumshtaki.
3 Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”
Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, “Njoo hapa katikati.”
4 Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.
Kisha, akawauliza, “Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao hawakusema neno.
5 Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa kabisa!
Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, “Nyosha mkono wako!” Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena.
6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya shauri la kumuua Yesu wakiwa na Maherode.
Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu.
7 Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata.
Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea,
8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni.
Idumea, ng'ambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda.
9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.
Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga.
10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa.
Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa.
11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”
Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaaza sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!”
12 Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.
Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu.
13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.
Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea,
14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye, na awatume kwenda kuhubiri
naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume, wakae naye, awatume kuhubiri
15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.
na wawe na mamlaka ya kuwafukuza pepo.
16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro);
Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro),
17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo);
Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake “wanangurumo”),
18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo,
Andrea na Filipo, Batholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanani na
19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.
Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.
20 Kisha Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula.
Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula.
21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”
Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba amepatwa na wazimu.
22 Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Anatoa pepo wachafu kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu!”
Nao walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, “Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo.”
23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani?
Hapo Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano, “Shetani anawezaje kumfukuza Shetani?
24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.
Ikiwa utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopigana, utawala huo hauwezi kudumu.
25 Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.
Tena, ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo itaangamia.
26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia.
Ikiwa basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali utaangamia kabisa.
27 Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali zake.
“Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang'anya mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kumnyang'anya mali yake.
28 Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa.
“Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote;
29 Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.” (aiōn g165, aiōnios g166)
lakini anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya dhambi ya milele.” (aiōn g165, aiōnios g166)
30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”
(Yesu alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”)
31 Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakasimama nje, wakamtuma mtu kumwita.
Mama yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe kutaka kumwona.
32 Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
Umati wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kukuona.”
33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”
Yesu akawaambia, “Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?”
34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.
Hapo akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, “Tazameni! Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.
35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”
Mtu yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu.”

< Marko 3 >