< Luka 9 >
1 Yesu kisha akawaita wale kumi na wawili pamoja, akawapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote,
2 kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.
3 Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote safarini: sio fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, hata msichukue kanzu ya ziada.
4 Katika nyumba yoyote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.
5 Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”
6 Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
7 Basi Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za yote yaliyotendeka. Naye akafadhaika, kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu.
8 Wengine wakasema Eliya amewatokea, na wengine wakasema kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka.
9 Herode akasema, “Yohana nilimkata kichwa. Lakini ni nani huyu ambaye ninasikia mambo kama haya kumhusu?” Akatamani sana kumwona.
10 Mitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji uitwao Bethsaida.
11 Lakini umati wa watu ukafahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.
12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakaenda kwa Yesu na kumwambia, “Waage makutano ili waende vijijini jirani na mashambani, ili wapate chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”
13 Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Nao wakajibu, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili. Labda twende tukanunue chakula cha kuwatosha watu hawa wote.”
14 Walikuwako wanaume wapatao 5,000. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.”
15 Wanafunzi wakafanya hivyo, wakawaketisha wote.
16 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega. Kisha akawapa wanafunzi ili wawagawie watu.
17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.
18 Wakati mmoja, Yesu alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”
19 Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya, na bado wengine husema kwamba ni mmoja wa manabii wa kale amefufuka kutoka kwa wafu.”
20 Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu.”
21 Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote jambo hilo.
22 Yesu akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na itampasa auawe, lakini siku ya tatu kufufuliwa kutoka mauti.”
23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.
24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.
25 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake?
26 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba, pamoja na malaika watakatifu.
27 Amin, nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu.”
28 Yapata siku nane baada ya Yesu kusema hayo, aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana, akaenda nao mlimani kuomba.
29 Alipokuwa akiomba, sura ya uso wake ikabadilika, nayo mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi.
30 Ghafula wakawaona watu wawili, ndio Mose na Eliya, wakizungumza naye.
31 Walionekana katika utukufu wakizungumza na Yesu kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu.
32 Petro na wenzake walikuwa wamelala usingizi mzito. Walipoamka, wakaona utukufu wa Yesu na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.
33 Mose na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Lakini Petro alikuwa hajui asemacho.
34 Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu, likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu.
35 Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, niliyemchagua. Msikieni yeye.”
36 Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Yesu akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu yeyote yale waliyokuwa wameyaona.
37 Kesho yake waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu.
38 Mtu mmoja katika ule umati wa watu akapaza sauti, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, kwani ndiye mtoto wangu wa pekee.
39 Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige kelele, kisha humwangusha na kumtia kifafa hata akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana, na hamwachi ila mara chache.
40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
41 Yesu akawajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Mlete mwanao hapa.”
42 Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, na akamrudisha kwa baba yake.
43 Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu walikuwa wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Yesu, yeye akawaambia wanafunzi wake:
44 “Sikilizeni kwa makini haya nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.”
45 Lakini wao hawakuelewa alimaanisha nini. Maana ya maneno hayo ilifichika kwao, hivyo hawakuyaelewa, nao wakaogopa kumuuliza maana yake.
46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote.
47 Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, naye akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake.
48 Kisha akawaambia, “Yeyote amkaribishaye mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi, na yeyote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma. Kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”
49 Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
50 Yesu akasema, “Msimzuie, kwa sababu yeyote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”
51 Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu.
52 Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu;
53 lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anakwenda zake Yerusalemu.
54 Wanafunzi wake, yaani Yakobo na Yohana, walipoona hayo, wakasema: “Bwana, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?”
55 Yesu akageuka na kuwakemea,
56 nao wakaenda kijiji kingine.
57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote uendako.”
58 Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.” Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”
61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa yangu.”
62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”