< Luka 1 >

1 Kwa kuwa watu wengi wamekaa ili kuandika habari za mambo yaliyotukia katikati yetu,
Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.
2 kama vile yalivyokabidhiwa kwetu na wale waliokuwa mashahidi walioyaona na watumishi wa Bwana,
Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.
3 mimi nami baada ya kuchunguza kila kitu kwa uangalifu kuanzia mwanzo, niliamua kukuandikia habari za mambo hayo, ewe mtukufu Theofilo,
Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,
4 ili upate kujua ukweli kuhusu yale uliyofundishwa.
ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
5 Wakati wa Herode mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja jina lake Zekaria, ambaye alikuwa wa ukoo wa kikuhani wa Abiya. Elizabeti mkewe alikuwa pia mzao wa Aroni.
Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.
6 Zekaria na Elizabeti mkewe wote walikuwa watu wanyofu mbele za Mungu, wakizishika amri zote za Bwana na maagizo yote bila lawama.
Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.
7 Lakini walikuwa hawana watoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa; nao wote wawili walikuwa wazee sana.
Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
8 Siku moja ilipokuwa zamu ya kikundi cha Zekaria, yeye akifanya kazi ya ukuhani Hekaluni mbele za Mungu,
Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,
9 alichaguliwa kwa kura kwa kufuata desturi za ukuhani, kuingia Hekaluni mwa Bwana ili kufukiza uvumba.
Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.
10 Nao wakati wa kufukiza uvumba ulipowadia, wale wote waliokuwa wamekusanyika ili kuabudu walikuwa nje wakiomba.
Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.
11 Ndipo malaika wa Bwana, akiwa amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia uvumba, akamtokea Zekaria.
Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.
12 Zekaria alipomwona huyo malaika, akafadhaika sana, akajawa na hofu.
Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
13 Lakini malaika akamwambia, “Usiogope, Zekaria, kwa maana Mungu amesikia maombi yako. Mkeo Elizabeti atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utamwita jina lake Yohana.
Lakini malaika akamwambia, “Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
14 Yeye atakuwa furaha na shangwe kwako, nao watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
15 Kwa kuwa atakuwa mkuu mbele za Bwana, kamwe hataonja mvinyo wala kinywaji chochote cha kulevya, naye atajazwa Roho Mtakatifu hata kabla ya kuzaliwa kwake.
Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
16 Naye atawageuza wengi wa wana wa Israeli warudi kwa Bwana Mungu wao.
Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
17 Naye atatangulia mbele za Bwana katika roho na nguvu ya Eliya, ili kuigeuza mioyo ya baba kuwaelekea watoto wao, na wasiotii warejee katika hekima ya wenye haki, ili kuliweka tayari taifa lililoandaliwa kwa ajili ya Bwana.”
Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.”
18 Zekaria akamuuliza malaika, “Jambo hilo linawezekanaje? Mimi ni mzee na mke wangu pia ana umri mkubwa.”
Zakariya akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.”
19 Malaika akamjibu, akamwambia, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu, nami nimetumwa kwako ili nikuambie habari hizi njema.
Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema.
20 Basi sasa kwa kuwa hujaamini maneno yangu ambayo yatatimizwa kwa wakati wake, utakuwa bubu hadi siku ile mambo haya yatakapotukia.”
Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia.”
21 Wakati huo watu walikuwa wanamngojea Zekaria nje huku wakishangaa kukawia kwake mle Hekaluni.
Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni.
22 Alipotoka akawa hawezi kusema nao, wao wakatambua kuwa ameona maono ndani ya Hekalu. Lakini kwa kuwa alikuwa bubu, akawa anawaashiria kwa mikono.
Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
23 Muda wake wa kuhudumu Hekaluni ulipomalizika, akarudi nyumbani kwake.
Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.
24 Baada ya muda usio mrefu, Elizabeti mkewe akapata mimba, naye akajitenga kwa miezi mitano.
Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema:
25 Akasema, “Hili ndilo Bwana alilonitendea aliponiangalia kwa upendeleo na kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.”
“Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu.”
26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mungu alimtuma malaika Gabrieli aende Galilaya katika mji wa Nazareti,
Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya,
27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yosefu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Maria.
kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi.
28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa, Bwana yu pamoja nawe!”
Malaika akamwendea, akamwambia, “Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe.”
29 Maria akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?”
Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini?
30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu.
Malaika akamwambia, “Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.
31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Yesu.
Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu.
32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake.
Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake.
33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” (aiōn g165)
Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.” (aiōn g165)
34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”
Maria akamjibu, “Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?”
35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.
Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.
36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa.
Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”
Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.”
38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.
Maria akasema, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema.” Kisha yule malaika akaenda zake.
39 Wakati huo Maria akajiandaa, akaharakisha kwenda katika mji mmoja kwenye vilima vya Uyahudi.
Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda.
40 Akaingia nyumbani kwa Zekaria na kumsalimu Elizabeti.
Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu,
Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa.
akasema kwa sauti kubwa, “Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.
43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”
Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia.”
46 Naye Maria akasema: “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Naye Maria akasema,
47 nayo roho yangu inamfurahia Mungu Mwokozi wangu,
“Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili unyonge wa mtumishi wake. Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu amenitendea mambo ya ajabu: jina lake ni takatifu.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
50 Rehema zake huwaendea wale wamchao, kutoka kizazi hadi kizazi.
Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
51 Kwa kuwa ametenda mambo ya ajabu kwa mkono wake; amewatawanya wale wenye kiburi ndani ya mioyo yao.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52 Amewashusha watawala toka kwenye viti vyao vya enzi, lakini amewainua wanyenyekevu.
amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
53 Amewashibisha wenye njaa kwa vitu vizuri, bali matajiri amewafukuza mikono mitupu.
Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
54 Amemsaidia mtumishi wake Israeli, kwa kukumbuka ahadi yake ya kumrehemu
Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
55 Abrahamu na uzao wake milele, kama alivyowaahidi baba zetu.” (aiōn g165)
Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele.” (aiōn g165)
56 Maria akakaa na Elizabeti karibu miezi mitatu, kisha akarudi nyumbani kwake.
Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
57 Ulipowadia wakati wa Elizabeti kujifungua, alizaa mtoto mwanaume.
Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
58 Majirani zake na jamii zake wakasikia jinsi Bwana alivyomfanyia rehema kuu, nao wakafurahi pamoja naye.
Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zekaria, ambalo ndilo jina la baba yake.
Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya.
60 Lakini mama yake akakataa na kusema, “Hapana! Jina lake ataitwa Yohana.”
Lakini mama yake akasema, “La, sivyo, bali ataitwa Yohane.”
61 Wakamwambia, “Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo.”
Wakamwambia, “Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?”
62 Basi wakamfanyia Zekaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani.
Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: “Jina lake ni Yohana.”
Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: “Yohane ndilo jina lake.” Wote wakastaajabu.
64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukaachiwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
65 Majirani wote wakajawa na hofu ya Mungu, na katika nchi yote ya vilima vya Uyahudi watu walikuwa wakinena juu ya mambo haya yote.
Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.
66 Kila aliyesikia habari hizi alishangaa akauliza, “Je, mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: “Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?” Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
67 Zekaria, baba yake, akajazwa na Roho Mtakatifu, naye akatoa unabii, akisema:
Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:
68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.
“Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake.
69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,
Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.
70 kama alivyonena kwa vinywa vya manabii wake watakatifu tangu zamani, (aiōn g165)
Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu, (aiōn g165)
71 kwamba atatuokoa kutoka kwa adui zetu, na kutoka mikononi mwao wote watuchukiao:
kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
72 ili kuonyesha rehema kwa baba zetu na kukumbuka Agano lake takatifu,
Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.
73 kiapo alichomwapia baba yetu Abrahamu:
Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi
74 kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu, tupate kumtumikia yeye pasipo hofu
tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,
75 katika utakatifu na haki mbele zake, siku zetu zote.
kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.
76 “Nawe mtoto wangu, utaitwa nabii wa Aliye Juu Sana; kwa kuwa utamtangulia Bwana na kuandaa njia kwa ajili yake,
Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
77 kuwajulisha watu wake juu ya wokovu utakaopatikana kwa kusamehewa dhambi zao,
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.
78 kwa ajili ya wingi wa rehema za Mungu wetu, nuru itokayo juu itatuzukia
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu,
79 ili kuwaangazia wale waishio gizani na katika uvuli wa mauti, kuiongoza miguu yetu katika njia ya amani.”
na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani.”
80 Yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu katika roho; akaishi nyikani hadi siku ile alipojionyesha hadharani kwa Waisraeli.
Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.

< Luka 1 >