< Mambo ya Walawi 9 >

1 Katika siku ya nane, Mose akawaita Aroni na wanawe, na wazee wa Israeli.
Katika siku ya nane, Musa akawaita Aroni na wanawe pamoja na wazee wa Israeli.
2 Akamwambia Aroni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka yako ya dhambi, na kondoo dume kwa sadaka yako ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, nao uwalete mbele za Bwana.
Akamwambia Aroni, “Twaa ndama dume kutoka kundini kwa ajili ya sadaka ya dhambi zako, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, na uwatoe mbele za Yahweh.
3 Kisha waambie Waisraeli: ‘Chukueni mbuzi dume kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na ndama na mwana-kondoo, wote wawili wawe wa umri wa mwaka mmoja, na wasio na dosari, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa,
Zungumza na watu wa Israeli na uwaambie, 'Twaeni beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi na ndama na mwana-kondoo, hawa wawili wawe na umri wa mwaka mmoja na bila dosari, ni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa;
4 na pia maksai na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya amani, ili kutoa dhabihu mbele za Bwana, pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta. Kwa kuwa leo Bwana atawatokea.’”
pia twaeni fahali na kondoo dume kwa sadaka za amani ili kuwatoa mbele za Yahweh, na sadaka za nafaka iliyochanganywa na mafuta, kwa sababu leo Yahweh atajidhihirisha kwenu.
5 Wakavileta vile vitu Mose alivyowaagiza mbele ya Hema la Kukutania, nalo kusanyiko lote likakaribia na kusimama mbele za Bwana.
Kwa hiyo wakaleta kwenye hema la kukutania vyote ambavyo Musa aliagiza, nalo kusanyiko lote la Israeli likakaribia na kusimama mbele za Yahweh.
6 Ndipo Mose akasema, “Hili ndilo Bwana alilowaagiza mlifanye, ili utukufu wa Bwana upate kuonekana kwenu.”
Kisha Musa akasema, “Hivi ndivyo Yahweh amewaamru nyinyi mfanye, ili kwamba utukufu wake uweze kuonekana kwenu.
7 Mose akamwambia Aroni, “Njoo madhabahuni ili utoe dhabihu yako ya sadaka ya dhambi na sadaka yako ya kuteketezwa, ufanye upatanisho kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya watu. Kisha utoe sadaka ya upatanisho kwa ajili ya watu, kama vile Bwana alivyoagiza.”
“Musa akamwambia Aroni, “Njoo karibu na Madhabahu na uteo sadaka yako ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, na kufanya upatanisho kwa ajili ya watu ili kufanya upatanisho kwa ajili yao kama vile ambavyo Yahweh amekwishaamru.”
8 Hivyo Aroni akaja madhabahuni na kumchinja yule ndama kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe.
Kwa hiyo Aroni akaikaribia madhabahu na akamchinja yule ndama kwa ajili ya sadaka ya dhambi, ambayo ilikuwa kwa ajili yake mwenyewe.
9 Wanawe wakamletea damu, naye akachovya kidole chake katika hiyo damu, akaitia kwenye pembe za madhabahu, nayo damu iliyobaki akaimwaga chini ya madhabahu.
Nao wana wa Aroni wakamletea hiyo damu, naye akakichofya kidole chake kwenye damu na kuiweka kwenye pembe za madhabahu, kisha akaimwaga damu chini ya kitako cha madhabahu.
10 Juu ya madhabahu akateketeza mafuta, figo na mafuta yanayofunika ini kutoka kwenye hiyo sadaka ya dhambi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Hata hivyo, aliyateketeza hayo mafuta, figo, na mafuta yanafunika ini juu ya madhabahu kuwa sadaka ya dhambi, kama vile Yahweh alivyokuwa amemwamru Musa.
11 Akateketeza nyama na ngozi nje ya kambi.
Na akaiteketeza hiyo nyama pamoja na ngozi nje ya kambi
12 Kisha Aroni akachinja sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu.
Aroni akaichinja sadaka ya kuteketezwa, nao wanawe wakampa hiyo damu, ambayo aliinyunza pande zote za madhabahu.
13 Wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu.
Kisha wakampa ile sadaka ya kuteketezwa, kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu.
14 Akasafisha sehemu za ndani na miguu, akaviteketeza juu ya sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.
Akaziosha sehemu za ndani pamoja na miguu na kuziteketeza juu ya dhabihu ya kuteketezwa juu ya Madhabahu.
15 Kisha Aroni akaleta sadaka ile iliyokuwa kwa ajili ya watu. Akachukua yule mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, akamchinja na kumtoa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kama alivyofanya kwa ile ya kwanza.
Aroni akaleta dhabihu ya watu— mbuzi, kisha akamtoa kuwa dhabihu kwa ajili ya dhambi yao naye akamchinja, akaitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi, kama alivyofanya kwa yule mbuzi wa kwanza.
16 Aroni akaleta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama ilivyoelekezwa.
Akaileta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama Yahweh alivyokuwa ameamru.
17 Pia akaleta sadaka ya nafaka, akachukua konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.
Akaileta sadaka ya nafaka; akakijaza kiganja chake nafaka na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya asubuhi ya kuteketezwa.
18 Akachinja maksai na kondoo dume kama sadaka ya amani kwa ajili ya watu. Wanawe Aroni wakampa ile damu, naye akainyunyiza kwenye madhabahu pande zote.
Pia akamchinja fahali na yule kondoo dume, dhabihu kwa ajili ya sadaka ya amani, ambayo ilikuwa kwa ajili ya watu. Nao wana wa Aronni wakampa damu, ambayo aliinyunyiza kila upande wa mdhabahu.
19 Lakini sehemu zile za mafuta ya yule maksai na kondoo dume, yaani mafuta ya mkia, mafuta yaliyofunika tumbo, ya figo na yaliyofunika ini,
Hata hivyo, waliyakata mafuta ya fahali na ya yule kondoo dume, mafuta ya kwenye mkia, mafuta yafunikayo sehemu za ndani, figo, na yale mafuta yaliyofunika mapafu.
20 hivi vyote wakaviweka juu ya vidari, kisha Aroni akayateketeza hayo mafuta ya wanyama juu ya madhabahu.
Wakazichukua hizi sehemu zilizokatwa wakaziweka juu ya vidari, na kisha Aroni akateketeza mafuta juu ya madhabahu.
21 Aroni akaviinua vile vidari na paja la kulia mbele za Bwana ili viwe sadaka ya kuinuliwa, kama Mose alivyoagiza.
Naye Aroni akavitikisa vidari na paja la kulia kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za Yahweh, kama vile Musa alivyokuwa ameamru,
22 Kisha Aroni akainua mikono yake kuwaelekea watu na kuwabariki. Naye baada ya kutoa dhabihu ya sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani, akashuka chini.
Kisha Aroni akainua juu mikono yake mbele ya watu na kuwabariki, kisha akashuka chini kutoka mahali alipokuwa akitoa hiyo sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani.
23 Kisha Mose na Aroni wakaingia kwenye Hema la Kukutania. Walipotoka nje, wakawabariki watu. Nao utukufu wa Bwana ukawatokea watu wote.
Musa na Aroni wakaingia ndani ya hema la kukutania, kisha wakatoka nje tena na kuwabariki watu, na utukufu wa Yahweh ukaonekana kwa watu wote.
24 Moto ukaja kutoka uwepo wa Bwana, ukairamba ile sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sehemu ya mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wote walipoona jambo hili, wakapiga kelele kwa furaha na kusujudu.
Moto ukashuka kutoka kwa Yahweh na ukairamba sadaka ya kuteketezwa na mafuta yaliyokuwa juu ya madhabahu. Watu wlipoona jambo hili, wakapiga kelele na kulala chini.

< Mambo ya Walawi 9 >