< Mambo ya Walawi 4 >

1 Bwana akamwambia Mose,
Bwana alisema na Musa na kumwambi,
2 “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote afanyapo dhambi bila kukusudia na akatenda lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana:
“Waambie wana wa Israeli 'mtu yeyote akifanya dhambi bila kukusudia, kufanya chochote ambacho Bwana ameagiza kutofanya, na kama akifanya chochote kilichozuiliwa, yafuatayo lazima yatatendeka.
3 “‘Ikiwa kuhani aliyetiwa mafuta amefanya dhambi na kuwaletea watu hatia, lazima alete kwa Bwana fahali mchanga asiye na dosari, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya dhambi aliyotenda.
Kama ni kuhani mkuu aliyetenda dhambi na kuleta hatia kwa watu, atatoa dume asiyekuwa na kasoro kwa Bwana kwa ajili ya dhambi aliyotenda kama sadaka ya dhambi.
4 Atamkabidhi huyo fahali kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Bwana. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo fahali na kumchinja mbele za Bwana.
Ataleta dume mbele ya mlango wa hema ya kukutania mbele ya Bwana, ataweka mikono juu ya dume, na atamchinja huyo dume mbele za Bwana.
5 Kisha kuhani huyo aliyetiwa mafuta atachukua sehemu ya damu ya huyo fahali na kuileta katika Hema la Kukutania.
Kuhani aliyewekewa mafuta atachukua damu ya dume na kuileta mbele ya hema ya kukutania.
6 Atachovya kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza sehemu yake mara saba mbele za Bwana mbele ya pazia la mahali patakatifu.
Kuhani atazamisha kidole chake katika damu na kuinyunyiza mara saba mbele za Bwana, mbele ya pazia la mahali pa takatifu.
7 Kisha kuhani atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba wenye harufu nzuri iliyoko mbele za Bwana katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ya huyo fahali ataimwaga chini ya hayo madhabahu ya kuteketezea sadaka kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
Na kuhani ataweka kiasi cha damu ya huyo dume juu ya pembe za madhabahu ya kuvukizia uvumba mbele za Bwana, katika hema ya kukutania na ataimwaga yote iliyobaki chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mahali pa kuinglia katika hema ya kukutania.
8 Atayaondoa mafuta yote ya fahali huyo wa sadaka ya dhambi, mafuta yale yanayofunika sehemu za ndani au zile zinazounganika nazo,
Atakata mafuta yote ya dume wa sadaka ya dhambi, mafuta yanayofunika matumbo na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
9 figo zote mbili na mafuta yaliyo juu yake karibu na kiuno na yale yanayofunika ini ambayo atayaondoa pamoja na figo zote,
figo mbili na mafuta yaliyopo pamoja nazo, yaliyo karibu na kiuno na kitambi cha maini pamoja na hizo figo.
10 kama vile mafuta yanayoondolewa kutoka kwenye maksai aliyetolewa sadaka ya amani. Kisha kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
Ataondoa zote vile vile kama yanavyoondolewa katika dume wa sadaka ya dhabihu ya amani. Kuhani atatekeza sehemu hizo katika madhabahu ya sadaka za kuteketezwa.
11 Lakini ngozi ya huyo fahali na nyama zake zote, pamoja na kichwa na miguu yake, sehemu za ndani na matumbo,
Ngozi ya dume na mabaki yoyote ya nyama, pamoja na kichwa chake, miguu yake, matumbo yake na mavi yake,
12 yaani sehemu nyingine zote zilizobaki za huyo fahali, lazima azitoe nje ya kambi mpaka mahali palipo safi kiibada, ambapo majivu hutupwa, naye atamchoma kwa moto juu ya kuni zilizoko juu ya lundo la majivu.
mabaki yote ya dume atayachukua nje ya mji mahali palipo safi, mahali wanapomwaga majivu; watateketeza sehemu zote juu ya kuni. Watateketeza sehemu zote mahali wanapomwaga majivu.
13 “‘Ikiwa jumuiya yote ya Israeli watatenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana, hata kama jumuiya haifahamu juu ya jambo hilo, wana hatia.
Kama mkutano wote wa wana wa Israeli wakitenda dhambi bila kukusudia, na mkutano hawatakumbuka kwamba wametenda dhambi, na kufanya vile Bwana aliagiza wasifanye na wakajisikia hatia.
14 Wanapotambua kuhusu dhambi waliyoitenda, lazima kusanyiko lilete fahali mchanga kuwa sadaka ya dhambi na kuikabidhi mbele ya Hema la Kukutania.
Na dhambi waliyofanya ikajulikana, mkutano watatoa ng'ombe dume mchanga kuwa sadaka ya dhambi watamleta mbele ya hema ya kukutania.
15 Wazee wa jumuiya wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali aliye mbele za Bwana, naye fahali atachinjwa mbele za Bwana.
Wazee wa mkutano wataweka mikono yao juu ya kichwa cha ng'ombe mbele za Bwana, na ng'ombe atachinjwa mbele za Bwana.
16 Kisha kuhani aliyetiwa mafuta ataiingiza sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya Hema la Kukutania.
Kuhani aliyetiwa mafuta ataleta damu ya ng'ombe katika hema ya kukutania,
17 Atachovya kidole chake kwenye damu na kuinyunyiza mara saba mbele za Bwana mbele ya hilo pazia.
kuhani atachovya kidole chake katika damu na kuinyunyizia mara saba mbele za Bwana mbele ya pazia.
18 Atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu yaliyo mbele za Bwana katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu ya kuteketezea sadaka, penye ingilio la Hema la Kukutania.
Ataweka kiasi cha damu katika pembe za madhabahu mbele za Bwana iliyo katika hema ya kukutania na ataimwaga damu yote chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo katika mlango wa kuingilia katika hema ya kukutania.
19 Atayaondoa mafuta yote ya yule fahali na kuyateketeza juu ya madhabahu,
Atakata mafuta yote na kuyatekeza katika madhabahu.
20 naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa.
Hivyo ndivyo atakavyomfanya huyo ng'ombe, kama alivyomfanya ng'ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia vivyo hivyo huyu ng'ombe, kuhani atawafanyia upatanisho watu nao watasamehewa.
21 Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya.
Atamchukua huyo ng'ombe nje ya mji na kumteketeza kama alivyomteketeza ng, ombe wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano.
22 “‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya Bwana Mungu wake, ana hatia.
Mtawala akitenda dhambi bila kukusudia kufanya moja ya yale Bwana Mungu wake ameagiza kutotenda, na anajisikia hatia
23 Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete mbuzi dume asiye na dosari kama sadaka yake.
na kama dhambi yake aliyotenda anaifahamu, ataleta dhabihu yake mbuzi mme asiye na kasoro.
24 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale ambapo sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za Bwana. Hii ni sadaka ya dhambi.
Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mbuzi na kumchinja mahali ambapo huchinja sadaka ya kuteketezwa mbele za Bwana. Hii ni sadaka ya dhambi.
25 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu.
Kuhani atachukua damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuiweka juu ya pembe za madhabahu kwa dhabihu ya kuteketezwa, na atamwaga damu chini ya madhabahu ya dhabihu ya kuteketezwa.
26 Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa.
Atateketeza mafuta yote katika madhabahu, kama vile mafuta ya dhabihu ya sadaka ya amani, Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya mtawala kulingana na dhambi yake, na mtawala atakuwa amesamehewa.
27 “‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana, yeye ana hatia.
Kama yeyote wa watu wa kawaida akitenda dhambi bila kukusudia, kufanya vitu ambavyo Bwana ameagiza kutokufanywa na kama ana hatia,
28 Atakapofahamishwa dhambi yake aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kama sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda.
ndipo dhambi yake aliyoitenda ikajulikana kwake, ndipo ataleta mbuzi mke asiyekuwa na kasoro awe dhabihu kwa ajili ya dhambi zake alizotenda.
29 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka.
Ataweka mikono yake juu ya sadaka ya dhambi na kuchinja sadaka ya dhambi mahali pa sadaka ya kuteketezwa.
30 Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu.
Kuhani atachukua kiasi cha damu kwa kidole chake na kuweka katika pembe za madhabahu ya dhabihu ya kuteketezwa. Damu yote iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu.
31 Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.
Atayaondoa mafuta yote, kama alivyoondoa mafuta katika dhabihu ya amani. Kuhani ataiteketeza katika madhabahu ili kuwa harufu nzuri kwa Bwana. Kuhani atafanya upatanisho kwa mtu, na atasamehewa.
32 “‘Ikiwa ataleta mwana-kondoo kama sadaka yake ya dhambi, atamleta jike asiye na dosari.
Kama mtu ataleta mwanakondoo kama dhabihu yake kwa sadaka ya dhambi, ataleta jike asiye na kasoro.
33 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo mwana-kondoo na kumchinja kwa ajili ya sadaka ya dhambi mahali sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa.
Ataweka mikono kichwani mwa sadaka ya dhambi na atamchinja kuwa sadaka ya dhambi mahali wanapochinjwa sadaka ya kuteketezwa.
34 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia juu ya pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na ile damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu.
Kuhani atachukua baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuweka katika pembe za madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, na ataimwaga damu yote chini ya madhabahu.
35 Ataondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kutoka kwenye mwana-kondoo wa sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu juu ya zile sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.
Ataondoa mafuta yote, kama akatavyo mafuta ya mwanakondoo dhabihu ya sadaka ya amani na kuhani ataiteketeza juu ya madhabahu juu ya sadaka ya Bwana itolewayo kwa moto. Kuhani ataleta upatanisho kwa dhambi aliyoifanya, naye atasamehewa.

< Mambo ya Walawi 4 >