< Luka 18 >

1 Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.
Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa.
2 Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwepo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu.
Alisema: “Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu.
3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’
Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake.
4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu,
Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,
5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’”
lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!”
6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu.
Basi, Bwana akaendelea kusema, “Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.
7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia?
Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza?
8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”
Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?”
9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine:
Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.
10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru.
“Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru.
11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru.
12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.
13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.
14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.”
15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.
Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.
16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.
Lakini Yesu akawaita kwake akisema: “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.
17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo.”
18 Mtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” (aiōnios g166)
Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?” (aiōnios g166)
19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake.
Yesu akamwambia, “Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’”
Unazijua amri: Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako.”
21 Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
Yeye akasema, “Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu.”
22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
Yesu aliposikia hayo akamwambia, “Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate.”
23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.
Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.
24 Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, “Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
Wale watu waliposikia hayo, wakasema, “Nani basi, atakayeokolewa?”
27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”
Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu.”
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
Naye Petro akamwuliza, “Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!”
29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu
Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.” (aiōn g165, aiōnios g166)
atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao.” (aiōn g165, aiōnios g166)
31 Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.
Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa.
32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua.
Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.
33 Naye siku ya tatu atafufuka.”
Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka.”
34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.
Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.
35 Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.
Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.
36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?”
Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, “Kuna nini?”
37 Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”
Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”
38 Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
Naye akapaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: “Mwana wa Daudi, nihurumie;”
40 Yesu akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Yesu akamuuliza,
Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza,
41 “Unataka nikufanyie nini?” Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”
“Unataka nikufanyie nini?” Naye akamjibu, “Bwana, naomba nipate kuona tena.”
42 Yesu akamwambia, “Basi upate kuona. Imani yako imekuponya.”
Yesu akamwambia, “Ona! Imani yako imekuponya.”
43 Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.
Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.

< Luka 18 >