< Luka 3 >

1 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Uyahudi, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania akiwa mfalme wa Abilene,
Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, alikuwa mkuu wa mikoa ya Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mkuu wa mkoa wa Abilene,
2 nao Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, neno la Mungu likamjia Yohana, mwana wa Zekaria huko jangwani.
na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu mjini Yerusalem. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane, mwana wa Zakariya, kule jangwani.
3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.
Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani, akihubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi.
4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.
Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni mapito yake.
5 Kila bonde litajazwa, kila mlima na kilima vitashushwa. Njia zilizopinda zitanyooshwa, na zilizoparuza zitasawazishwa.
Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyooshwa, njia mbaya zitatengenezwa.
6 Nao watu wote watauona wokovu wa Mungu.’”
Na, watu wote watauona wokovu utokao kwa Mungu.”
7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?
Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: “Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mngeweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?
8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka mawe haya.
Basi, onyesheni kwa matendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kusema: Sisi ni watoto wa Abrahamu. Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyageuza mawe haya yawe watoto wa Abrahamu!
9 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
Lakini, sasa hivi shoka limewekwa tayari kukata mizizi ya miti. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”
10 Ule umati wa watu ukamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”
Umati wa watu ukamwuliza, “Tufanye nini basi?”
11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”
Akawajibu, “Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo.”
12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”
Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, “Mwalimu, tufanye nini?”
13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”
Naye akawaambia, “Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa.”
14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?” Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”
Nao askari wakamwuliza, “Na sisi tufanye nini?” Naye akawajibu, “Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu.”
15 Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo.
Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane: kuwa labda yeye ndiye Kristo.
16 Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuniliko mimi, ambaye sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
Hapo Yohane akawaambia wote, “Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”
Yeye ni kama mtu anayeshika mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka, aipure nafaka yake, akusanye ngano ghalani mwake, na makapi ayachome kwa moto usiozimika.”
18 Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwasihi na kuwahubiria watu Habari Njema.
Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema.
19 Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya,
Lakini Yohane alimgombeza Herode, mkuu wa mkoa, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia, mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya.
20 Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yohana gerezani.
Kisha Herode akazidisha ubaya wake kwa kumtia Yohane gerezani.
21 Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka.
Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa. Na alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka,
22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”
na Roho Mtakatifu akamshukia akiwa na umbo kama la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.”
23 Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Eli,
Yesu alipoanza kazi yake hadharani, alikuwa na umri upatao miaka thelathini, na watu walidhani yeye ni mwana wa Yosefu, mwana wa Heli.
24 Eli alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi, Lawi alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Yanai, Yanai alikuwa mwana wa Yosefu,
Heli alikuwa mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, mwana wa Melki, mwana wa Yanai, mwana wa Yosefu,
25 Yosefu alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Amosi, Amosi alikuwa mwana wa Nahumu, Nahumu alikuwa mwana wa Esli, Esli alikuwa mwana wa Nagai,
mwana wa Matathia, mwana wa Amosi, mwana wa Nahumu, mwana wa Hesli, mwana wa Nagai,
26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi, Maathi alikuwa mwana wa Matathia, Matathia alikuwa mwana wa Semeini, Semeini alikuwa mwana wa Yoseki, Yoseki alikuwa mwana wa Yoda,
mwana wa Maathi, mwana wa Matathia, mwana wa Shemeni, mwana wa Yoseki, mwana wa Yuda,
27 Yoda alikuwa mwana wa Yoanani, Yoanani alikuwa mwana wa Resa, Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli, Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli, Shealtieli alikuwa mwana wa Neri,
mwana wa Yohanani, mwana wa Resa, mwana wa Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mwana wa Neri,
28 Neri alikuwa mwana wa Melki, Melki alikuwa mwana wa Adi, Adi alikuwa mwana wa Kosamu, Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu, Elmadamu alikuwa mwana wa Eri,
mwana wa Melki, mwana wa Adi, mwana wa Kosamu, mwana wa Elmadamu, mwana wa Eri,
29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua, Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri, Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu, Yorimu alikuwa mwana wa Mathati, Mathati alikuwa mwana wa Lawi,
mwana wa Yoshua, mwana wa Eliezeri, mwana wa Yorimu, mwana wa Mathati, mwana wa Lawi,
30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni, Simeoni alikuwa mwana wa Yuda, Yuda alikuwa mwana wa Yosefu, Yosefu alikuwa mwana wa Yonamu, Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu, Eliakimu alikuwa mwana wa Melea,
mwana wa Simeoni, mwana wa Yuda, mwana wa Yosefu, mwana wa Yonamu, mwana wa Eliakimu,
31 Melea alikuwa mwana wa Mena, Mena alikuwa mwana wa Matatha, Matatha alikuwa mwana wa Nathani, Nathani alikuwa mwana wa Daudi,
mwana wa Melea, mwana wa Mena, mwana wa Matatha, mwana wa Nathani, mwana wa Daudi,
32 Daudi alikuwa mwana wa Yese, Yese alikuwa mwana wa Obedi, Obedi alikuwa mwana wa Boazi, Boazi alikuwa mwana wa Salmoni, Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni,
mwana wa Yese, mwana wa Obedi, mwana wa Boazi, mwana wa Salmoni, mwana wa Nashoni,
33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu, Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu, Aramu alikuwa mwana wa Hesroni, Hesroni alikuwa mwana wa Peresi, Peresi alikuwa mwana wa Yuda,
mwana wa Aminadabu, mwana wa Admini, mwana wa Arni, mwana wa Hesroni, mwana wa Feresi, mwana wa Yuda,
34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo, Yakobo alikuwa mwana wa Isaki, Isaki alikuwa mwana wa Abrahamu, Abrahamu alikuwa mwana wa Tera, Tera alikuwa mwana wa Nahori,
mwana wa Yakobo, mwana wa Isaka, mwana wa Abrahamu, mwana wa Tera, mwana wa Nahori,
35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi, Serugi alikuwa mwana wa Reu, Reu alikuwa mwana wa Pelegi, Pelegi alikuwa mwana wa Eberi, Eberi alikuwa mwana wa Sala,
mwana wa Serugi, mwana wa Reu, mwana wa Pelegi, mwana wa Eberi, mwana wa Sala,
36 Sala alikuwa mwana wa Kenani, Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi, Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu, Shemu alikuwa mwana wa Noa, Noa alikuwa mwana wa Lameki,
mwana wa Kainani, mwana wa Arfaksadi, mwana wa Shemu, mwana wa Noa, mwana wa Lameki,
37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela, Methusela alikuwa mwana wa Enoki, Enoki alikuwa mwana wa Yaredi, Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli, Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani,
mwana wa Mathusala, mwana wa Henoki, mwana wa Yaredi, mwana wa Mahalaleli, mwana wa Kenani,
38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi, Enoshi alikuwa mwana wa Sethi, Sethi alikuwa mwana wa Adamu, Adamu alikuwa mwana wa Mungu.
mwana wa Enosi, mwana wa Sethi, mwana wa Adamu, aliyekuwa wa Mungu.

< Luka 3 >