< Mambo ya Walawi 13 >

1 Bwana akawaambia Mose na Aroni,
Yahweh akazungumza na Musa na Aroni, akasema,
2 “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au alama nyeupe juu ya ngozi yake ambayo yaweza kuwa ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa Aroni kuhani ama kwa wanawe, kuhani mmojawapo.
Mtu yeyote anayeonekana na uvimbe au pele au doa ling'aalo juu ya ngozi ya mwili wake, na likawa limeambukizwa ugonjwa wa ngozi mwilini mwake, ni lazima aletwe kwa Aroni kuhani mkuu au kwa mmoja wa wanawe makuhani.
3 Kuhani atachunguza hicho kidonda kilichopo juu ya ngozi yake, na kama nywele za mahali palipo na kidonda zimebadilika kuwa nyeupe, na ikiwa kidonda kimeingia ndani ya ngozi, basi ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma. Kuhani atakapomchunguza, atamtangaza mtu huyo kuwa ni najisi kwa kawaida ya ibada.
Naye kuhanai atachunguza ugonjwa huo kwenye ngozi ya mwili wake. Iwapo malaika zilizopo eneo lenye ugonjwa zimegeuka kuwa nyeupe, na iwapo ugonjwa umejitokeza juu ya ngozi, huo ni ugonjwa wa kuambukiza. Baada cha kuhani kumchunguza, atamtangaza kuwa ni najisi.
4 Kama alama juu ya ngozi yake ni nyeupe, lakini haionekani kuwa imeingia ndani zaidi ya ngozi, na nywele kwenye alama hiyo hazijageuka kuwa nyeupe, kuhani atamtenga mtu huyo mahali pa pekee kwa siku saba.
Iwapo lile doa ling'aalo katika ngozi yake ni jeupe, na kuonekana kwake halikwenda chini zaidi ya ngozi, na iwapo malaika za eneo lenye ugonjwa hazijabadilika kuwa nyeupe, naye kuhani atamtenga mgonjwa kwa siku saba.
5 Siku ya saba, kuhani atamchunguza, na kama hakuona badiliko kwenye kile kidonda na hakijaenea juu ya ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba.
Katika siku ya saba, huyo kuhani itambidi kumchunguza tena ili kuona kama katika maamzi yake huo ugonjwa siyo mbaya, na kama haujaenea kwenye ngozi. Iwapo haujaenea, basi, kuhani atamtenga kwa siku saba zaidi.
6 Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama kidonda kimepungua na hakijaenea juu ya ngozi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa ni safi, ni upele tu. Ni lazima mtu huyo afue mavazi yake, naye atakuwa safi.
Naye kuhani atamchunga tena katika siku ya saba ili kuona kama ugonjwa ubepona na haujasambaa zaidi kwenye ngozi. kama haujasambaa, basi, kuhani atamtangaza kuwa yeye ni safi. Ni upele tu. Naye atafua nguo zake, na kisha yeye yu safi.
7 Lakini ikiwa ule upele utaenea juu ya ngozi yake baada ya yeye kujionyesha kwa kuhani na kutangazwa kuwa safi, ni lazima aende tena kwa kuhani.
Lakini endapo ule upele utakuwa umishasambaa kwenye ngozi baada ya kuwa amejionyesha kwa kuhani kwa ajili kusafishwa kwake, itambidi kujionyesha tena kwa kuhani.
8 Kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, atamtangaza kuwa najisi, kwani ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma.
Naye kuhani atamchunguza ilikuona kama huo upele umsambaa zaidi ndani ya ngozi. Na endapo utakuwa umesambaa, kisha kuhani atamtangaza kuwa najisi. Huo ni ugonjwa wa kuambukiza.
9 “Wakati mtu yeyote ana ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani.
Iwapo ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza umo kwa mtu fulani, naye mtu huyo yapasa aletwe kwa kuhan.
10 Kuhani atamchunguza na kama kuna uvimbe mweupe juu ya ngozi ambao umefanya nywele kuwa nyeupe, na kama kuna nyama mbichi ndani ya uvimbe,
Kuhani atamchunguza ili kuona kama kunauvimbe mweupe katika ngozi yake, endapo malaika zitakuwa zimebadilika kuwa nyeupe, au kumekuwa na nyama mbichi kwenye uvimbe.
11 ni ugonjwa sugu wa ngozi, na kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga tena kwa sababu ni najisi tayari.
Kama ipo, basi, huo ni ugonjwa sugu wa ngozi, naye kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga kwa kuwa yeye tayari ni najisi.
12 “Ikiwa ugonjwa utakuwa umeenea kwenye ngozi yake yote kwa kadiri kuhani atakavyoweza kuona, kwamba umeenea kwenye ngozi yote ya huyo mgonjwa kutoka kichwani mpaka wayo,
Iwapo huo ugonjwa unajitokeza na kupanuka zaidi kwenye ngozi, na kuifunika ngozi ya mtu kwa ugonjwa tangu kichwani pake hata miguuni, maadamu anajitokeza kwa kuhani,
13 kuhani atamchunguza, na kama ugonjwa umeenea mwili mzima, atamtangaza huyo mtu kuwa safi. Kwa kuwa mwili wote umekuwa mweupe, yeye ni safi.
naye kuhani atamchunguza ili kuona kama huo ugonjwa umeshaenea mwili wake wote. Ikiwa imetokeo hivyo, kuhani atamtangaza mtu huyo aliye na ugonjwa kuwa ni safi. Ikiwa amebadilika kuwa mweupe, huyo ni safi.
14 Lakini itokeapo nyama mbichi kwenye ngozi yake, atakuwa najisi.
Lakini ikiwa nyama mbichi imeonekana juu yake, atakuwa najisi.
15 Kuhani atakapoiona hiyo nyama mbichi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hiyo nyama mbichi ni najisi, ana ugonjwa wa kuambukiza.
Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi na kumtanga kuwa najisi kwa sababu hiyo nyama mbichi ni najisi. Huo ni ugonjwa wa kuambukiza.
16 Hiyo nyama mbichi ikigeuka na kuwa nyeupe, ni lazima amwendee kuhani.
Lakini endapo hiyo nyama mbichi inageuka kuwa nyeupe tena, naye huyo mtu hana budi kwenda kwa kuhani.
17 Kuhani atamchunguza, na kama vidonda vimekuwa vyeupe, kuhani atamtangaza mgonjwa huyo kuwa safi; kisha atakuwa safi.
Kuhani atamchunguza ili kuona kama hiyo nyama imebadilika kuwa nyeupe. Kama imekuwa hivyo naye kuhani atatangaza kwamba mtu huyo kuwa ni safi.
18 “Wakati mtu ana jipu juu ya ngozi yake nalo likapona,
Mtu anapokuwa na jipu juu yangozi yake na limishapona,
19 napo mahali palipokuwa na jipu pakatokea uvimbe mweupe, au alama yenye wekundu na weupe, ni lazima akajionyeshe kwa kuhani.
na mahali pa jipu pamekuwa na uvimbe au doa lenye kung'aa, wekundu unaochanganyikana na weupe, yapasa kuonyeshwa kwa kuhani.
20 Kuhani atapachunguza, na kama uvimbe umezama ndani ya ngozi, na nywele zimegeuka kuwa nyeupe, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza uliojitokeza pale jipu lilipokuwa.
Naye kuhani atalichunguza ili kuona kama linaonekana limekwenda chini ya ngozi, na kama hizo malaika zimebadilika kuwa nyeupe, kama ni hivyo, kuhani atamtangaza kuwa najisi. Huo ni ugonjwa wa kuambukiza, endapo utakuwa umezalishwa mahali lilipokuwa jipu hilo.
21 Lakini ikiwa wakati kuhani anapopachunguza pakawa hapana nywele nyeupe ndani yake, wala hakuna shimo bali pamepungua, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
Lakini endapo kuhani atakuwa amelichunguza na haoni malaika nyeupe ndani yake, na kwamba iliko chini ya ngozi bali limefifia, kisha kuhani atamtenga kwa siku saba.
22 Kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
Kama linaenea kwa kupanuka kwenye ngozi, kisha kuhani atamtangaza kuwa najisi. Huo ni ugonjwa wa kuambukiza.
23 Lakini ikiwa ile alama haijabadilika wala kuenea, ni kovu tu kutokana na jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi.
Lakini kama hilo doa lenye kung'ara linabaki mahali pake na halijasambaa, basi hilo ni kovu la jipu, naye kuhani atamtangaza kuwa safi.
24 “Wakati mtu ameungua kwenye ngozi yake, pakatokea alama yenye wekundu na weupe, au alama nyeupe ikaonekana penye nyama mbichi pale palipoungua,
Ngozi inapoungua na nyama mbichi ya inamekuwa na wekundu uliochanganyika na weupe au doa jeupe,
25 kuhani ataichunguza ile alama, na kama nywele zilizoko juu yake zimegeuka kuwa nyeupe, napo pametokea shimo, basi huo ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza ambao umetokea juu ya jeraha la moto. Kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
kisha kuhani ataichunguza kuona kama malaika zilizoko kwenye doa hilo zimebadilika na kuwa nyeupe, na kama limeonekana kwenda chini zaidi ya ngozi, kama limekuwa hivyo, basi huo ni ugonjwa wa kuambukiza. Umejitokeza kwenye jeraha la moto, naye kuhani atamtangaza kuwa najisi. Huo ni ugonjwa wa kuambukiza.
26 Lakini kama kuhani akichunguza na kuona kwamba hakuna nywele nyeupe kwenye alama ile, wala hakuna shimo napo pameanza kupungua, basi kuhani atamtenga kwa siku saba.
Lakini endapo kuahani analichunguza na naona kwamba hakuna malaika nyeupe kwenye doa, na kwamba halikuenda chini ya ngozi bali linafifia, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
27 Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
Kisha yapasa kuahani kumchunguza tena katika siku ya saba. Iwapo litakuwa limesambaa kwa upana kwenye ngozi, naye kuhani atamtangaza kuwa najisi. Huo ni ugojwa wa kuambukiza.
28 Lakini, kama alama ile haikubadilika na wala haijaenea kwenye ngozi, napo pamepungua, ni uvimbe kutokana na jeraha la moto, na kuhani atamtangaza kuwa safi; ni kovu tu kutokana na kuungua.
Iwapo hilo doa lisalia mahali pake na halitakuwa limesambaa kwenye ngozi bali limefifia, ni uvimbe tu kutokana na kuungua moto, naye kuhani atamtangaza kuwa safi, kwa kuwa siyo zaidi ya jeraha la kuungua.
29 “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana kidonda juu ya kichwa au juu ya kidevu,
Iwapo mwanaume au mwanamke ana ugonjwa wa kuambukiza kichwani au kidevuni pake,
30 kuhani atakichunguza kile kidonda, na kama ataona kuwa kimeingia ndani, na nywele zilizoko juu yake ni njano na nyembamba, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi, kwani ni upele; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza wa kichwa au kidevu.
kisha kuhani atamchunguza mtu huyo kwa ajili ya ugonjwa wa kuambukiza ili kuona kama unakwenda ndani zaidi ya ngozi, na kama kuna nywele za manjano, nyembamba ndani yake. endapo zinaonekana, kisha kuhani atamtangaza kuwa najisi. Huo ni mwasho, ugonjwa wa kuambukiza kichwani au kidevuni.
31 Lakini kama kuhani akichunguza aina hii ya kidonda, kionekane kuwa hakina shimo na hakuna nywele nyeusi juu yake, basi atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
Iwapo kuhani anachunguza ugonjwa wa mwasho na anagundu kuwa hauko chini ya ngozi, na kama hakuna nywele nyeusi ndani yake, kisha kuhani atamtenga mtu huyo mwenye ugonjwa wa mwasho kwa siku saba.
32 Siku ya saba kuhani atachunguza kidonda kile, na kama upele haujaenea, na hakuna nywele za manjano juu yake, wala hakuna shimo lolote,
Katika siku ya saba kuhani atauchunguza tena huo ugonjwa ili kuona kama umesambaa, Endapo hakuna malaika za manjano, na iwapo ugonjwa uko usawa ngozi tu,
33 mtu huyo ni lazima anyolewe, isipokuwa mahali palipo na ugonjwa, naye kuhani atamtenga kwa siku nyingine saba.
basi, yapasa mtu huyo kunyolewa., lakini sehemu yenye ugonjwa haitanyolewa, naye kuhani atamtenga mtu huyo mwenye ugonjwa wa mwasho kwa siku saba.
34 Siku ya saba kuhani atachunguza tena ule upele; ikiwa haujaenea kwenye ngozi na hakuna shimo mahali pale, kuhani atamtangaza kuwa safi. Lazima afue nguo zake, naye atakuwa safi.
Katika siku ya saba kuhani atauchunguza tena ugonjwa ili kuona kama umacha kusambaa ndani ya ngozi. Iwapo unaonekana kuwa hukwenda chini zaidi ya ngozi, kisha kuhani atamtangaza kuwa safi. Mtu huyo yapasa kufua nguo zake, na kisha atakuwa safi.
35 Lakini ikiwa upele utaenea juu ya ngozi baada ya kutangazwa kuwa safi,
Lakini ikiwa ugonjwa wa mwasho umeenea kwa sehemu kubwa kwenye ngozi baada ya kuhani kutangaza kuwa alikuwa safi,
36 kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, kuhani hana haja ya kutazama kama kuna nywele za manjano, mtu huyo ni najisi.
naye kuhani itabidi amchunguze tena. Iwapo ugonjwa utakuwa umesambaa katika ngozi, kuhani hahitajiki kutafuta nywele za manjano. Mtu huyo ni najisi.
37 Hata hivyo, katika uchunguzi wake akiona hapajabadilika, na nywele nyeusi zimeota juu yake, upele umepona. Yeye si najisi, kuhani atamtangaza kuwa safi.
Lakini iwapo katika mtazamo wa kuhani inaonekana kuwa huo ugonjwa wa mwasho umekoma kusambaa, basi huo ugonjwa umekwisha pona. Yeye ni safi, naye kuhani atamtangaza kuwa safi.
38 “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana alama nyeupe juu ya ngozi yake,
Iwapo mwanume au mwanamke ana madoa juu ya ngozi,
39 kuhani atamchunguza, na kama alama hizo zina weupe uliofifia, ni vipele visivyo na madhara vilivyojitokeza kwenye ngozi; mtu huyo ni safi.
kisha kuhani atamchunguza mtu huyo ili kuona kama hayo madoa ni meupe kwa kufiifia, ambalo ni kovu tu lililojitokeza kwenye ngozi. Yeye yu safi.
40 “Wakati mwanaume hana nywele naye ana upaa, yeye ni safi.
Iwapo nywele za mtu zimenyonyoka kichwani, yeye ni kipara lakini yu safi.
41 Ikiwa hana nywele kwenye ngozi ya kichwa chake, na ana upaa tangu kwenye paji, ni safi.
Na iwapo nywele zake zimenyonyoka upande wa mbele wa kichwa chake, na iwapo paji lake la uso lina kipara, yeye yu safi.
42 Lakini kama ana kidonda chenye wekundu na weupe kwenye kichwa chake chenye upaa, au kwenye paji la uso, ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza unaojitokeza kichwani au kwenye paji lake la uso.
Lakini endapo kuna kidonda chenye wekundu uliochanganyika na weupe, juu ya kipara chake au paji lake la uso, huo ni ugonjwa wa kuambukiza uliojitokeza.
43 Kuhani atamchunguza, na kama kidonda kilichovimba juu ya kichwa chake au kwenye paji la uso ni chekundu au cheupe kama ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza,
Naye kuhani atamchunguza ili kuona iwapo uvimbe wa eneo linaugua juu ya upara wake au paji lake la uso lina wekundu uliochanganyika na weupe, kama kuonekana kwa ugonjwa wa kuambukiza kwenye ngozi.
44 mtu huyo ni mgonjwa, na ni najisi. Kuhani atamtangaza kuwa najisi kwa sababu ya kidonda kwenye kichwa chake.
Ikionekana hivyo, basi huyo ana ugonjwa wa kuambukiza naye ni najisi. Hakika kuhani atamtangaza kuwa najisi kwa sababu ya ugonjwa wake kichwani pake.
45 “Mtu mwenye ugonjwa kama huo wa kuambukiza ni lazima avae nguo zilizoraruka, awachilie nywele zake bila kuzichana, afunike sehemu ya chini ya uso wake, na apige kelele, ‘Najisi! Najisi!’
Mtu aliye na ugojwa wa kuambukiza atavaa nguo zilizochanika, ni lazima nywele zake ziachwe wazi, na yampasa kufunika uso wake mpaka puani na kupiga kelele, 'Najisi, najisi.'
46 Kwa muda wote atakaokuwa na ugonjwa huo wa kuambukiza atabaki kuwa najisi. Ni lazima aishi peke yake; ni lazima aishi nje ya kambi.
Naye atakuwa najisi siku zote za ugonjwa wake wa kuambukiza. Kwa sababu anao ugonjwa unaosambaa, yapasa kuishi peke yake nje ya kambi.
47 “Kama vazi lolote lina maambukizo ya upele: likiwa ni vazi la sufu au kitani,
Kuna wakati fulani vazi la mtu hupata ukungu juu yake. Laweza kuwa vazi, ama la sufu au kitani,
48 lolote lililofumwa au kusokotwa likiwa la kitani au la sufu, ngozi yoyote au chochote kilichotengenezwa kwa ngozi,
au kitu chochote kilichosukwa au kufumwa kutokana na sufu au kitani, au ngozi au kitu chochote kilichotengenezwa kwa ngozi.
49 tena kama maambukizo kwenye vazi, au ngozi, au lililofumwa au kusokotwa, au kifaa chochote cha ngozi, ni rangi ya kijani au nyekundu, huo ni upele unaoenea na ni lazima kuhani aonyeshwe.
Iwapo sehemu iliyochafuliwa ina rangi ya kijani au nyekundu katika vazi, ngozi, kifaa kilichosukwa au kufumwa, basi huo ni ukungu uanasambaa, ni lazima uonyeshwe kwa kuhani.
50 Kuhani atachunguza upele huo na kukitenga kifaa hicho kwa siku saba.
Yapasa kuhani akichunguze hicho kifaa kwa ajili ya ukungu; ni lazima akitenge kitu chochote kilicho na ukungu kwa siku saba.
51 Siku ya saba atakichunguza, na kama upele umeenea kwenye nguo, au kifaa kilichofumwa au kusokotwa, au ngozi, kwa vyovyote vile itumikavyo, ni upele uangamizao, kifaa hicho ni najisi.
Naye atauchunguza tena huo ukungu katika siku ya saba. Endapo utakuwa umesambaa katika kifaa hicho, basi ni wazi kwamba huo ni ukungu wenye kuangamiza, na hicho kifaa ni najisi.
52 Ni lazima aichome hiyo nguo, ikiwa ni ya sufu ama kitani iliyofumwa ama kusokotwa, ama chombo chochote cha ngozi chenye maambukizo, kwa kuwa ni upele unaoangamiza; chombo chote ni lazima kichomwe moto.
Na mwenye kukimiliki atalazimika kukichoma na kukiteketeza kabisa hicho kifaa kilichoonekana na ukungu ndani yake, haijalishi kiwe ni kifaa cha aina gani, kwani huo ukungu unaweza kusababisha ugonjwa.
53 “Lakini wakati kuhani atakapokichunguza na kuona kuwa ule upele haujaenea kwenye nguo iliyofumwa au kusokotwa, au vifaa vya ngozi,
Iwapo kuhani anakichunguza hicho kifaa na kuona kwamba ukungu haujaenea kwenye vazi au chombo kilichosukwa au kusokotwa kutokana na sufu, kitani au ngozi,
54 ataagiza kwamba kifaa chenye maambukizo kisafishwe. Kisha atakitenga kwa siku saba.
basi atawaagiza wakisafishe hicho kifaa kilichopatikana na ukungu, naye yampasa kukitenga kwa siku saba zaidi.
55 Baada ya kifaa chenye maambukizo kusafishwa, kuhani atakichunguza, na kama upele haujaonyesha badiliko lolote, hata kama haujaenea, ni najisi. Kichome kwa moto, iwe upele umeenea upande mmoja au mwingine.
Kisha kuhani atakichunguza tena hicho kifaa chenye ukungu baada ya kuwa kimesafinshwa. Kama ukungu haukubadilika rangi yake, hata kama haukusambaa, kifaa hicho ni najisi. Yapasa kichomwe, haijalishi ni wapi ukungu huo utakuwa umekichafua.
56 Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kuoshwa, basi atararua sehemu iliyo ambukizwa ya nguo au ngozi au kifaa kilichofumwa au kusokotwa.
Iwapo kuhani anakichunguza hicho kifaa, na kama ukungu umefifia baada ya kuwa umeoshwa, basi atakirarua kile kipande kilichochaufuliwa kutoka kwenye vazi au kutoka kwenye ngozi, au kutoka kwenye chombo kilichosukwa au kusokotwa.
57 Lakini kama ikijitokeza tena kwenye nguo au kitu kilichofumwa au kusokotwa, ama kifaa cha ngozi, kwamba ule upele unaenea, chochote chenye upele ni lazima kichomwe kwa moto.
Ikiwa ukungu unazidi kuonekana katika vazi, ama katika chombo kilichosukwa au kufumwa, au katika kitu chochote kilichotengenezwa kwa ngozi, basi, ukungu utakuwa unasambaa. Kifaa chochote kilicho na ukungu ni lazima kichomwe.
58 Nguo, au kitu kilichofumwa au kusokotwa, au kifaa chochote cha ngozi ambacho kimesafishwa na kuondolewa upele, ni lazima kioshwe tena, nacho kitakuwa safi.”
Vazi au kitu chochote kilichosukwa au kufumwa kutokana na sufu, au kitani, au ngozi au kitu chochote kilichotengenezwa kwa ngozi—iwapo unakisafisha kifaa nao ukungu ukawa umetoka, nacho kifaa lazima kisafishwe mara ya pili, kisha kitakuwa safi.
59 Haya ni masharti kuhusu maambukizo ya upele kwenye mavazi ya sufu au kitani, yaliyofumwa ama kusokotwa, ama kifaa chochote cha ngozi, kwa ajili ya kuvitangaza kuwa safi au najisi.
Hii ndiyo sheria ihusuyo ukungu katika vazi la sufu au kitani, au kwenye kitu chochote kilichosukwa au kufumwa kutokana na sufu, au kitani, au kitu chochote kilichotengenewa kwa ngozi, ili kwamba mweze kuvitangaza kuwa safi au najisi.

< Mambo ya Walawi 13 >