< Mambo ya Walawi 26 >
1 “‘Msijitengenezee sanamu au kusimamisha kinyago cha kuchonga, au mnara, wala jiwe la kuabudia, na pia msijiwekee jiwe lililochongwa katika nchi yenu na kusujudu mbele yake. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
2 “‘Zishikeni Sabato zangu na kuheshimu mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Bwana.
3 “‘Ikiwa mtafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii maagizo yangu,
4 nitawanyeshea mvua katika majira yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.
5 Kupura nafaka kwenu kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu. Pia kuvuna zabibu kutaendelea mpaka wakati wa kupanda mbegu, nanyi mtakula na kushiba, na mtaishi salama katika nchi yenu.
6 “‘Nitawapa amani katika nchi, mpate kulala pasipo kutiwa hofu na yeyote. Nitawaondoa wanyama wakali watoke kwenye nchi, nao upanga hautapita katika nchi yenu.
7 Mtawafukuza adui zenu, nanyi mtawaua kwa upanga mbele yenu.
8 Watu wenu watano watafukuza adui mia, watu wenu mia watafukuza adui elfu kumi, nao adui zenu wataanguka kwa upanga mbele yenu.
9 “‘Nitawaangalia kwa upendeleo na kuwafanya mzae na kuzidisha idadi yenu, nami nitalishika Agano langu na ninyi.
10 Wakati wa kuvuna mtakuwa bado mnakula mavuno ya mwaka uliopita, na itawalazimu kuyaondoa ghalani ili mpate nafasi ya mavuno mapya.
11 Nitafanya makao yangu miongoni mwenu, nami sitawachukia.
12 Nitatembea katikati yenu niwe Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu.
13 Mimi ndimi Bwana Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili msiendelee kuwa watumwa wa Wamisri, nikavunja kongwa lenu, na kuwawezesha kutembea mkiwa mmeinua vichwa vyenu juu.
14 “‘Lakini kama hamtanisikiliza na kutimiza maagizo haya yote,
15 nanyi kama mtazikataa amri zangu na kuzichukia sheria zangu, tena mkishindwa kutimiza amri zangu na hivyo mkavunja agano langu,
16 ndipo nitakapowafanyia hili: Nitawaletea juu yenu hofu ya ghafula, magonjwa ya kufisha, na homa itakayopofusha macho yenu na kuwaondolea uhai wenu. Mtapanda mbegu bila mafanikio, kwa sababu adui zenu wataila.
17 Nitauelekeza uso wangu dhidi yenu ili mshindwe na adui zenu; wale wanaowachukia watawatawala, nanyi mtakimbia ingawa hakuna mtu anayewafukuza.
18 “‘Kama baada ya haya yote hamtanisikiliza, nitawaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.
19 Nitakivunja kiburi chenu cha ukaidi na kuifanya anga iliyo juu yenu iwe kama chuma, na ardhi yenu kama shaba.
20 Nguvu zenu zitatumika bila ya mafanikio, kwa sababu ardhi yenu haitawazalia mazao yake, wala miti ya nchi yenu haitazaa matunda yake.
21 “‘Kama mtaendelea kuwa na uadui nami, na kukataa kunisikiliza, nitawazidishia mateso yenu mara saba zaidi, kama dhambi zenu zinavyostahili.
22 Nitawatuma wanyama mwitu dhidi yenu, nao watawaibieni watoto wenu, watawaangamiza ngʼombe wenu, na kuifanya idadi yenu kuwa ndogo, hivi kwamba barabara zenu zitakuwa hazina watu.
23 “‘Ikiwa pamoja na mambo haya hamtakubali maonyo yangu lakini mkaendelea kuweka uadui nami,
24 mimi mwenyewe nitaweka uadui nanyi, na kuwatesa kwa ajili ya dhambi zenu mara saba zaidi.
25 Nitawaletea upanga juu yenu ili kuwapatiliza kwa kuvunja Agano langu. Mtakapokimbilia mijini mwenu, nitatuma tauni katikati yenu, nanyi mtatiwa mikononi mwa adui zenu.
26 Nitakapowaondolea upatikanaji wa mkate wenu, wanawake kumi wataoka mkate wenu katika tanuru moja, nao wataugawa mkate kidogo kwa kupima. Mtakula, lakini hamtashiba.
27 “‘Kama hata baada ya haya bado hamtanisikiliza lakini mkaendelea kuweka uadui nami,
28 ndipo katika hasira yangu nitaweka uadui nanyi, nami mwenyewe nitawaadhibu mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
29 Mtakula nyama ya wana wenu na nyama ya binti zenu.
30 Nitapaharibu mahali penu pa juu pa kuabudia miungu, nibomoe madhabahu zenu za kufukizia uvumba, na kuzilundika maiti zenu juu ya sanamu zenu zisizo na uhai, nami nitawachukia ninyi sana.
31 Nitaifanya miji yenu kuwa magofu, na kuharibu mahali patakatifu penu pa kuabudia, nami sitapendezwa na harufu nzuri ya sadaka zenu.
32 Nitaiharibu nchi, ili adui zenu watakaokuja kuishi humo washangae.
33 Nitawatawanya ninyi miongoni mwa mataifa, na kuufuta upanga wangu na kuwafuatia. Nchi yenu itaharibiwa, nayo miji yenu itakuwa magofu.
34 Ndipo nchi itafurahia Sabato zake muda wote ule itakapokuwa ukiwa, nanyi mkiwa katika nchi ya adui zenu. Ndipo nchi itapumzika na kufurahia Sabato zake.
35 Wakati wote nchi itakapobaki ukiwa, itapumzika na kufurahia Sabato zake ambazo haikuzipata mlipokuwa mnaishi humo.
36 “‘Kwa habari ya wenzenu wale watakaobaki, nitaifanya mioyo yao kuwa na hofu kuu katika nchi za adui zao, kiasi kwamba sauti ya jani linalopeperushwa na upepo itawafanya wakimbie. Watakimbia kana kwamba wanakimbia upanga, nao wataanguka, ingawa hakuna anayewafukuza.
37 Watajikwaa mmoja juu ya mwingine kama wakimbiao upanga, hata ingawa hakuna anayewafuatia. Hivyo hamtaweza kusimama mbele ya adui zenu.
38 Mtaangamia katikati ya mataifa; nchi ya adui zenu itawala.
39 Wale wenu watakaobaki wataangamia katika nchi za adui zao kwa sababu ya dhambi zao; pia kwa sababu ya dhambi za baba zao wataangamia.
40 “‘Lakini kama watatubu dhambi zao na dhambi za baba zao, udanganyifu wao dhidi yangu na uadui wao kwangu,
41 ambao ulinifanya niwe na uadui nao hata nikawapeleka katika nchi ya adui zao, wakati mioyo yao isiyotahiriwa itanyenyekea na kutubu dhambi yao,
42 nami nitakumbuka agano langu na Yakobo, na agano langu na Isaki, na agano langu na Abrahamu, nami nitaikumbuka nchi.
43 Kwa kuwa wataiacha nchi ukiwa, nayo itafurahia Sabato zake wakati itakuwa ukiwa bila wao. Wataadhibiwa kwa ajili ya dhambi zao, kwa sababu walizikataa sheria zangu na kuzichukia amri zangu.
44 Lakini pamoja na hili, wakati watakuwa katika nchi ya adui zao, sitawakataa wala kuwachukia kiasi cha kuwaharibu kabisa na kuvunja agano langu nao. Mimi ndimi Bwana Mungu wao.
45 Lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano langu na baba zao, ambao niliwatoa Misri mbele ya mataifa ili niwe Mungu wao. Mimi ndimi Bwana.’”
46 Hizi ndizo amri, sheria na pia masharti ambazo Bwana alifanya kati yake mwenyewe na Waisraeli katika Mlima Sinai kupitia kwa Mose.