< Luka 23 >
1 Kisha umati wote wa watu ukainuka na kumpeleka Yesu kwa Pilato.
Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato.
2 Nao wakaanza kumshtaki wakisema: “Tumemwona huyu mtu akipotosha taifa letu, akiwazuia watu wasilipe kodi kwa Kaisari na kujiita kuwa yeye ni Kristo, mfalme.”
Wakaanza kumshtaki wakisema: “Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme.”
3 Basi Pilato akamuuliza Yesu, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?” Yesu akajibu, “Wewe wasema.”
Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.”
4 Pilato akawaambia viongozi wa makuhani na watu wote waliokuwepo, “Sioni sababu ya kutosha kumshtaki mtu huyu!”
Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, “Sioni kosa lolote katika mtu huyu.”
5 Lakini wao wakakazana kusema, “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika Uyahudi yote, tangu Galilaya alikoanzia, hadi sehemu hii!”
Lakini wao wakasisitiza wakisema: “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa.”
6 Pilato aliposikia hayo akauliza, “Huyu mtu ni Mgalilaya?”
Pilato aliposikia hayo, akauliza, “Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?”
7 Alipofahamu kwamba Yesu alikuwa chini ya mamlaka ya Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa pia Yerusalemu.
Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu.
8 Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amesikia mambo mengi kumhusu yeye. Pia alitarajia kumwona akifanya miujiza kadha wa kadha.
Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza.
9 Herode akamuuliza maswali mengi, lakini Yesu hakumjibu lolote.
Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno.
10 Wakati huo viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwepo wakitoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
11 Herode na askari wake wakamdhihaki Yesu na kumfanyia mzaha. Wakamvika vazi zuri sana, wakamrudisha kwa Pilato.
Basi, herode pamoja na maaskari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato.
12 Siku hiyo, Herode na Pilato wakawa marafiki; kabla ya jambo hili walikuwa na uadui kati yao.
Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki.
13 Basi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu,
Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu,
14 akawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake.
akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake.
15 Wala Herode hakumwona na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo.
Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo.
16 Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.” [
Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.”
17 Kwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.]
Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.
18 Ndipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!”
Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!”
19 (Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.)
(Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)
20 Pilato, akitaka kumwachia Yesu, akasema nao tena.
Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;
21 Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”
lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!”
22 Kwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”
Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya kosa gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”
23 Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu zaidi, wakidai kwamba Yesu asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda.
Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.
24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe.
Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.
25 Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Yesu mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.
Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
26 Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu.
Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu.
27 Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea.
Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia.
28 Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu.
Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu.
29 Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’
Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!
30 Ndipo “‘wataiambia milima, “Tuangukieni!” na vilima, “Tufunikeni!”’
Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: Tuangukieni! na vilima, Tufunikeni!
31 Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?”
Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?”
32 Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulubiwe.
Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto.
Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.
34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.
Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.”
Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!”
36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe,
Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki
37 na wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
38 Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi. Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.
Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.”
39 Mmoja wa wale wahalifu waliosulubiwa pamoja naye akamtukana, akasema: “Wewe si ndiye Kristo? Jiokoe mwenyewe na utuokoe na sisi.”
Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.”
40 Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake, akasema, “Je, wewe humwogopi Mungu, wakati uko kwenye adhabu iyo hiyo?
Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.
41 Sisi tumehukumiwa kwa haki kwa kuwa tunapata tunayostahili kwa ajili ya matendo yetu. Lakini huyu mtu hajafanya kosa lolote.”
Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”
42 Kisha akasema, “Yesu, unikumbuke utakapokuja katika Ufalme wako.”
Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.”
43 Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.”
44 Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa,
Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likafunika nchi yote mpaka saa tisa,
45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.
na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka vipande viwili.
46 Yesu akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.
Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, naiweka roho yangu mikononi mwako.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.
47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”
Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.”
48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao.
Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni.
49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.
Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yosefu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi,
Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Armathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika;
51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa mwenyeji wa Arimathaya huko Uyahudi, naye alikuwa anaungojea Ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa.
Alikuwa akitazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao.
52 Yosefu alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
53 Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado.
Kisha, akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika.
54 Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.
Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza.
55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Yesu wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yosefu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa.
Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa
56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.
Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi kuyapaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.