< Luka 1 >
1 Kwa kuwa watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotukia katikati yetu,
Wengi wamejitahidi kuweka katika mpangilio simulizi kuhusu masuala ambayo yametimizwa kati yetu,
2 kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale waliokuwa mashahidi walioyaona na watumishi wa Bwana,
kama walivyotupatia sisi, ambao tangu mwanzo ni mashahidi wa macho na watumishi wa ujumbe.
3 mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo, ewe mtukufu Theofilo,
Hivyo nami pia, baada ya kuchuguza kwa uangalifu chanzo cha mambo haya yote tokea mwanzo - nimeona ni vema kwangu pia kukuandikia katika mpangilio wake - mheshimiwa sana Theofilo.
4 ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa.
Ili kwamba uweze kujua ukweli wa mambo uliyofundishwa.
5 Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni.
Katika siku za Herode, mfalme wa Yudea, palikuwa na kuhani fulani aliyeitwa Zekaria, wa ukoo wa Abiya. Mke wake alitoka kwa binti za Haruni, na jina lake aliitwa Elizabeti.
6 Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama.
Wote walikuwa wenye haki mbele za Mungu; walitembea bila lawama katika amri zote na maagizo ya Bwana.
7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana.
Lakini hawakuwa na mtoto, kwasababu Elizabethi alikuwa tasa, na kwa wakati huu wote wawili walikuwa wazee sana.
8 Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu,
Sasa ilitokea kwamba Zakaria alikuwa katika uwepo wa Mungu, akiendelea na wajibu wa kikuhani katika utaratibu wa zamu yake.
9 alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba.
Kulingana na desturi ya kuchagua ni kuhani yupi atakayehudumu, alikuwa amechaguliwa kwa kura kuingia katika hekalu la Bwana na hivyo angefukiza uvumba.
10 Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.
Kundi lote la watu lilikuwa likiomba nje wakati wa kufukizwa kwa ufumba.
11 Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria.
Sasa malaika wa Bwana alimtokea na kasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia.
12 Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu.
Zakaria alitishika alipomuona; hofu ikamwangukia.
13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana.
Lakini malaika akamwambia, “Usiogope Zakaria, kwasababu maombi yako yamesikika. Mke wako Elizabeth atakuzalia mwana. Jina lake utamwita Yohana.
14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
Utakuwa na furaha na uchangamfu, na wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.
15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.
Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele ya macho ya Bwana. Hatakunywa divai au kinywaji kikali, na atakuwa amejazwa na Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
16 Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao.
Na watu wengi wa Israel watageuzwa kwa Bwana Mungu wao.
17 Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.”
Atakwenda mbele za uso wa Bwana katika roho na nguvu ya Eliya. Atafanya hivi ili kurejesha mioyo ya baba kwa watoto, ili kwamba wasiotii wataenenda katika hekima ya wenye haki. Atafanya hivi kuweka tayari kwa Bwana watu ambao wameandaliwa kwa ajili yake.”
18 Zekaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”
Zakaria akamwambia malaika, “Nitawezaje kujua hili? Kwasababu mimi ni mzee na mke wangu miaka yake imekuwa mingi sana.”
19 Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema.
Malaika akajibu na kumwambia, “Mimi ni Gabrieli, ambaye husimama mbele za Mungu. Nilitumwa kukwambia, kukuletea habari hii njema.
20 Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”
Na tazama, hutaongea, utakuwa kimya, hutaweza kuongea mpaka siku ile mambo haya yatakapotokea. Hii ni kwasababu ulishindwa kuamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati mwafaka.”
21 Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni.
Sasa watu walikuwa wakimsubiri Zakaria. Walishangazwa kwamba alikuwa anatumia muda mwingi hekaluni.
22 Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.
Lakini alipotoka nje, hakuweza kuongea nao. Wakatambua kwamba alikuwa amepata maono alipokuwa hekaluni. Aliendelea kuonesha ishara na alibaki kimya.
23 Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake.
Ikatokea kwamba siku za huduma yake zilipokwisha aliondoka kurudi nyumbani kwake.
24 Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.
Baada ya Zakaria kurudi nyumbani kutoka kwenye huduma yake hekaluni, mke wake akawa mjamzito. Naye hakutoka nyumbani mwake kwa muda wa miezi mitano. Akasema,
25 Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”
“Hili ndilo amabalo Bwana amefanya kwangu aliponitazama kwa upendeleo ili kuiondoa aibu yangu mbele za watu.”
26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti,
Sasa, katika mwezi wa sita wa mimba ya Elizabeti, Mungu alimwambia malaika Gabrieli kwenda kwenye mji wa Galilaya uitwao Nazareti,
27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria.
kwa bikra aliyekuwa ameposwa na mwanaume ambaye jina lake lilikuwa Yusufu. Yeye alikuwa wa ukoo wa Daudi, na jina la bikra huyo lilikuwa Mariamu.
28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!”
Akaja kwake na akasema, “Salaam, wewe uliyepokea neema kuu! Bwana amependezwa nawe.”
29 Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?”
Lakini maneno ya malaika yalimchanganya na hakuelewa kwa nini malaika alisema salaam hii ya ajabu kwake.
30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu.
Malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu, maana umepata neema kutoka kwa Mungu.
31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Yesu.
Na tazama, utabeba mimba katika tumbo lako na utazaa mwana. Nawe utamwita jina lake 'Yesu.'
32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake.
Atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake.
33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” (aiōn )
Atatawala juu ya ukoo wa Yakobo milele na ufalme wake hautakuwa na mwisho. (aiōn )
34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”
Mariamu akamwambia malaika, hili litatokea kwa namna gani, maana sijawahi kulala na mwanaume yeyote?
35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.
Malaika akajibu na akamwambia, “Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na nguvu ya Aliye Juu Sana itakuja juu yako. Kwa hiyo, mtakatifu atakayezaliwa ataitwa Mwana wa Mungu.
36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa.
Na tazama, ndugu yako Elizabeti anaujauzito wa mwana kwenye umri wake wa uzee. Huu ni mwezi wa sita kwake, ambaye alikuwa anaitwa mgumba.
37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”
Maana hakuna lisilowezekana kwa Mungu.”
38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.
Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa kike wa Bwana. Acha iwe hivyo kwangu sawa sawa na ujumbe wako.” Kisha malaika akamwacha.
39 Wakati huo Maria akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye vilima vya Uyahudi.
Ndipo katika siku hizo Mariamu aliondoka na kwa haraka alikwenda katika nchi ya vilima, kwenye mji katika nchi ya Yudea.
40 Akaingia nyumbani kwa Zekaria na kumsalimu Elizabeti.
Alikwenda nyumbani mwa Zekaria na akamsalimia Elizabeti.
41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu,
Sasa, ilitokea kwamba Elizabeti aliposikia salamu ya Mariamu, mtoto tumboni mwake akaruka, na Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu.
42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa.
Akapaza sauti yake na kusema kwa sauti kuu, “umebarikiwa wewe zaidi miongoni mwa wanawake, na mtoto aliyemo tumboni mwako amebarikiwa.
43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
Na imekuwaje kwangu kwamba, mama wa Bwana wangu ilipasa aje kwangu?
44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
Kwa kuwa tazama, iliposikika masikoni mwangu sauti ya kusalimia kwako, mtoto tumboni mwangu akaruka kwa furaha.
45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”
Na amebarikiwe mwanamke yule ambaye aliamini ya kwamba ungetokea ukamilifu wa mambo yale aliyoambiwa kutoka kwa Bwana.”
46 Naye Maria akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Mariamu akasema, nafsi yangu inamsifu Bwana,
47 nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu,
na roho yangu imefurahi katika Mungu Mwokozi wangu.
48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,
Kwa maana ameiangalia hali ya chini ya mtumishi wake wa kike. Tazama, tangu sasa katika vizazi vyote wataniita mbarikiwa.
49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu.
Kwa maana yeye aliyemweza amefanya mambo makubwa kwangu, na jina lake ni takatifu.
50 Rehema zake huwaendea wale wamchao, kutoka kizazi hadi kizazi.
Rehema yake inadumu toka kizazi hata kizazi kwa wale wanao mheshimu yeye.
51 Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao.
Ameonesha nguvu kwa mkono wake; amewatawanya wale ambao walijivuna juu ya mawazo ya mioyo yao.
52 Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi, lakini amewainua wanyenyekevu.
Amewashusha chini wana wa wafalme toka katika viti vyao vya enzi na kuwainua juu walio na hali ya chini.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.
Aliwashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.
54 Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu
Ametoa msaada kwa Israeli mtumishi wake, ili kukumbuka kuonesha rehema
55 Abrahamu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.” (aiōn )
(kama alivyosema kwa baba zetu) kwa Abrahamu na uzao wake milele.” (aiōn )
56 Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.
Mariamu alikaa na Elizabeti yapata miezi mitatu hivi ndipo akarudi nyumbani kwake.
57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume.
Sasa wakati ulikuwa umewadia kwa Elizabeti kujifungua mtoto wake na akajifungua mtoto wa kiume.
58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.
Jirani zake na ndugu zake walisikia jinsi Bwana alivyoikuza rehema kwake, na wakafurahi pamoja naye.
59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake.
Sasa ilitokea siku ya nane kwamnba walikuja kumtahiri mtoto. Ingewapasa kumwita jina lake, “Zekaria,” kwa kuzingatia jina la baba yake,
60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”
Lakini mama yake akajibu na kusema, “Hapana; ataitwa Yohana.”
61 Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”
Wakamwambia, hakuna hata mmoja katika ndugu zako anayeitwa kwa jina hili.”
62 Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani.
Wakamfanyia ishara baba yake kuashiria yeye alitaka jina aitwe nani.
63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.”
Baba yake akahitaji kibao cha kuandikia, na akaandika, “Jina lake ni Yohana.” Wote wakashangazwa na hili.
64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
Ghafla mdomo wake ukafunguliwa na ulimi wake ukawa huru. Akaongea na kumsifu Mungu.
65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote.
Hofu ikawajia wote walioishi karibu nao. Mambo haya yakaenea katika nchi yote ya vilima vya Yudea.
66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
Na wote walioyasikia wakayatunza mioyoni mwao, wakisema, “Mtoto huyu kuwa wa namna gani?” Kwasababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:
Baba yake Zekaria alijazwa na Roho Mtakatifu na akatoa unabii, akisema,
68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.
“Asifiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sababu amesaidia na alishughulikia wokovu kwa watu wake.
69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,
Ametuinulia pembe ya wokovu katika nyumba ya mtumishi wake Daudi, kutoka miongoi mwa mwa ukoo wa mtumishi wake Daudi,
70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake watakatifu tangu zamani, (aiōn )
kama alivyosema kwa kinywa cha manabii wake waliokuweko katika nyakati za kale. (aiōn )
71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu, na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:
Atatuoka kutoka kwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu na kukumbuka Agano lake takatifu,
Atafanya hivi kuonesha rehema kwa baba zetu, na kukumbuka agano lake takatifu,
73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:
kiapo alichokisema kwa Abrahamu baba yetu.
74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu
Aliapa kuthibitha kwamba ingewezekana kumtumikia Yeye bila hofu, baada ya kuokolewa kutoka katika mikononi ya adui zetu.
75 katika utakatifu na haki mbele zake, siku zetu zote.
katika utakatifu na haki mbele zake siku zetu zote.
76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana; kwa kuwa utamtangulia Bwana na kuandaa njia kwa ajili yake,
Ndiyo, na wewe mtoto, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana, kwa kuwa utaenenda mbele za uso wa Bwana ili kumwandalia njia, kuwaandaa watu kwa ajili ya ujio wake,
77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovu utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,
kuwafahamisha watu wake kwamba, wataokolewa kwa njia ya kusamehewa dhambi zao.
78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu, nuru itokayo juu itatuzukia
Hili litatokea kwa sababu ya huruma ya Mungu wetu, sababu ambayo jua tokea juu litatujia,
79 ili kuwaangazia wale waishio gizani na katika uvuli wa mauti, kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”
kuangaza kwao wakaao gizani na katika uvuli wa mauti. Atafanya hivi kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.”
80 Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionyesha hadharani kwa Waisraeli.
Sasa, yule mtoto akakua na kuwa mwenye nguvu rohoni na alikaa nyikani mpaka siku ya kujitokeza kwake kwa Israeli.