< Luka 4 >

1 Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani. Akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi nyikani,
Yesu alitoka katika mto Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani.
2 mahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula chochote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.
Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa.
3 Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”
Ndipo Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”
4 Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’”
Yesu akamjibu, “Imeandikwa: Mtu haishi kwa mkate tu.”
5 Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja.
Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonyesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia,
6 Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa yeyote ninayetaka.
“Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza.
7 Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”
Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu.”
8 Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’”
Yesu akamjibu, “Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako, na utamtumikia yeye peke yake.”
9 Kisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa,
Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu,
10 kwa maana imeandikwa: “‘Atakuagizia malaika zake ili wakulinde;
kwa maana imeandikwa: Atawaamuru malaika wake wakulinde,
11 nao watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’”
na tena, Watakuchukua mikononi mwao usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.”
12 Yesu akamjibu, “Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”
Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa: Usimjaribu Bwana Mungu wako.”
13 Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao.
Ibilisi alipokwishamjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.
14 Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando.
Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.
15 Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao, na kila mmoja akamsifu.
Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.
16 Yesu akaenda Nazareti, alipolelewa, na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome,
Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi, kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.
17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:
Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:
18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa sababu amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoonewa,
“Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani amenipaka mafuta niwahubirie maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa,
19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”
na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.”
20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.
Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.
21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”
Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia likisomwa, limetimia leo.”
22 Wote waliokuwako wakamsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”
Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakanena, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”
23 Yesu akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii: ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’”
Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: Mganga jiponye mwenyewe, na pia mtasema: Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye hapa pia katika kijiji chako.”
24 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika katika mji wake mwenyewe.
Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi katika kijiji chake.
25 Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Eliya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima.
Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Eliya. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.
26 Hata hivyo Eliya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.
Hata hivyo, Eliya hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarepta, Sidoni.
27 Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Elisha, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.”
Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani, mwenyeji wa Siria.”
28 Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana.
Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.
29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima mahali ambapo mji huo ulikuwa umejengwa, ili wamtupe chini kutoka kwenye mteremko mkali.
Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.
30 Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya huo umati wa watu akaenda zake.
Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.
31 Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya, na katika siku ya Sabato akawa anafundisha.
Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu katika mkoa wa Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.
32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.
Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.
33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu. Naye akapiga kelele kwa nguvu akisema,
Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na roho ya pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:
34 “Tuache! Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”
“We! Yesu wa Nazareti! Kwa nini unatuingilia? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni mjumbe Mtakatifu wa Mungu!”
35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha yule mtu chini mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.
Lakini Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
36 Watu wote wakashangaa, wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Anawaamuru pepo wachafu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!”
Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”
37 Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.
Habari zake zikaenea mahali pote katika mkoa ule.
38 Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mama mkwe wa Simoni akiwa ameshikwa na homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie.
Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.
39 Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka saa ile ile, naye akaanza kuwahudumia.
Yesu akaenda akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Mara yule mama akainuka, akawatumikia.
40 Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Yesu watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya.
Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.
41 Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Kristo.
Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe u Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walimfahamu kwamba yeye ndiye Kristo.
42 Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke.
Kesho yake asubuhi Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta, na walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.
43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”
Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.”
44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.
Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.

< Luka 4 >