< Mambo ya Walawi 22 >

1 Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akazungumza na Musa, kusema,
2 “Mwambie Aroni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi Bwana.
“Ongea na Aroni na wanawe, waambie wajiepushe na vitu vitakatifu vya watu wa Israeli wanavyovitenga kwangu. Wasilinajisi jina langu. Mimi ndimi Yahweh.
3 “Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa yeyote wa wazao wako ni najisi kwa taratibu za kiibada, naye akakaribia sadaka takatifu zile Waisraeli wanazoweka wakfu kwa Bwana, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi Bwana.
Waambie, 'Ikiwa mmoja wa wazao wenu katika vizazi vyenu vyote anakaribia vitu vitakatiifu vile ambavyo watu wa Israeli wamevitenga kwa Yahweh, wakati akiwa najisi, sharti mtu huyo akatiliwe mbali atoke mbele zangu. Mimi ndimi Yahweh.
4 “‘Ikiwa mzao wa Aroni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu mpaka atakasike. Pia atakuwa najisi ikiwa atagusa kitu chochote kilicho najisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa,
Hatakuwapo yeyote wa uzao wa Aroni aliye na ungonjwa wa ngozi wa kuambukiza, au maambukizi yatirirkayo kutoka mwilini mwake, atakayekula sehemu yoyote ya dhabihu inatolewayo kwa Yahweh mpaka atakapotakasika. Yeyote agusaye kitu chochote kilichonajisi kwa njia ya kugusa maiti, au kwa kumgusa mtu yeyote aliyetokwa na shahawa,
5 au ikiwa atagusa kitu chochote kitambaacho kimfanyacho mtu najisi, au mtu yeyote awezaye kumtia unajisi, hata unajisi uwe gani.
au yeyote agusaye mnyama atakayemtia unajisi, au mtu yeyote atakayemfanya najisi, kwa hiyo unajisi wowote unaweza kuwa—
6 Mtu anayegusa kitu chochote cha aina hiyo atakuwa najisi mpaka jioni. Kamwe hatakula sadaka yoyote takatifu mpaka yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji.
kuhani yeyote agusaye kitu chochote kisichosafi atakuwa najisi hata jioni. Hatakula chochote cha vitu vitakatifu, isipokuwa ameuosha mwili wake katika maji.
7 Wakati jua linapotua, atakuwa safi, na baadaye anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake.
Jua linapotua, ndipo atakuwa safi. Baada ya machweo anaweza kula kutoka katika vitu vitakatifu, kwasababu hivyo ni vyakuala vyake.
8 Kamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi Bwana.
Asile mzoga wowote uliookotwa au mnyama aliyeraruliwa na wanyama pori, ambaye kwake atajitia unajisi. Mimi ndimi Yahweh.
9 “‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu.
Ni lazima makuhani wafuate maagizo yangu, ama sivyo watakuwa na hatia ya dhambi na wangeweza kufa kwa kunitia unajisi. Mimi ndimi Yahweh ninayewafanya wao watakatifu.
10 “‘Hakuna mtu yeyote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, hata mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila.
Hakuna mtu kutoka nje ya familia ya kuahani, wakiwemo wageni wa kuhani au watumwa wake wa kuajiliwa, atakayeweza kula kitu chochote kilicho kitakatifu.
11 Lakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani.
Lakini kama huyo kuhani amenunua mtumwa kwa fedha yake mwenyewe, mtumwa huyo anaweza kula kutoka katika vitu vilivyotengwa kwa Yahweh. Na watu wa familia ya kuhani na watumwa waliozaliwa nyumbani mwake, pia wanaweza kula pamoja naye kutoka katika vitu hivyo.
12 Ikiwa binti wa kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula chochote cha matoleo matakatifu.
Ikiwa binti wa kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, hataweza kula chochote cha mchango wa matoleo matakatifu.
13 Lakini ikiwa binti wa kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, na akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula chochote katika chakula hiki.
Lakini ikiwa huyo binti wa kuhani ni mjane au ametalikiwa, na ikiwa hana mtoto, na anarudi kuishi knyumbani kwa baba yake kama alivyokuwa wakati wa ujana wake, anaweza kula kutoka katika chakula cha baba yake. Lakini hakuna yeyote asiye wa familia ya kikuhani anatakayeruhusiwa kula kutoka katika chakula cha kuhani.
14 “‘Ikiwa mtu yeyote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo.
Kama mtu anakula chakula kitakatifu bila ya kukijua, naye atamlipa kuahani kwa ajili ya hicho; itampasa kuongeza moja ya tano juu yake na kukirejesha kwa kuhani.
15 Kamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa Bwana
Haiwapasi watu wa Israeli kutoheshimu vitu vitakatifu ambavyo vimeinuliwa juu na kuletwa kwa Yahweh,
16 kwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi Bwana niwafanyaye watakatifu.’”
kisha wakajisababishia wenyewe kuchukua dhambi amabyo ingewafanya kuwa na hatia ya kula chakula kitakatifu, kwa kuwa mimi ndimi Yahweh awafanyaye wao watakatifu.”
17 Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akazungumza na Musa, akasema,
18 “Sema na Aroni na wanawe, na Waisraeli wote uwaambie: ‘Ikiwa mmoja wenu, aliye Mwisraeli au mgeni anayeishi katika nchi ya Israeli, atatoa matoleo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Bwana, iwe kutimiza nadhiri au kuwa sadaka ya hiari,
“Sema na Aroni na wanawe, na kwa watu wa Israeli wote. Waambie, Mwisraeli yeyote, au Mgeni anayeishi katika Israeli, waletapo dhabihu—iwe ni kutimiza kiapo, au iwe ni sadaka ya hiari, au wanaleta kwa Yahweh sadaka ya kuteketezwa kwa moto,
19 lazima mtoe mnyama dume asiye na dosari, akiwa ngʼombe, mbuzi au kondoo, ili aweze kukubalika kwa niaba yako.
ikiwa wanataka ikubalike, ni lazima watowe mnyama dume asiye na dosari, kutoka kwenye kundi la ng'ombe, kondoo au mbuzi
20 Kamwe usitoe kitu chochote chenye dosari kwa sababu hakitakubaliwa kwa niaba yako.
Lakini hamtatoa chochote kilicho na dosari. Sitakipokea kwa niaba yenu.
21 Mtu yeyote aletapo sadaka ya amani kwa Bwana kutoka kundi la ngʼombe au mbuzi ili kutimiza nadhiri maalum au sadaka ya hiari, lazima sadaka hiyo isiwe na dosari au waa ili ikubalike.
Yeyote atoae dhabihu ya sadaka ya ushirika kutoka katika kundi la ng'ombe au la kondoo kwa Yahweh ili kutimiza kiapo, au kama sadaka ya hiari, ili ikubalike, ni lazima isiwe na kilema. Ni lazima pasiweko na kasoro katika mnyama.
22 Kamwe usimtolee Bwana mnyama aliye kipofu, aliyejeruhiwa wala aliye kilema, au chochote kilicho na uvimbe, au chenye upele au vidonda vinavyotoka usaha. Kamwe chochote cha aina hii kisiwekwe juu ya madhabahu kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto.
Msitoe kabisa wanyama waliovipofu, waliojeruhiwa, wala walio na kilema, wenye upele, vidonda vitokavyo usaha, wala wenye vigaga. Msiwatoe hawa kuwa dhabihu ya kuteketezwa kwa moto iliyotolewa kwa Yahweh juu ya madhabahu.
23 Lakini waweza ukatoa ngʼombe au kondoo mwenye kilema au aliyedumaa kama sadaka ya hiari, lakini hii haitakubalika kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri.
Unaweza kumleta makisai au mwana-kondoo mlemavu au aliyedumaa kuwa sadaka ya hiari, lakini sadaka kama hiyo kwa ajili kutimiza kiapo, haitapokelewa.
24 Kamwe usimtolee Bwana mnyama ambaye mapumbu yake yamejeruhiwa, au kuhasiwa, au kuraruliwa au kukatwa. Kamwe usifanye hivi katika nchi yako mwenyewe,
Usitoe kwa Yahweh mnyama yeyote aliyetiwa jeraha, kupondwa, au kukatwa korodani zake.
25 na kamwe usikubali wanyama wa aina hii kutoka mkono wa mgeni ili kuwatoa wanyama hao kuwa chakula kwa Mungu wako. Wanyama hao hawatakubaliwa kwa niaba yako, kwa sababu wana vilema, nao wana dosari.’”
Usifanye haya katika nchi yako. Usilete mkate wa Mungu wako kutoka mkononi mwa mgeni. Hao wanyama wenye vilema na dosari ndani yao, hawatapokelewa kabisa kwa ajili yako.
26 Bwana akamwambia Mose,
Yahweh akamwambia Musa na akasema,
27 “Wakati ndama, mwana-kondoo au mwana-mbuzi azaliwapo, atabaki na mama yake kwa siku saba. Kuanzia siku ya nane na kuendelea anaweza kukubaliwa kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto.
“Wakati ndama, mwana—kondo au mwana—mbuzi azaliwapo, sharti abaki na mama yake kwa muda wa siku saba. Ndipo kuanzia siku ya nane na kuendelea, anaweza kupokelewa kuwa dhabihu iliyofanywa kwa moto kwa Yahweh.
28 Usimchinje ngʼombe na ndama wake, au kondoo na kitoto chake siku moja.
Usimchinje ng'ombe jike pamoja na ndama wake au mbuzi jike pamoja na kitoto chake kwa siku moja.
29 “Unapomtolea Bwana dhabihu ya shukrani, itoe kwa namna ambayo itakubalika kwa niaba yako.
Utoapo sadaka ya shukrani kwa Yahweh utaitoa kwa njia iliyokubalika.
30 Ni lazima iliwe siku iyo hiyo, pasipo kubakiza chochote mpaka asubuhi. Mimi ndimi Bwana.
Ni lazima iliwe siku iyo hiyo inayotolewa. Hutakiwi kubakiza chochote hata asubuhi. Mimi ndimi Yahweh.
31 “Shikeni maagizo yangu na kuyafuata. Mimi ndimi Bwana.
Kwa hiyo imewapasa kuzishika amri zangu na kuzifuata. Mimi ndimi Yahweh.
32 Msilinajisi Jina langu takatifu. Lazima nikubalike kuwa mtakatifu kwa Waisraeli. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu,
Msiliabishe jina langu takatifu. Ni lazima nitambuliwe kuwa ni mtakatifu na watu wa Israeli. Mimi ndimi Yahweh niwafanyaye ninyi watakatifu,
33 na niliyewatoa katika nchi ya Misri niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana.”
ambaye amewaleta kutoka katika nchi ya Misri ili niwe Mungu wenu: Mimi ndimi Yahweh.”

< Mambo ya Walawi 22 >