< Mambo ya Walawi 5 >
1 “‘Ikiwa mtu atakuwa ametenda dhambi kwa sababu hakusema alipotakiwa kutoa ushahidi hadharani kuhusu jambo aliloona au kujua habari zake, yeye anastahili adhabu.
2 “‘Au kama mtu akigusa kitu chochote ambacho ni najisi, iwe ni mizoga ya wanyama pori walio najisi, au ya wanyama wafugwao walio najisi, au ya viumbe vitambaavyo ardhini, hata akiwa hana habari, amekuwa najisi na mwenye hatia.
3 “‘Au kama akigusa kitu kilicho kichafu kinachotokana na binadamu, kitu chochote kile kinachoweza kumfanya awe najisi, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia.
4 “‘Au kama mtu ameapa kufanya kitu chochote bila kufikiri, kiwe chema au kibaya, kwa vyovyote mtu aweza kuapa bila kujali, hata akiwa hana habari, atakapofahamu atakuwa na hatia.
5 “‘Wakati mtu yeyote atakapokuwa na hatia katika mojawapo ya haya, lazima akiri ni kwa njia gani ametenda dhambi,
6 na kama adhabu ya dhambi aliyoitenda, lazima alete kwa Bwana kondoo jike au mbuzi jike kutoka kwenye kundi lake kama sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yake.
7 “‘Lakini huyo mtu kama hataweza kumtoa mwana-kondoo, ataleta hua wawili au makinda mawili ya njiwa kwa Bwana kuwa adhabu kwa ajili ya dhambi yake, mmoja wa hao ndege kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na wa pili kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
8 Atawaleta kwa kuhani, ambaye atamtoa kwanza ndege mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Atamvunja shingo na kuacha kichwa chake kikiningʼinia,
9 naye atanyunyiza sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi kwenye pembe za madhabahu. Damu iliyobaki lazima ichuruzwe chini ya madhabahu. Hii ni sadaka ya dhambi.
10 Kisha kuhani atamtoa yule ndege wa pili kama sadaka ya kuteketezwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na hivyo kufanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.
11 “‘Ikiwa basi, hawezi kupata hua wawili au makinda mawili ya njiwa, ataleta sehemu ya kumi ya efa ya unga laini kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Kamwe asiweke mafuta wala uvumba juu yake, kwa sababu ni sadaka ya dhambi.
12 Atauleta unga kwa kuhani, ambaye atachukua konzi moja kama sehemu ya kumbukumbu na atauteketeza kwenye madhabahu juu ya sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto. Hii ni sadaka ya dhambi.
13 Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi yoyote ya hizo alizotenda, naye atasamehewa. Sadaka iliyobaki itakuwa ya kuhani, kama ilivyokuwa ile sadaka ya nafaka.’”
14 Bwana akamwambia Mose:
15 “Mtu anapokiuka na kutenda dhambi pasipo kukusudia kuhusu mojawapo ya mambo matakatifu ya Bwana, huyo mtu ataleta kwa Bwana kama adhabu kondoo dume mmoja kutoka kundi lake, asiye na dosari na mwenye thamani halisi kifedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu. Hii ni sadaka ya hatia.
16 Ni lazima alipe kwa yale aliyoshindwa kufanya kuhusu vitu vitakatifu, kwa kuongeza sehemu ya tano ya thamani ile na kuitoa yote kwa kuhani, ambaye atamfanyia upatanisho kwa huyo kondoo dume kama sadaka ya dhambi, naye atasamehewa.
17 “Kama mtu akifanya dhambi na kufanya yale yaliyokatazwa katika mojawapo ya amri za Bwana, hata ikiwa hajui, yeye ana hatia na anastahili adhabu.
18 Atamletea kuhani kama sadaka ya hatia kondoo dume kutoka kundi lake, kondoo asiye na dosari na mwenye thamani halisi kifedha. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa kosa alilotenda bila kukusudia, naye atasamehewa.
19 Hii ni sadaka ya hatia; amekuwa na hatia kwa kufanya kosa dhidi ya Bwana.”