< Mambo ya Walawi 7 >

1 “‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya hatia, ambayo ni takatifu sana:
Hii ndiyo sheria ya sadaka ya hatia. Kwa sababu hiyo ni sadaka takatifu sana.
2 Sadaka ya hatia itachinjiwa mahali pale ambapo sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa, nayo damu yake itanyunyizwa pande zote za madhabahu.
Ni lazima waichinje sadaka ya hatia mahali panapostali kuchinjwa, na ni lazima watainyunyiza damu yake pande zote za madhabahu.
3 Mafuta yake yote yatatolewa sadaka: mafuta ya mkia na mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani,
Mafuta yote yaliyomo ndani yake yataondolewa: mafuta ya mkiani, mafuta yaliyo sehamu za ndani,
4 figo zote mbili pamoja na mafuta yanayozizunguka yaliyo karibu na kiuno na yale yanayofunika ini, ambayo yataondolewa pamoja na hizo figo.
zile figo mbili pamoja na mafuta yaliyo juu yake, yaliyo karibu na kiuno, na yanayofunika ini—nyama hii yote lazima iondolewe pamoja na hizo figo.
5 Kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia.
Kuhani ataviteketeza vipande hivi juu ya madhabahu viwe dhabihu iliyofanywa kwa Yahweh kwa moto. Hii ni sadaka ya hatia
6 Mwanaume yeyote katika jamaa ya kuhani aweza kuila, lakini lazima iliwe mahali patakatifu; ni takatifu sana.
Kila mwanaume miongoni mwa familia ya kuhani anaweza kula sehemu ya sadaka hii. Lakini ni lazima iliwe ndani ya mahali patakatifu kwa sababu ni takatifu sana.
7 “‘Sheria hii ya sadaka ya hatia ni sawasawa na ile ya sadaka ya dhambi: Nyama ya yule mnyama aliyetolewa sadaka ni ya yule kuhani anayesimamia ibada ya upatanisho.
Nayo sadaka ya dhambi ni kama ilivyo sadaka ya hatia. Ni sheria ileile hutumika kwa zote mbili. Zote ni mali ya kuhani azitumiaye kufanya upatanisho.
8 Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya mtu yeyote anaweza kuichukua ngozi ya mnyama yule aliyetolewa iwe yake.
Kuhani atoaye sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya mtu yeyote anaweza kuchuku ngozi ya sadaka hiyo kwa ajili yake mwenyewe.
9 Kila sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni au kupikwa katika sufuria au katika kikaangio itakuwa ya kuhani anayeitoa.
Kila sadaka ya nafaka inayookwa mekoni, na kila sadaka kama hiyo ipikwayo kaangoni au kwenye sufuria itakuwa ya kuhani aitoaye.
10 Nayo kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au iko kavu, itakuwa ya wana wa Aroni, nayo itagawanywa sawa kati yao.
Kila sadaka ya nafaka, ama iwe unga mkavu au uliochanganywa na mafuta ya zeitu itakuwa ya ukoo wa Aroni kwa usawa.
11 “‘Haya ndiyo masharti kwa ajili ya sadaka ya amani ambayo mtu aweza kuileta kwa Bwana:
Hii ndiyo sheria ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo watu watazitoa kwa Yahweh.
12 “‘Ikiwa mtu atatoa sadaka ya amani kwa ajili ya kuonyesha shukrani, pamoja na sadaka hii ya shukrani, atatoa maandazi yasiyotiwa chachu yaliyochanganywa na mafuta, mikate myembamba isiyotiwa chachu iliyopakwa mafuta, maandazi ya unga laini uliokandwa vizuri na kuchanganywa na mafuta.
Iwapo mtu yeyote anaitoa ili kuonyesha shukrani kwa Yahweh, basi ataitoa pamoja na dhabih uya mikate iliyotengenezwa bila hamira, bali kwa mafuta ya zeituni yaliyochanganywa na unga lakini bila hamira, na maandazi yaliyotengenezwa bila hamira, bali yaliyopakwa mafuta juu yake, na mikate miembamba iliyofanywa kwa unga laini uliochanganywa na mafuta.
13 Pamoja na sadaka hii ya amani ya shukrani ataleta sadaka ya maandazi yaliyotengenezwa kwa chachu.
Kwa kusudi la kutoa shukrani, pia anapaswa kutoa pamoja na sadaka yake ya amani, vipande vya mikate iliyotiwa hamira.
14 Ataleta moja ya kila aina ya andazi kama sadaka, matoleo kwa Bwana; hii ni ya kuhani anayenyunyiza damu ya sadaka ya amani.
Ni lazima atatoa moja kila aina ya sadaka hizi kama sadaka iliyoletwa kwa Yahweh. Nayo itakuwa ya makuhani wanaonyunyizia damu ya sadaka ya amani kwenye madhabahu.
15 Nyama ya sadaka ya amani kwa ajili ya shukrani lazima iliwe siku iyo hiyo inapotolewa; hutabakiza kitu chochote mpaka asubuhi.
Mtu anayeleta sadaka ya amani kwa kusudi la kutoa shukrani ni lazima ataila nyama ya sadaka yake siku ya kutoa dhabihu. Hatakiwi kusaza chochote kilicho cha sadaka hiyo hata asubuhi ya pili.
16 “‘Lakini kama sadaka yake ni kwa ajili ya nadhiri au ni sadaka ya hiari, sadaka hiyo italiwa siku hiyo inapotolewa, lakini chochote kinachobakia kinaweza kuliwa kesho yake.
Lakini iwapo dhabihu ya matoleo yake kusudi lake ni nadhiri, au kwa kusudi la sadaka ya hiari, nyama yake italiwa siku iyo hiyo aitoapo dhabihu yake, lakini chochote kinachosalia cha sadaka hiyo kinaweza kuliwa siku inayofuata.
17 Nyama yoyote ya sadaka inayobaki mpaka siku ya tatu lazima iteketezwe kwa moto.
Hata hivyo, nyama yoyote ya dhabihu inayobaki siku ya tatu ni lazima ichomwe moto.
18 Kama nyama yoyote ya sadaka ya amani italiwa siku ya tatu, Bwana hataikubali. Haitahesabiwa kwake huyo aliyeitoa, kwa kuwa ni najisi. Mtu atakayekula sehemu yake yoyote atahesabiwa hatia.
Iwapo kipande chochote cha nyama hiyo ya dhabihu kinachobaki kinaliwa katika siku ya tatu, hakitakubalika, wala hakitatolewa kwa aliyeitoa. Kitakuwa ni kitu cha kuchukiza, na mtu akilaye atabeba hatia ya dhambi mwenyewe yake.
19 “‘Nyama ile inayogusa chochote ambacho ni najisi kwa kawaida ya ibada kamwe haitaliwa, ni lazima iteketezwe kwa moto. Kuhusu nyama nyingine, mtu yeyote aliye safi kwa kawaida ya ibada anaweza kuila.
Nyama yoyote inayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa. Ni lazima ichomwe moto. Na kwa ajili ya nyama inayobaki, yeyote aliye safi anaweza kuila.
20 Lakini kama mtu yeyote najisi akila nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Bwana, huyo mtu lazima akatiliwe mbali na watu wake.
Hata hivyo, mtu najisi anayekula nyama kutoka kwenye dhabihu ya matoleo ya amani ambayo ni ya Yahweh yapasa mtu huyu akatiliwe mbali kutoka kwa watu wake.
21 Kama mtu yeyote akigusa kitu kilicho najisi, iwe ni uchafu wa mwanadamu, au mnyama najisi, au kitu chochote kilicho najisi, kitu cha kuchukiza, kisha akala nyama yoyote ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Bwana, mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.’”
Iwapo mtu yeyote anagusa kitu chochote kilichonajisi—iwe ni unajisi wa binadamu, au wa mnyama aliyenajisi, au wa kitu fulani kilichonajisi na chenye kuchukiza, na kisha akala baadhi ya nyama ya dhabihu ya sadaka ya amani iliyotolewa kwa Yahweh, lazima mtu huyo akatiliwe mbali kutoka kwa watu wake.
22 Bwana akamwambia Mose,
Kisha Yahweh akazungumza na Musa, akisema,
23 “Waambie Waisraeli: ‘Msile mafuta yoyote ya ngʼombe, kondoo wala mbuzi.
“Zungumza na watu wa Israeli na uwaambie, 'hamruhusiwi kula mafuta ya fahali au kondoo au mbuzi.
24 Mafuta ya mnyama aliyekutwa amekufa au ameraruliwa na mnyama pori yanaweza kutumika kwa kazi nyingine yoyote, lakini kamwe msiyale.
Mafuta ya mnyama yoyote afaye peke yake bila ya kuwa dhabihu, au mafuta ya mnyama yeyote aliyeraruliwa na wanyama pori, yanaweza kutumika kwa makusudi mengine, lakini hakika hamtayala.
25 Mtu yeyote alaye mafuta ya mnyama ambaye ametolewa sadaka kwa Bwana kwa moto ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
Yeyote atakayekula mafuta ya mnyama ambayo watu wanaweza kuyatoa kuwa dhabihu ya iliyofanywa kwa Yahweh kwa moto, mtu huyo lazima atakatiliwa mbali kutoka kwa watu wake.
26 Popote mtakapoishi, kamwe msinywe damu ya ndege yeyote wala ya mnyama.
Hamtakula damu yoyote katika mojawapo ya nyumba zenu, ama iwe kutoka kwa ndege au mnyama.
27 Ikiwa mtu yeyote atakunywa damu, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.’”
Yeyote alaye damu yoyote, mtu huyo lazima akatiliwe mbali kutoka kwa watu wake.'”
28 Bwana akamwambia Mose,
Kwa hiyo Yahweh akazungumza na Musa na akasema,
29 “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote aletaye sadaka ya amani kwa Bwana ataleta sehemu ya sadaka hiyo kama dhabihu yake kwa Bwana.
“Zungumza na watu wa Israeli na uwaambie, 'Yeye atoaye dhabidhu ya sadaka ya amani kwa Yahweh lazima alete sehemu ya dhabihu yake kwa Yahweh.
30 Ataleta sadaka kwa mikono yake mwenyewe iliyotolewa kwa Bwana kwa moto; ataleta mafuta ya huyo mnyama pamoja na kidari, naye atainua hicho kidari mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa.
Mikono yake mwenyewe lazima iilete hiyo sadaka ifanywayo kwa Yahweh kwa moto. Naye atayaleta hayo mafuta pamoja na kidari, ili kwamba kidari kiweze kutikiswa kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za Yahweh.
31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu, lakini kidari kitakuwa cha Aroni na wanawe.
Kuhani atayachoma mafuta hayo juu ya madhabahu, lakini kile kidari kitakuwa mali ya Aroni na uzao wake.
32 Paja la kulia la sadaka zako za amani utampa kuhani kama matoleo.
Ni lazima utatoa paja la kulia kwa kuhani kama sadaka iliyotokana na dhabihu ya sadaka yako ya amani.
33 Mwana wa Aroni atoaye damu na mafuta ya sadaka ya amani ndiye atakayepewa paja hilo la kulia kuwa fungu lake.
Yule kuhani, mmoja wa wazao wa Aroni, atoaye damu na mafuta ya sadaka ya amani—ni lazima atapata paja la kulia kama mgao wake wa sadaka.
34 Kutoka kwenye sadaka za amani za Waisraeli, mimi Mungu nimepokea kidari kile kilichoinuliwa pamoja na lile paja lililotolewa, nami nimevitoa kwa kuhani Aroni na wanawe kuwa fungu lao la kawaida kutoka kwa Waisraeli.’”
Kwa kuwa nimetwaa kidari, na paja la sadaka ya kutikiswa kutoka kwa watu wa Israeli uwe mchango wao, na amepewa Aroni kuhani na wanawe kuwa mgao wao wa kawaida.
35 Hii ndiyo sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, ambazo zilitengwa kwa ajili ya Aroni na wanawe siku ile walipowekwa wakfu ili kumtumikia Bwana katika kazi ya ukuhani.
Huu ndiyo mgao wa Aroni na uzao wake utokanao na matoleo yaliyofanywa kwa Yahweh kwa moto, siku ile Musa alipowaweka wakfu ili kumtumikia Yahweh katika kazi ya kuhani.
36 Siku ile walipotiwa mafuta, Bwana aliagiza kwamba Waisraeli wawape hili kama fungu lao la kawaida kwa vizazi vijavyo.
Huu ndio mgao ambao Yahweh aliamru waweze kupewa kutoka kwa watu wa Israeli, katika siku hiyo aliyowatia mafuta ya upako wawe makuhani. Nao utakuwa mgao wao wa kila siku katika vizazi vyote.
37 Basi haya ndiyo masharti kuhusu sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya nafaka, sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia, sadaka ya kuwekwa wakfu, na sadaka ya amani,
Hii ndiyo sheria ya sadaka ya kuteketezwa, ya sadaka ya nafaka, ya sadaka ya dhambi, ya sadaka ya hatia, ya sadaka ya kuweka wakfu, na ya dhabihu, ya sadaka za amani,
38 ambayo Bwana alimpa Mose juu ya Mlima Sinai siku ile alipowaagiza Waisraeli walete sadaka zao kwa Bwana, katika Jangwa la Sinai.
ni sheria ambazo Yahweh alizitoa kwa Musa kwenye Mlima Sinai siku aliyowaamru watu wa Israeli kutoa dhabihu zao kwa Yahweh katika jangwa la Sinai.'”

< Mambo ya Walawi 7 >