< Luka 14 >
1 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii.
Siku moja ya Sabato, Yesu alikwenda kula chakula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo; watu waliokuwapo hapo wakawa wanamchunguza.
2 Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili.
Mbele yake Yesu palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kuvimba mwili.
3 Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?”
Yesu akawauliza walimu wa Sheria na Mafarisayo, “Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya sabato?”
4 Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.
Lakini wao wakakaa kimya. Yesu akamshika huyo mgonjwa, akamponya, akamwacha aende zake.
5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?”
Halafu akawaambia, “Ni nani kati yenu ambaye mtoto wake au ng'ombe wake akitumbukia shimoni, hangemtoa hata kama ni siku ya Sabato?”
6 Nao hawakuwa na la kusema.
Nao hawakuweza kumjibu swali hilo.
7 Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu:
Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano:
8 “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe.
“Kama mtu akikualika arusini, usiketi mahali pa heshima isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe;
9 Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa.
na mwenyeji wenu ninyi wawili atakuja na kukwambia: Mwachie huyu nafasi. Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho.
10 Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote.
Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akwambie: Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi. Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe.
11 Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”
Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa, na anayejishusha, atakwezwa.”
12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako.
Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, “Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri, wasije nao wakakualika nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea.
13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu,
Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema viwete na vipofu,
14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka.”
15 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!”
Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, “Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika Ufalme wa Mungu.”
16 Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi.
Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi.
17 Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’
Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake awaambie walioalikwa, Njoni, kila kitu ni tayari.
18 “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’
Lakini wote, kwa namna moja, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: Nimenunua shamba, kwa hiyo sina budi kwenda kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.
19 “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’
Mwingine akasema: Nimenunua ng'ombe jozi tano wa kulima; sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.
20 Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’
Na mwingine akasema: Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.
21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’
Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na waliolemaa.
22 “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’
Baadaye, mtumishi huyo akasema: Bwana mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.
23 “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa.
Yule bwana akamwambia mtumishi: Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae.
24 Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’”
Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu.”
25 Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia,
Hapo, makundi mengi yakawa yanaandamana pamoja na Yesu. Basi, akawageukia akawaambia,
26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe.
“Mtu yeyote akija kwangu, asipowachukia baba na mama yake, mke wake, watoto, ndugu na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Mtu asipochukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha?
Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia?
29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki,
La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka
30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
wakisema: Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.
31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000?
“Au, ni mfalme gani ambaye, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, hataketi kwanza chini na kufikiri kama ataweza, kwa askari wake elfu ishirini?
32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani.
Kama anaona hataweza, atawatuma wajumbe kutaka masharti ya amani wakati mfalme huyo mwingine angali mbali.
33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho.
34 “Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itafanywaje ili iweze kukolea tena?
“Chumvi ni nzuri; lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini?
35 Haifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje. “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”
Haifai kitu wala kwa udongo wala kwa mbolea. Watu huitupilia mbali. Sikieni basi, kama mna masikio!”