< Luka 18 >
1 Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.
Kisha akawaambia mfano wa namna wanavyopaswa kuomba daima, na wasikate tamaa.
2 Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwepo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu.
akaisema, 'Kulikuwa na hakimu katika mji fulani, ambaye hakuwa anamwogopa Mungu na hakuwaheshimu watu.
3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’
Kulikuwa na mjane katika jiji hilo, naye alimwendea mara nyingi, akisema, 'Nisaidie kupata haki dhidi ya mpinzani wangu.'
4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Ijapokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu,
Kwa muda mrefu hakuwa tayari kumsaidia, lakini baada ya muda akasema moyoni mwake, `Ingawa mimi simwogopi Mungu au kuheshimu mtu,
5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’”
lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua nitamsaidia kupata haki yake, ili asije akanichosha kwa kunijia mara kwa mara. ''
6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu.
Kisha Bwana akasema, 'Sikiliza alivyosema huyo hakimu dhalimu.
7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia?
Je Mungu pia hataleta haki kwa wateule wake ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, yeye hatakuwa mvumilivu kwao?
8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”
Nawaambia kwamba ataleta haki kwao upesi. Lakini wakati Mwana wa Adamu atakapokuja, je, atakuta imani duniani? '
9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine:
Ndipo akawaambia mfano huu kwa baadhi ya watu ambao wanajiona wenyewe kuwa wenye haki na kuwadharau watu wengine,
10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru.
'Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo mwingine mtoza ushuru.
11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
Farisayo akasimama akaomba mambo haya juu yake mwenyewe, 'Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine ambao ni wanyang'anyi, watu wasio waadilifu, wazinzi, au kama huyu mtoza ushuru.
12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
Nafunga mara mbili kila wiki. Natoa zaka katika mapato yote ninayopata. '
13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
Lakini yule mtoza ushuru, alisimama mbali, bila hakuweza hata kuinua macho yake mbinguni, akagonga kifua chake akisema, 'Mungu, nirehemu mimi mwenye dhambi.'
14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
Nawaambia, mtu huyu alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki kuliko yule mwingine, kwa sababu kila ajikwezaye atashushwa, lakini kila mtu anayejinyenyekeza atainuliwa. '
15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.
Watu walimletea watoto wao wachanga, ili aweze kuwagusa, lakini wanafunzi wake walipoona hayo, wakawazuia.
16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa wale walio kama hawa.
Lakini Yesu akawaita kwake akisema, 'Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie. Maana ufalme wa Mungu ni wa watu kama hao.
17 Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”
Amin, nawaambia, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto ni dhahiri hatauingia. '
18 Mtawala mmoja akamuuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” (aiōnios )
Mtawala mmoja akamwuliza, akisema, 'Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?' (aiōnios )
19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna yeyote aliye mwema ila Mungu peke yake.
Yesu akamwambia, 'Kwa nini unaniita mwema? Hakuna mtu aliye mwema, ila Mungu peke yake.
20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’”
Unazijua amri- usizini, usiue, Usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.
21 Akajibu, “Amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”
Yule mtawala akasema, 'Mambo haya yote nimeyashika tangu nilipokuwa kijana.'
22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
Yesu alipoyasikia hayo akamwambia, '“Umepungukiwa jambo moja. Lazima uuze vyote ulivyonavyo na uwagawie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni -kisha njoo, unifuate. '
23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.
Lakini tajiri aliposikia hayo, alihuzunika sana, kwa sababu alikuwa tajiri sana.
24 Yesu akamtazama, akasema, “Tazama jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
Kisha Yesu, akamwona alivyohuzunika sana akasema, 'Jinsi gani itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”
Maana ni rahisi sana kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu. '
26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
Wale waliosikia hayo, wakasema, 'Nani basi, atakayeweza kuokolewa?'
27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu yanawezekana kwa Mungu.”
Yesu akajibu, 'Mambo yasiyowezekana kwa mwanadamu kwa Mungu yanawezekana.”
28 Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwa navyo tukakufuata!”
Petro akasema, 'Naam, sisi tumeacha kila kitu na tumekufuata wewe. '
29 Yesu akajibu, “Amin, nawaambia, hakuna hata mtu aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu
Kisha Yesu akawaambia, Amin, nawaambia kwamba hakuna mtu aliyeacha nyumba, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto, kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya, na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.” (aiōn , aiōnios )
ambaye hatapokea mengi zaidi katika ulimwengu huu, na katika ulimwengu ujao, uzima wa milele. ' (aiōn , aiōnios )
31 Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.
Baada ya kuwakusanya wale kumi na wawibili, akawaambia, 'Tazama, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote ambayo yameandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Adamu yatakamilishwa.
32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumuua.
Kwa maana atatiwa mikononi mwa watu wa Mataifa na atatendewa dhihaka na jeuri, na kutemewa mate.
33 Naye siku ya tatu atafufuka.”
Baada ya kumchapa viboko watamwua na siku ya tatu atafufuka. '
34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.
Hawakuelewa mambo haya, na neno hili lilikuwa limefichwa kwao, na hawakuelewa mambo yaliyosemwa.
35 Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.
Ikawa Yesu ulipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya barabara akiomba msaada,
36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?”
aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza nini kinatokea.
37 Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”
Wakamwambia kwamba Yesu wa Nazareti anapita.
38 Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”
Hivyo yule kipofu akalia kwa sauti, akisema, 'Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu.'
39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea, wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”
wale waliokuwa wakitembea walimkemea huyo kipofu, wakamwambia anyamaze. Lakini yeye akazidi kulia kwa sauti, 'Mwana wa Daudi, unirehemu.
40 Yesu akasimama, akawaamuru wamlete huyo mtu kwake. Alipokaribia, Yesu akamuuliza,
Yesu akasimama akaamuru mtu yule aletwe kwake. Kisha yule kipofu alipomkaribia, Yesu akamwuliza,
41 “Unataka nikufanyie nini?” Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”
'Unataka nikufanyie nini?' Akasema, 'Bwana, nataka kuona.'
42 Yesu akamwambia, “Basi upate kuona. Imani yako imekuponya.”
Yesu akamwambia, 'Upate kuona. Imani yako imekuponya. '
43 Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.
Mara hiyo akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Walipoona hili, watu wote wakamsifu Mungu.