< Mambo ya Walawi 16 >

1 Bwana akasema na Mose baada ya kifo cha wale wana wawili wa Aroni waliokufa walipokaribia mbele za Bwana.
Yahwe alizungumza na Musa - hii ni baada vifo vya wana wawili wa Haruni, walipomkaribia Yahwe na ndipo wakafa.
2 Bwana akamwambia Mose: “Mwambie ndugu yako Aroni asije wakati wowote atakavyo yeye ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, nyuma ya pazia pale mbele ya kiti cha rehema kile kilichoko juu ya Sanduku la Agano, la sivyo atakufa, kwa sababu huwa ninatokea ndani ya wingu juu ya kile kiti cha rehema.
Yahwe alimwambia Musa, “Ongea na Haruni kaka yako na umwambie hapana kuja tu wakati wowote katika patakatifu pa patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kifuniko cha upatanisho kilicho juu ya sanduku. Akifanya hivyo, anakufa, kwasababu naonekana katika wingu juu ya kifuniko cha upatanisho.
3 “Hivi ndivyo Aroni atakavyoingia katika mahali patakatifu: atachukua fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
Hivi ndivyo jinsi Haruni lazima aje katika patakatifu pa patakatifu. Yeye lazima aingie pamoja na ndama kama sadaka ya dhambi, na kondoo dume kama sadaka ya dhambi.
4 Atavaa koti takatifu la kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani; atafunga mshipi wa kitani kiunoni, na kuvaa kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu, kwa hiyo ni lazima aoge kwa maji kabla ya kuyavaa mavazi hayo.
Ni lazima avae kanzu ya kitatani, na lazima avae ndani yake nguo ya kitani, na lazima avae mshipi wa kitani na kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu. Lazima aoge mwili wake katika maji na avae mavazi haya.
5 Atachukua mbuzi dume wawili kutoka kwa jumuiya ya Israeli kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
Lazima achukue kwenye umati wa watu wa Israeli mbuzi wawili waume kama sadaka ya dhambi na kondoo dume moja ikiwa ni sadaka ya kuteketezwa.
6 “Aroni atamtoa huyo fahali kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi ili afanye upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake.
Ndipo Haruni lazima alete ng'ombe kama sadaka ya dhambi, ambayo itakuwa kwaajili yake mwenyewe, kufanya upatanisho kwaajili yake mwenyewe na familia yake.
7 Kisha atawachukua wale mbuzi dume wawili na kuwaleta mbele za Bwana kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
Ndipo lazima achukue mbuzi wawili na kuwaweka mbele ya Yahwe katika mlango wa kuingilia kwenye hema ya mkutano.
8 Aroni atapiga kura kwa ajili ya hao mbuzi wawili, mmoja kwa ajili ya Bwana na mwingine kwa ajili ya kubebeshwa dhambi.
Ndipo Haruni lazima apige kura kwaajili ya mbuzi hao wawili, kura moja kwaajili ya Yahwe, na kura nyingine kwaajili ya msingiziwa.
9 Aroni atamleta yule mbuzi ambaye kura ya Bwana imemwangukia na kumtoa dhabihu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
Ndipo Haruni lazima awasilishe mbuzi ambaye kura imeangukia kwa Yahwe, na kumtoa mbuzi huyo kama sadaka ya dhambi.
10 Lakini mbuzi aliyechaguliwa kwa kura kuwa wa kubebeshwa dhambi atatolewa akiwa hai mbele za Bwana, atumike kwa kufanya upatanisho kwa kumwacha aende jangwani akiwa amebebeshwa dhambi.
Lakini mbuzi ambaye kura ya usingiziwa imemwangukia lazima aletwe kwa Yahwe akiwa hai, kufanya upatanisho kwa kumwachia aende porini kama, mbuzimsingiziwa.
11 “Aroni atamleta yule fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na nyumba yake, naye atamchinja huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe.
Pia Haruni lazima alete ng'ombe kwaajili ya sadaka ya dhambi, ambayo itakuwa kwaajili yake mwenyewe, lazima afanye upatanisho kwaajili yake mwenyewe na familia yake, hivyo lazima yeye amuue huyo ng'ombe kama sadaka ya dhambi kwaajili yake mwenyewe.
12 Atachukua chetezo kilichojaa makaa yanayowaka kutoka madhabahuni mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba laini uliosagwa vizuri wenye harufu, na kuvipeleka nyuma ya pazia.
Haruni lazima achukue chetezo iliyojaa mkaa wa moto kutoka kwenye madhabahu mbele ya Yahwe, na mikono imejaa ubani mzuri, na kuleta vitu hivi ndani ya pazia.
13 Ataweka uvumba juu ya moto mbele za Bwana, na moshi wa uvumba utafunika kile kiti cha rehema kilicho juu ya Ushuhuda, ili asife.
Hapo lazima aweke ubani juu ya moto mbele za Yahwe ili kwamba wingu kutoka kwenye ubani liweze kufunika kifuniko cha agano la imani ya upatanisho. Yeye afanye hivyo ili kwamba asife.
14 Atachukua sehemu ya damu ya fahali, na kwa kidole chake atanyunyiza sehemu ya mbele ya kiti cha rehema; kisha atanyunyiza sehemu ya hiyo damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kiti cha rehema.
Ndipo lazima achukue kiasi cha damu ya ng'ombe na kuinyunyiza kwa kidole chake mbele ya kifuniko cha upatanisho. Lazima anyunyize kiasi cha damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kifuniko cha upatanisho.
15 “Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, na kuichukua damu yake nyuma ya pazia, na aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake.
Ndipo lazima aue mbuzi kwaajili ya sadaka ya dhambi ambayo ni kwaajili ya watu na kuileta damu yake ndani kwenye pazi. Hapo lazima aifanyie damu kama alivyofanya kwenye damu ya fahali: lazima ainyunyize juu ya kifuniko cha upatanisho na mbele ya kifunuko cha upatanisho.
16 Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zozote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania, ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao.
Yeye lazima afanye upatanisho kwaajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya matendo ya unajisi ya watu wa Israeli, na kwa sababu ya uasi na dhambi zao zote. Yeye pia lazima afanye haya kwaajili ya hema ya mkutano, ambapo Yahwe anaishi kati yao, katika uwepo wa matendo yao ya unajisi.
17 Mtu yeyote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania, kuanzia wakati Aroni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu, hadi atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe na nyumba yake, pamoja na jumuiya yote ya Israeli.
Hakuna mtu anayetakiwa kuwepo katika hema ya mkutano wakati Haruni anaingia kufanya upatanisho katika mahali patakatifu pa patakatifu, na mpaka atoke nje na amemaliza kufanya upatanisho kwaajili yake mwenyewe na kwaajili ya familia yake, na kwaajili umati wa Israeli.
18 “Kisha atatoka aje kwenye madhabahu yaliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi, na kuiweka kwenye pembe za madhabahu.
Yeye lazima aende nje kwenye madhabahu hapo mbele za Yahwe na kufanya upatanisho kwaajili ya hiyo, na lazima achukue kiasi cha damu ya mbuzi na kuiweka juu ya pembe za madhabahu yote kuzunguka.
19 Atanyunyiza baadhi ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.
Anatakiwa anyunyize kiasi cha damu juu yake kwa kidole chake mara saba kuitakasa na kuitenga maalumu kwa Yahwe, mbali kutoka matendo ya unajisi wa watu wa Israeli.
20 “Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai.
Atakapo maliza kupatanisha kwaajili ya mahali patakatifu sana, hema la mkutano, na madhabahu, lazima amlete mbuzi aliyehai.
21 Aroni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo.
Haruni lazima aweke mikono yake yote juu ya kichwa cha mbuzi huyu aliyehai na akiri juu yake maovu yote ya watu wa Israeli, uasi wao wote, dhambi zao zote. Ndipo lazima aweke dhambi hizo juu ya kichwa cha mbuzi na amwachie katika uangalizi wa mtu aliyetari kumwongoza mbuzi huyo porini.
22 Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani.
Mbuzi lazima abebe juu yake mwenyewe uovu wote kwenda mahali pakiwa. Kule msituni, huyo mtu amwache mbuzi aende huru.
23 “Kisha Aroni ataenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale.
Ndipo Haruni anapaswa kwenda tena humo kwenye hema ya mkutano na kuvua mavazi ya kitani ambayo amayavaa kabla hajaenda mahali patakatifu sana, na anatakiwa kuyaacha mavazi hayo pale.
24 Ataoga kwa maji katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Kisha atatoka na kutoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya watu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya watu.
Anapaswa aoshe mwili wake kwa maji mahali patakatifu, na avae nguo zake za kawaida; pia lazima atoke nje kutoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya kuteketezwa kwaajili ya wale watu, na kwa njia hii anafanya upatanisho kwaajili yake mwenyewe na kwaajili ya watu.
25 Pia atachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya dhambi juu ya madhabahu.
Lazima yeye achome mafuta ya sadaka ya dhambi juu ya madhabahu.
26 “Yule mtu anayemwachia yule mbuzi wa kubebeshwa dhambi ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji; baadaye anaweza kuingia kambini.
Huyu mtu anayemwacha mbuzi msingiziwa aende huru anafua nguo zake na kuosha mwili wake katika maji; baada ya hayo, anaweza kurudi tena kambini.
27 Yule fahali na mbuzi waliotolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi, ambao damu yao ilikuwa imeletwa Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kufanya upatanisho, ni lazima watolewe nje ya kambi. Ngozi zao, nyama, na matumbo pamoja na mavi vitateketezwa kwa moto.
Yule fahali kwaajili ya sadaka ya dhambi na mbuzi kwaajili ya sadaka za dhambi, ambaye damu yake ililetwa kufanya upatanisho katika mahali patakatifu, lazima ipelekwe nje ya kambi. kule lazima wachome, ngozi zao, nyama yao na kinyesi chao.
28 Mtu atakayevichoma ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji; baadaye ataweza kuingia kambini.
Huyu anayechoma sehemu hizo lazima afue nguo zake na aoge mwili wake katika maji; baada ya hapo, anaweza kurudi tena kwenye kambi.
29 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ni lazima mfunge, wala msifanye kazi yoyote, iwe mzawa au mgeni anayeishi miongoni mwenu,
Hii itakuwa sharti kwaajili yenu kwamba katika mwezi wa saba, kwenye siku ya kumi ya mwezi, mtanyenyekea wenyewe na msifanye kazi, iwe mwenyeji wa kuzaliwa au mgeni anayeishi kati yenu.
30 kwa sababu siku hii upatanisho utafanyika kwa ajili yenu ili kuwatakasa. Kisha mtakuwa safi mbele za Bwana kutokana na dhambi zenu zote.
Hii ni kwasababu katika siku hii ya upatanisho utafanywa kwaajili yenu, kuwatakasa ninyi kutoka dhambi zenu zote ili mwe safi mbele za Yahwe.
31 Ni Sabato ya mapumziko, na lazima mfunge; ni agizo la kudumu.
Hii ni maalumu kwa Sabato ya kupumzika kwaajili yenu, na lazima mnyenyekee wenyewe na msifanye kazi. Hili litakuwa sharti kati yenu.
32 Kuhani ambaye ametiwa mafuta na kuwekwa wakfu ili kuingia mahali pa baba yake kama kuhani mkuu atafanya upatanisho. Atavaa mavazi matakatifu ya kitani,
Kuhani mkuu, ambaye atapakwa mafuta na kuwekwa wakfu kuwa kuhani mkuu katika nafasi ya baba yake, lazima afanye upatanisho huu na kuvaa mavazi ya kitani, hayo ni mavazi matakatifu.
33 na kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, na pia kwa ajili ya makuhani, pamoja na jumuiya yote ya watu.
Lazima afanye upatanisho kwaajili ya mahali patakatifu sana; lazima afanye upatanisho kwaajili ya hema ya mkutano na madhabahu, na lazima afanye upatanisho kwaajili ya makuhani na kwaajili ya kusanyiko la watu.
34 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Upatanisho utafanywa mara moja tu kwa mwaka kwa ajili ya dhambi zote za Waisraeli.” Ndivyo ilivyofanyika, kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
Hii daima itakuwa sharti kwaajili yako, kufanya upatanisho kwaajili ya watu wa Israeli kwasababu ya dhambi zao zote, mara moja kwa kila mwaka.” Na ilikuwa ikifanika kama Yahwe alivyomwamuru Musa.

< Mambo ya Walawi 16 >