< Marko 2 >
1 Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba amerudi nyumbani.
Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani.
2 Hivyo watu wengi wakakusanyika kiasi kwamba hapakubaki nafasi yoyote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.
Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,
3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne.
wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne.
4 Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia.
Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya dari iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.
5 Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”
Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”
6 Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao,
Baadhi ya walimu wa Sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,
7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”
“Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake.”
8 Mara moja Yesu akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, “Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’?
Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu aliyepooza, Umesamehewa dhambi zako, au kumwambia, Inuka! Chukua mkeka wako utembee?
10 Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza,
Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,
11 “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.”
“Nakwambia simama, chukua mkeka wako uende nyumbani!”
12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”
Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, “Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili.”
13 Yesu akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akaanza kuwafundisha.
Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha.
14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru, akamwambia, “Nifuate.” Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.
Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Lawi akasimama, akamfuata.
15 Yesu alipokuwa akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi pamoja na “wenye dhambi” walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimfuata.
Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake.
16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na “wenye dhambi,” wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Yesu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
Basi, baadhi ya walimu wa Sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watoza ushuru, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”
17 Yesu aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Yesu alipowasikia, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi.”
18 Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumuuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?”
Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
19 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati angali pamoja nao? Wakati bwana arusi bado yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.
Yesu akajibu, “Walioalikwa harusini wanawezaje kufunga kama bwana harusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana harusi hawawezi kufunga.
20 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Siku hiyo ndipo watakapofunga.
Lakini wakati utafika ambapo bwana harusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.
21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kitachanika kutoka ile nguo iliyochakaa, nayo itachanika zaidi.
“Hakuna mtu anayekata kiraka kutoka katika nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama akifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi.
22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, nayo hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”
Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama akifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!”
23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.
Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano.
24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”
Mafarisayo wakawaambia, “Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya wakati wa Sabato?”
25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula?
Yesu akawajibu, “Je, hamjapata kusoma juu ya kile alichofanya Daudi wakati alipohitaji chakula? Yeye pamoja na wenzake waliona njaa,
26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.”
naye akaingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa Kuhani Mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake.”
27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.
Basi, Yesu akawaambia, “Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato!
28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”
Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ni Bwana hata wa Sabato.”