< Luka 10 >

1 Baada ya hayo, Bwana akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye.
Baada ya mambo hayo, Bwana akachagua sabini wengine, na kuwatuma wawili wawili wamtangulie katika kila mji na eneo alilotarajia kwenda.
2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.
Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Hivyo basi muombeni Bwana wa mavuno, ili kwamba atume haraka wafanyakazi katika mavuno yake.
3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa mwitu.
Enendeni katika miji. Angalieni, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu.
4 Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.
Msibebe mfuko wa pesa, wala mikoba ya wasafiri, wala viatu, wala msimsalimie yeyote njiani.
5 “Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’
Katika nyumba yeyote mtakayo ingia, kwanza semeni, 'Amani iwe katika nyumba hii.'
6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia.
kama mtu wa amani yupo pale, amani yenu itabaki juu yake, lakini kama sivyo, itarudi kwenu.
7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.
Bakini katika nyumba hiyo, kuleni na mnywe watakachokitoa, kwa maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msihame kutoka nyumba hii kwenda nyingine.
8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu,
Mji wowote muuingiao, na wakawapokea, kuleni chochote kitakachowekwa mbele yenu,
9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’
na ponyeni wagonjwa waliomo humo. Semeni kwao, 'Ufalme wa Mungu umekuja karibu yanu'
10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:
Lakini katika mji wowote mtakaoingia, na wasiwapokee, nendeni nje katika barabara na semeni,
11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’
'Hata vumbi katika mji wenu lililonata miguu mwetu tunalikung'uta dhidi yenu! Lakini tambueni hili, Ufalme wa Mungu umekaribia.'
12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.
Ninawambieni kwamba siku ya hukumu itakuwa ni usitahamilivu zaidi kwa Sodoma kuliko mji huo.
13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.
Ole kwako Korazini, Ole kwako Bethsaida! Kama kazi kuu zilizo fanyika ndani yako ingalifanyika Tiro na Sidoni, Wangelitubu zamani sana, wakikaa ndani ya nguo za gunia na majivu.
14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi.
Lakini itakuwa usitahamilivu zaidi siku ya hukumu kwa Tiro na Sidoni zaidi yenu.
15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.” (Hadēs g86)
Wewe Kapernaumu, Unafikiri utainuliwa mpaka Mbinguni? Hapana, utashushwa chini mpaka kuzimu (Hadēs g86)
16 “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”
Atakaye wasikiliza ninyi anisikiliza mimi, na yeyote atakaye wakataa anikataa mimi, na yeyote anikataaye mimi anmtakaa aliyenituma”
17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”
Wale sabini walirudi kwa furaha, wakisema, “Bwana, hata mapepo wanatutii katika jina lako.”
18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi.
Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama radi.
19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru.
Tazama, nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za adui, na hapana chochote kwa njia yoyote kitakachowadhuru.
20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Hata hivyo msifurahi tu katika hili, kwamba roho zinawatii, lakini furahini zaidi kwamba majina yenu yameandikwa mbinguni.”
21 Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
Katika mda uleule alifurahi sana katika Roho Mtakatifu, na kusema, “Ninakusifu wewe, Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa sababu umeyaficha mambo haya kutoka kwa wenye hekima na akili, na kuyafunua kwa wasio fundishwa, kama watoto wadogo. Ndio, Baba, kwa kuwa ilipendeza katika machoni pako.”
22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”
“Kila kitu kimekabidhiwa kwangu na Baba yangu, na hakuna afahamuye Mwana ni nani ila Baba, na hakuna afahamuye Baba ni nani ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana hutamani kujifunua kwake.”
23 Basi Yesu akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona.
Akawageukia wanafunzi, akasema faraghani, “Wamebarikiwa wayaonayo haya ambayo ninyi mnayaona.
24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”
Ninawambia ninyi, kwamba manabii wengi na wafalme walitamani kuona mambo myaonayo, na hawakuyaona, na kusikia kusikia mnayoyaikia, na hawakuyasikia.”
25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” (aiōnios g166)
Tazama, mwalimu fulani wa sheria ya Kiyahudi alisimama na kumjaribu, akisema, “Mwalimu, nifanye nini niurithi izima wa milele?” (aiōnios g166)
26 Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Sheria? Kwani unasoma nini humo?”
Yesu akamwambia, “Kimeandikwa nini katika sheria? Unaisoma je?”
27 Akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’”
Akajibu akasema, “Utampenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote, na jirani yako kama nafsi yako mwenyewe.”
28 Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”
Yesu akasema, “Umejibu kwa usahihi. Fanya hivi na utaishi.”
29 Lakini yule mtaalamu wa sheria, akitaka kujionyesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Yesu, “Jirani yangu ni nani?”
Lakini mwalimu, akitamani kujihesabia haki mwenyewe, Akamwambia Yesu, “Na jirani yangu ni nani?”
30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa.
Yesu akijibu akasema, “Mtu fulani alikuwa akitelemka kutoka Yerusalem kwenda Yeriko. Akaangukia kati ya wanyang'anyi, waliomnyang'anya mali yake, na kumpiga na kumuacha karibu akiwa nusu mfu.
31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.
Kwa bahati kuhani fulani alikuwa akishuka katika njia hiyo, alipo muona alipita upande mwingine.
32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani
Vivyo hivyo Mlawi pia, alipofika mahali pale na kumuona, akapita upande mwingine.
33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia.
Lakini Msamaria mmoja, alipokuwa akisafiri, alipita pale alipokuwa mtu huyo. alipomuona, alisukumwa kwa huruma.
34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.
Alimkaribia na kumfunga vidonda vyake, akimwiga mafuta na divai juu yake. Alimpandisha juu ya mnyama wake, na kumpeleka katika nyumba ya wageni na kumhudumia.
35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbiliakampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
Siku ilyofuata alichukua dinari mbili, na akampatia mmiliki wa nyumba ya wageni na kumwambia, 'Muhudumie na chochote cha ziada utakacho tumia, nitakulipa nitakaporudi.'
36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”
Ni yupi kati ya hawa watatu, unafikiri, alikuwa ni jirani kwake yeye aliyeangukia kati ya wanyang'anyi?”
37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.” Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
Mwalimu alisema, “Ni yule aliyeonesha huruma kwake.” Yesu akamwambia, “Nenda na ukafanye vivyo hivyo”
38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake.
Sasa walipokuwa wakisafiri, waliingia katika kijiji fulani, na mwanamke mmoja jina lake Martha alimkaribisha nyumbani kwake.
39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale aliyokuwa akisema.
Alikuwa na dada aliyeitwa Mariamu, aliekaa miguuni pa Bwana na kusikiliza neno lake.
40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”
Lakini Martha alijipa shughuli nyingi za kuandaa mlo. Alikwenda kwa Yesu, na kusema, “Bwana, haujali kwamba dada yangu ameniacha nihudumu peke yangu? Hivyo basi mwambie anisaidie.”
41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi?
Lakini Bwana alimjibu na kumwambia, “Martha, Martha, una sumbuka juu ya mambo mengi,
42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”
lakini ni kitu kimoja tu cha muhimu. Mariamu amechagua kilicho chema, ambacho hakitaondolewa kutoka kwake.”

< Luka 10 >