< Luka 8 >

1 Baada ya haya Yesu alikwenda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye,
Baada ya hayo, Yesu alipitia katika miji na vijiji akitangaza Habari Njema za Ufalme wa Mungu. Wale kumi na wawili waliandamana naye.
2 pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa. Miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba;
Pia wanawake kadhaa ambao Yesu alikuwa amewatoa pepo wabaya na kuwaponya magonjwa, waliandamana naye. Hao ndio akina Maria (aitwaye Magdalene), ambaye alitolewa pepo wabaya saba;
3 Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode; Susana; na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.
Yoana, mke wa Kuza, mfanyakazi mkuu wa Herode; Susana na wengine kadhaa. Hao wanawake walikuwa wakiwatumikia kwa mali yao wenyewe.
4 Umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka kila mji, akawaambia mfano huu:
Kundi kubwa la watu lilikuwa linakusanyika, na watu walikuwa wanamjia Yesu kutoka kila mji. Naye akawaambia mfano huu:
5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila.
“Mpanzi alikwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akipanda zile mbegu, nyingine zilianguka njiani, na wapita njia wakazikanyaga, na ndege wakazila.
6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu.
Nyingine zilianguka penye mawe, na baada ya kuota zikanyauka kwa kukosa maji.
7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea.
Nyingine zilianguka kati ya miti ya miiba. Ile miti ya miiba ilipoota ikazisonga.
8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.” Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikaota na kuzaa asilimia mia.” Baada ya kusema hayo, akapaaza sauti, akasema, “Mwenye masikio na asikie!”
9 Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo.
Wanafunzi wake wakamwuliza Yesu maana ya mfano huo.
10 Naye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili, “‘ingawa wanatazama, wasione; ingawa wanasikiliza, wasielewe.’
Naye akajibu, “Ninyi mmejaliwa kujua siri za Ufalme wa Mungu, lakini hao wengine sivyo; ila hao huambiwa kwa mifano, ili wakitazama wasiweze kuona, na wakisikia wasifahamu.
11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu.
“Basi, maana ya mfano huu ni hii: mbegu ni neno la Mungu.
12 Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka.
Zile zilizoanguka njiani zinaonyesha watu wale wanaosikia lile neno, halafu Ibilisi akaja na kuliondoa mioyoni mwao wasije wakaamini na hivyo wakaokoka.
13 Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.
Zile zilizoanguka penye mawe zinaonyesha watu wale ambao wanaposikia juu ya lile neno hulipokea kwa furaha. Hata hivyo, kama zile mbegu, watu hao hawana mizizi maana husadiki kwa kitambo tu, na wanapojaribiwa hukata tamaa.
14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.
Zile zilizoanguka kwenye miti ya miiba ni watu wale wanaosikia lile neno, lakini muda si muda, wanapokwenda zao, husongwa na wasiwasi, mali na anasa za maisha, na hawazai matunda yakakomaa.
15 Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.
Na zile zilizoanguka kwenye udongo mzuri ndio watu wale wanaolisikia lile neno, wakalizingatia kwa moyo mwema na wa utii. Hao huvumilia mpaka wakazaa matunda.
16 “Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga.
“Watu hawawashi taa na kuifunika kwa chombo au kuiweka mvunguni. Lakini huiweka juu ya kinara ili watu wanapoingia ndani wapate kuona mwanga.
17 Kwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi.
“Chochote kilichofichwa kitafichuliwa na siri yoyote itagunduliwa na kujulikana hadharani.
18 Kwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyangʼanywa.”
“Kwa hiyo, jihadharini jinsi mnavyosikia; maana aliye na kitu ataongezewa, lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani kuwa anacho, kitachukuliwa.”
19 Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu.
Hapo mama na ndugu zake Yesu wakamjia, lakini hawakuweza kumkaribia kwa sababu ya umati wa watu.
20 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”
Yesu akapewa habari kwamba mama na ndugu zake walikuwa nje, wanataka kumwona.
21 Yesu akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulifanya.”
Lakini Yesu akawaambia watu wote, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”
22 Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo ya ziwa.” Nao wakaondoka.
Siku moja, Yesu alipanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvuke ziwa twende mpaka ng'ambo.” Basi, wakaanza safari.
23 Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.
Walipokuwa wanasafiri kwa mashua, Yesu alishikwa na usingizi, akalala. Dhoruba kali ikaanza kuvuma, maji yakaanza kuingia ndani ya mashua, wakawa katika hatari.
24 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!” Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari.
Wale wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwamsha wakisema, “Bwana, Bwana! Tunaangamia!” Yesu akaamka, akaikemea dhoruba na mawimbi, navyo vikatulia, kukawa shwari.
25 Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?” Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”
Kisha akawaambia, “Iko wapi imani yenu?” Lakini wao walishangaa na kuogopa huku wakiambiana, “Huyu ni nani basi, hata anaamuru dhoruba na mawimbi, navyo vinamtii?”
26 Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, ambayo iko upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya.
Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ng'ambo ya ziwa.
27 Yesu aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini.
Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo, hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini.
28 Alipomwona Yesu, alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!”
Alipomwona Yesu, alipiga kelele na kujitupa chini mbele yake, na kusema kwa sauti kubwa “We, Yesu Mwana wa Mungu Aliye Juu una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!”
29 Wakati huo Yesu alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.
Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikwishamwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani.
30 Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.
Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akajibu, “Jina langu ni Jeshi” —kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa.
31 Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda katika Shimo. (Abyssos g12)
Hao pepo wakamsihi asiwaamuru wamtoke na kwenda kwenye shimo lisilo na mwisho. (Abyssos g12)
32 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu.
Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa.
33 Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama.
Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakazama majini.
34 Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani.
Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari, mjini na mashambani.
35 Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Yesu, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Yesu, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa.
Watu wakaja kuona yaliyotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, ana akili zake, wakaogopa.
36 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa.
Wale watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza hao jinsi yule mtu alivyoponywa.
37 Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Yesu aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake.
Wakazi wa nchi ya Gerase walishikwa na hofu kubwa. Kwa hiyo wakamwomba Yesu aondoke, aende zake. Hivyo Yesu alipanda tena mashua, akaondoka.
38 Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Yesu afuatane naye, lakini Yesu akamuaga, akamwambia:
Yule mtu aliyetokwa na wale pepo akamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu hakumruhusu, bali akamwambia,
39 “Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Yesu alimtendea.
“Rudi nyumbani ukaeleze yote Mungu aliyokutendea.” Basi, yule mtu akaenda akitangaza kila mahali katika mji ule mambo yote Yesu aliyomtendea.
40 Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea.
Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea.
41 Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake,
Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake,
42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa. Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.
kwa kuwa binti yake wa pekee, mwana wa pekee mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa mahututi. Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande.
43 Katika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya.
Kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya.
44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.
Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu.
45 Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?” Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”
Yesu akasema, “Ni nani aliyenigusa?” Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, “Mwalimu, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!”
46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”
Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka.”
47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara.
Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponyeshwa mara moja.
48 Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”
Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”
49 Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”
Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: “Binti yako ameshakufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?”
50 Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”
Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, “Usiogope; amini tu, naye atapona.”
51 Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti.
Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana.
52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”
Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, “Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!”
53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa.
Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa.
54 Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!”
Lakini Yesu akamshika mkono akasema, “Mtoto amka!”
55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula.
Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula.
56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.
Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka.

< Luka 8 >