< Marko 14 >

1 Zilikuwa zimebaki siku mbili tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumkamata Yesu kwa hila na kumuua.
Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Makuhani wakuu na walimu wa Sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.
2 Lakini walisema, “Tusilifanye jambo hili wakati wa Sikukuu, maana watu wanaweza wakafanya ghasia.”
Lakini walisema, “Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.”
3 Yesu alikuwa Bethania nyumbani kwa Simoni aliyekuwa na ukoma. Wakati alipokuwa ameketi mezani akila chakula cha jioni, mwanamke mmoja aliingia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa. Akaivunja hiyo chupa, akamiminia hayo manukato kichwani mwa Yesu.
Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani.
4 Baadhi ya watu waliokuwepo pale walikuwa wakisemezana wao kwa wao, “Upotevu huu wote ni wa nini?
Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika wakajisemea, “Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya?
5 Mafuta haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari 300, na fedha hizo wakapewa maskini.” Wakamkemea vikali huyo mwanamke.
Yangaliweza kuuzwa kwa fedha kiasi cha denari mia tatu, wakapewa maskini!” Wakamkemea huyo mama.
6 Lakini Yesu akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Mwacheni! Yeye amenitendea jambo zuri sana.
Lakini Yesu akawaambia, “Mwacheni; kwa nini mnamsumbua? Amenitendea jambo jema.
7 Maskini mtakuwa nao siku zote na mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaotaka. Lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.
Maskini mnao daima pamoja nanyi; mnaweza kuwasaidia wakati wowote mnaopenda. Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.
8 Huyu mwanamke amenitendea lile aliloweza. Ameumiminia mwili wangu manukato ili kuniandaa kwa maziko yangu.
Yeye amefanya alivyoweza; ameupaka mwili wangu marashi kuutayarisha kwa maziko.
9 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”
Nawaambieni kweli, popote ulimwenguni Habari Njema itakapohubiriwa, kitendo hiki alichofanya kitatajwa kwa ajili ya kumkumbuka.”
10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi kumi na wawili, akaenda kwa viongozi wa makuhani ili kumsaliti Yesu kwao.
Kisha Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, alienda kwa makuhani wakuu ili kumsaliti Yesu.
11 Walifurahi sana kusikia jambo hili na wakaahidi kumpa fedha. Hivyo yeye akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti.
Makuhani wakuu waliposikia habari hiyo, walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Basi, Yuda akaanza kutafuta nafasi ya kumsaliti Yesu.
12 Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo kwa desturi mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”
Siku ya kwanza ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wakati ambapo mwana kondoo wa Pasaka huchinjwa, wanafunzi wake walimwuliza, “Wataka tukuandalie wapi karamu ya Pasaka?”
13 Basi akawatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake, akawaambia, “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni.
Basi Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake akiwaambia, “Nendeni mjini, nanyi mtakutana na mtu anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni
14 Mwambieni mwenye nyumba ile atakayoingia, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba changu cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’
mpaka katika nyumba atakayoingia, mkamwambie mwenye nyumba, Mwalimu anasema: wapi chumba changu ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?
15 Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kilichopambwa tena kilicho tayari. Tuandalieni humo.”
Naye atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani kilichotayarishwa na kupambwa. Tuandalieni humo.”
16 Wale wanafunzi wakaondoka na kwenda mjini, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
Wanafunzi wakaondoka, wakaenda mjini, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia. Wakaandaa karamu ya Pasaka.
17 Ilipofika jioni, Yesu akaja pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili.
Ilipokuwa jioni, Yesu alifika pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
18 Walipoketi mezani wakila, Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti, mmoja anayekula pamoja nami.”
Walipokuwa mezani wakila, Yesu alisema, “Kweli nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami, atanisaliti.”
19 Wakaanza kuhuzunika na kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”
Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?”
20 Akawajibu, “Ni mmoja miongoni mwenu ninyi kumi na wawili, yule anayechovya mkate kwenye bakuli pamoja nami.
Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu ninyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli.
21 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa.”
Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!”
22 Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni mle; huu ndio mwili wangu.”
Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.”
23 Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wote wakanywa kutoka humo.
Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa; nao wote wakanywa katika kikombe hicho.
24 Akawaambia, “Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.
Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi.
25 Amin, nawaambia, sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya katika Ufalme wa Mungu.”
Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika Ufalme wa Mungu.”
26 Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.
Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.
27 Yesu akawaambia, “Ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo watatawanyika.’
Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Ninyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema: Nitampiga mchungaji nao kondoo watatawanyika.
28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya.”
29 Petro akasema, “Hata kama wengine wote watakuacha, mimi sitakuacha.”
Petro akamwambia “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!”
30 Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia; leo, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, wewe mwenyewe utanikana mara tatu.”
Yesu akamwambia, “Kweli nakwambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.”
31 Lakini Petro akasisitiza zaidi, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe.” Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo.
32 Wakaenda mahali paitwapo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa, nami niende nikaombe.”
Basi, wakafika katika bustani iitwayo Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.”
33 Kisha akawachukua pamoja naye Petro, Yakobo na Yohana. Akaanza kuhuzunika sana na kutaabika.
Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.
34 Akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe.”
Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe.”
35 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba kwamba kama ingewezekana saa hiyo ya mateso imwondokee.
Akaenda mbele kidogo, akajitupa chini kifudifudi, akasali kwamba, kama ingewezekana, asiipitie saa hiyo ya mateso.
36 Akasema, “Abba, Baba, mambo yote yawezekana kwako. Niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali vile upendavyo wewe.”
Akasema, “Baba yangu, kwako mambo yote yanawezekana. Uniondolee kikombe hiki; lakini isiwe kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”
37 Akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Simoni, umelala? Je, hukuweza kukesha hata kwa saa moja?
Kisha akarudi kwa wanafunzi wale watatu, akawakuta wamelala. Basi, akamwuliza Petro, “Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?”
38 Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”
Kisha akawaambia, “Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
39 Akaenda tena kuomba, akisema maneno yale yale.
Akaenda kusali tena akirudia maneno yaleyale.
40 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. Nao hawakujua la kumwambia.
Kisha akarudi tena, akawakuta wamelala. Macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. Hawakujua la kumjibu.
41 Akaja mara ya tatu, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Imetosha! Saa imewadia. Tazameni, Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi.
Alipowajia mara ya tatu aliwaambia, “Mnalala bado na kupumzika? Sasa imetosha! Saa imefika! Mwana wa Mtu anakabidhiwa kwa watu waovu.
42 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”
Amkeni, twendeni zetu. Tazameni, yule atakayenisaliti amekaribia.”
43 Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee.
Yesu alipokuwa bado anasema, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika pamoja na umati wa watu wenye mapanga na marungu. Watu hao walikuwa wametumwa na makuhani wakuu, walimu wa Sheria na wazee.
44 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.”
Msaliti Yuda alikuwa amewapa ishara: “Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni, mkampeleke chini ya ulinzi.”
45 Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.” Akambusu.
Yuda alipofika tu, alimwendea Yesu moja kwa moja, akasema, “Mwalimu!” Kisha akambusu.
46 Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi.
Basi, hao watu wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.
47 Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
Mmoja wa wale waliokuwa wamesimama hapo pamoja na Yesu akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
48 Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi?
Yesu akawaambia, “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang'anyi?
49 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.”
Kila siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini sasa lazima Maandiko Matakatifu yatimie.”
50 Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
Hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
51 Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata,
Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anamfuata Yesu akiwa amevaa shuka. Nao wakajaribu kumkamata.
52 alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
Lakini yeye akaponyoka, akaiachilia ile shuka, akakimbia uchi.
53 Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja.
Basi, wakampeleka Yesu kwa Kuhani Mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na walimu wa Sheria walikuwa wamekutanika.
54 Petro akamfuata kwa mbali, hadi uani kwa kuhani mkuu. Huko akaketi pamoja na walinzi, akiota moto.
Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ya wa Kuhani Mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto.
55 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote.
Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakupata.
56 Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.
Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana.
57 Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema:
Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema:
58 “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’”
“Tulimsikia mtu huyu akisema, Nitaliharibu Hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono.”
59 Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.
Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana.
60 Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”
Basi, Kuhani Mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?”
61 Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote. Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”
Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?”
62 Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa Mwenyezi, akija katika mawingu ya mbinguni.”
63 Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi?
Hapo Kuhani Mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi?
64 Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?” Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo.
Mmesikia kufuru yake! Ninyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa.
65 Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.
Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani aliyekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi.
66 Petro alipokuwa bado yuko chini kwenye ua wa jumba la kifalme, tazama akaja mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu.
Petro alipokuwa bado chini ukumbini, mmoja wa wajakazi wa kuhani Mkuu alikuja.
67 Alipomwona Petro akiota moto, akamtazama sana, akamwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”
Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.”
68 Lakini Petro akakana, akasema, “Sijui wala sielewi unalosema.” Naye akaondoka kuelekea kwenye njia ya kuingilia.
Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika.
69 Yule mtumishi wa kike alipomwona mahali pale, akawaambia tena wale waliokuwa wamesimama hapo, “Huyu mtu ni mmoja wao.”
Yule mjakazi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, “Mtu huyu ni mmoja wao.”
70 Lakini Petro akakana tena. Baada ya muda kidogo wale waliokuwa wamesimama hapo karibu na Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya!”
Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya.”
71 Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui huyu mtu mnayesema habari zake!”
Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, “Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake.”
72 Papo hapo jogoo akawika mara ya pili. Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alikuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Akavunjika moyo, akalia sana.
Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Petro akabubujika machozi.

< Marko 14 >