< Marko 13 >
1 Yesu alipokuwa akitoka Hekaluni, mmojawapo wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa, na majengo haya yalivyo mazuri!”
Yesu alipokuwa akitembea kutoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake akamwuliza, “Mwalimu, tazama mawe haya yakushangaza na majengo!”
2 Ndipo Yesu akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali yote yatabomolewa.”
Akamwambia, Unaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalo salia juu ya jingine ambalo halitaangushwa chini”.
3 Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani,
Naye alipokuwa amekaa juu ya Mlima wa Mizeituni nyuma ya hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamwuliza kwa siri,
4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”
“Tuambie, mambo haya yatakuwa lini? Ni nini dalili ya mambo haya kutokea?”
5 Yesu akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye.
Yesu alianza kuwaambia, “Kuweni makini kwamba mtu yoyote asiwapotoshe.
6 Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi.
Wengi watakuja kwa jina langu wakisema, 'Mimi ndiye', na watawapotosha wengi.
7 Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
Mtakaposikia vita na tetesi za vita, msiogope; mambo haya hayana budi kutokea, lakini mwisho bado.
8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
Taifa litainuka kinyume na taifa jingine, na ufalme kinyume na ufalme. Patakuwa na matetemeko sehemu mbalimbali, na njaa. Huu ni mwanzo wa utungu.
9 “Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao.
Iweni macho. Watawapeleka hadi mabarazani, na mtapingwa katika masinagogi. Mtasimamishwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kama ushuhuda kwao.
10 Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia.
Lakini injili lazima kwanza ihubiriwe kwa mataifa yote.
11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.
Watakapo wakamata na kuwakabidhi, msiogope kuhusu kile mtakachosema. Ndani ya muda huo, mtapewa nini cha kusema; hamtakuwa ninyi mtakaoongea, bali Roho Mtakatifu.
12 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe.
Ndugu atamshitaki ndugu kuuawa, baba na mtoto wake. Watoto watasimama kinyume cha baba zao na kuwasababisha kuuawa.
13 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
Mtachukiwa na kila mtu kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, mtu huyo ataokoka.
14 “Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.
Mtakapoona chukizo la uharibifu limesimama pale lisipotakiwa kusimama (asomaye na afahamu), ndipo walioko ndani ya Yuda wakimbilie milimani,
15 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote.
naye aliyeko juu ya nyumba asishuke chini ya nyumba, au kuchukua chochote kilichoko nje,
16 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.
na aliyeko shambani asirudi kuchukua vazi lake.
17 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!
Lakini ole wao wanawake wenye mimba na wanyonyeshao katika siku hizo!
18 Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi.
Ombeni kwamba isitokee wakati wa baridi.
19 Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka leo, na wala haitakuwako tena kamwe.
Kwani patakuwa na mateso makubwa, ambayo hayajawahi kutokea, tangu Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka sasa, hapana, wala haitatokea tena.
20 Kama Bwana asingelifupisha siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu yeyote. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo.
Mpaka Bwana atakapopunguza siku, hakuna mwili utakaookoka, lakini kwa ajili ya wateule, atakaowachagua, atapunguza namba za siku.
21 Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristohuyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki.
Wakati huo kama mtu yeyote atawaambia, Tazama, Kristo yuko hapa!' au 'Tazama, yuko pale!' msiamini.
22 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule.
Kwani Wakristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea na watatoa ishara na maajabu, ili kwamba, wawadanganye, yamkini hata wateule.
23 Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.
Iweni macho! Nimekwisha wambia haya yote kabla ya wakati.
24 “Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki, “‘jua litatiwa giza nao mwezi hautatoa nuru yake;
Lakini baada ya mateso ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake,
25 nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’
nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu zilizoko mbinguni zitatikisika.
26 “Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.
Ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu kubwa na utukufu.
27 Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.
Ndipo atatuma malaika zake na atawakusanya pamoja wateule wake kutoka pande kuu nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
28 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
Kwa mtini jifunzeni. Kama tawi liwezavyo kutoa na kuweka haraka majani yake, ndipo mtajua kwamba kiangazi kiko karibu.
29 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.
Ndivyo ilivyo, mtakapoona mambo haya yakitokea, jueni kwamba yuko karibu, na malango.
30 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
Kweli, nawambieni, hiki kizazi hakitapita mbali kabla mambo haya hayajatokea.
31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
32 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.
Lakini kuhusu siku hiyo au saa, hakuna ajuaye, hata malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia.
Iweni macho, Tazama, kwa sababu hamjui ni muda gani yatatokea. (Zingatia: Mstari huu, “Muwe waangalifu, Tazameni na ombeni kwa sababu...” haumo kwenye nakala za kale).
34 Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe.
Ni kama mtu anayeenda safarini: akaacha nyumba yake, na kumweka mtumwa wake kuwa mtawala wa nyumba, kila mmoja na kazi yake. Na kumwamuru mlinzi kukaa macho.
35 “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko.
Kwa hiyo iweni macho! Kwani hamjui ni lini bwana wa nyumba atakaporudi nyumbani, yawezekana ni jioni, usiku wa manane, wakati jogoo atakapowika, au asubuhi.
36 Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala.
Kama akija ghafla, asikukute umelala.
37 Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’”
Kile nikisemacho kwako nakisema kwa kila mtu: Kesheni”!