< Luka 21 >

1 Yesu alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu.
Yesu alitazama kwa makini, akawaona matajiri walivyokuwa wanatia sadaka zao katika hazina ya Hekalu,
2 Akamwona pia mjane mmoja maskini akiweka humo sarafu mbili ndogo za shaba.
akamwona pia mama mmoja mjane akitumbukiza humo sarafu mbili ndogo.
3 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo zaidi ya watu wengine wote.
Basi, akasema, “Nawaambieni kweli, mama huyu mjane ametia zaidi katika hazina kuliko wote.
4 Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kutokana na wingi wa mali zao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
Kwa maana, wengine wote wametoa sadaka zao kutokana na ziada ya mali zao, lakini huyu mama, ingawa ni maskini, ametoa kila kitu alichohitaji kwa kuishi.”
5 Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonyesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Yesu akawaambia,
Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanazungumza juu ya Hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe ya thamani, pamoja na sadaka zilizotolewa kwa Mungu. Yesu akasema,
6 “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
“Haya yote mnayoyaona—zitakuja siku ambapo hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa.”
7 Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonyesha kwamba yanakaribia kutendeka?”
Basi, wakamwuliza, “Mwalimu, mambo hayo yatatokea lini? Na ni ishara gani zitakazoonyesha kwamba karibu mambo hayo yatokee?”
8 Yesu akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate.
Yesu akawajibu, “Jihadharini, msije mkadanganyika. Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: Mimi ndiye, na, Wakati ule umekaribia. Lakini ninyi msiwafuate!
9 Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”
Basi, mtakaposikia habari za vita na misukosuko, msitishike; maana ni lazima hayo yatokee kwanza, lakini mwisho wa yote, bado.”
10 Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine.
Halafu akaendelea kusema: “Taifa moja litapigana na taifa lingine, na ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine.
11 Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, kutakuwa na njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani.
12 “Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu.
Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu.
13 Hii itawapa nafasi ya kushuhudia.
Hii itawapeni fursa ya kushuhudia Habari Njema.
14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka.
Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea,
15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.
kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hivyo kwamba zenu hawataweza kustahimili wala kupinga.
16 Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, na baadhi yenu watawaua.
Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti ninyi; na baadhi yenu mtauawa.
17 Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu.
Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu.
18 Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia.
Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.
19 Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.
Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.
20 “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia.
“Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo mtambue ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa.
21 Wakati huo, wale walio Uyahudi wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo, nao wale walioko mashambani wasiingie mjini.
Hapo walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini.
22 Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa.
Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie.
23 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu.
Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa.
24 Wataanguka kwa makali ya upanga, na wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote. Nao mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa Mataifa hadi muda wa hao watu wa Mataifa utimie.
Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.
25 “Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari.
“Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.
26 Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika.
Watu watazirai kwa sababu ya uoga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.
27 Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu.
Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.
28 Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”
Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.”
29 Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote.
Kisha akawaambia mfano: “Angalieni mtini na miti mingine yote.
30 Inapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua wenyewe ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia.
Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
31 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.
Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.
32 “Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
Nawaambieni hakika, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka.
33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”
Mbingu na dunia vitapita, lakini maneno yangu hayatapita.
34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo.
“Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, Siku ile itawajieni ghafla.
35 Kwa maana kama vile mtego unasavyo, ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote waishio katika uso wa dunia yote.
Kwa maana itawajia kama mtego, wote wanaoishi duniani pote.
36 Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”
Muwe waangalifu basi, na salini daima ili muweze kupata nguvu ya kupita salama katika mambo haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele ya Mwana wa Mtu.”
37 Kila siku Yesu alikuwa akifundisha Hekaluni, na jioni ilipofika, alikwenda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha.
Wakati wa mchana, siku hizo, Yesu alikuwa akifundisha watu Hekaluni; lakini usiku alikuwa akienda katika mlima wa Mizeituni na kukaa huko.
38 Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.
Watu wote walikuwa wanakwenda Hekaluni asubuhi na mapema, wapate kumsikiliza.

< Luka 21 >