< Mambo ya Walawi 10 >
1 Nadabu na Abihu, wana wa Aroni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea Bwana moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu.
Nadabu na Abihu, wana wa Aroni, wakachukua kila mtu kifukizo chake, akaweka moto ndani yake, na kisha uvumba. Kisha wakatoa moto usiokuabalika mbele za Yahweh, moto ambao hakuwaamru wao kuutoa.
2 Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Bwana na kuwaramba, nao wakafa mbele za Bwana.
Kwa hiyo moto ukashuka chini mbele za Yahweh na kuwala, nao wakafa mbele za Yahweh.
3 Kisha Mose akamwambia Aroni, “Hili ndilo alilonena Bwana wakati aliposema: “‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia nitajionyesha kuwa mtakatifu; machoni pa watu wote nitaheshimiwa.’” Aroni akanyamaza.
Kisha Musa akamwambia Aroni, Hivi ndiyo Yahweh alivyokuwa akizunguzia aliposema, 'Nitaufunua utakatifu wangu kwa wale wajao mbele zangu. Nami nitatukuzwa mbele za watu wote.'” Naye Aroni hakusema neno lolote.
4 Mose akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Aroni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya binamu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.”
Musa akamwita Mishaeli na Elzafani, wana wa Uzieli mjomba wa Aroni, naye akamwambia, “njoo huku na uwatowe ndugu zako nje ya kambi watoke mbele ya hema.”
5 Hivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Mose alivyoamuru.
Hivyo wakakaribia na kuwachukua wangali wamevaa kanzu zao za kikuhani, nao wakawapeleka nje ya kambi, kama Musa alivyokuwa ameelekeza. Kisha Musa akamwambia Aroni na wanawe wengine wawili, Eliezari na Ithamari, “
6 Ndipo Mose akamwambia Aroni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na Bwana ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao Bwana amewaangamiza kwa moto.
Msiache wazi nywele za vichwa vyenu, wala msirarue nguo zenu, ili kwamba msije mkafa, na kwamba Yahweh asilikasirikie kusanyiko zima. Lakini waacheni jamaa zenu, nyumba yote ya Israeli waweze kufanya ibada za maombolezo kwa ajili ya hao ambao Yahweh amewaangamiza kwa moto.
7 Msitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya Bwana ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Mose alivyosema.
Msiende nje kutoka kwenye ingilio la hema la kukutania, ama sivyo mtakufa, kwa kuwa mafuta ya Yahweh ya upako yako juu yenu.” Kwa hiyo wakatenda sawasawa na maelekezo ya Musa.
8 Kisha Bwana akamwambia Aroni,
Mungu akazungumza na Aroni, akisema,
9 “Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa Agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo.
“Msinywe mvinyo wala kinywaji kikali, wewe, au wanao wanaobaki pamoja nawe, ili kwamba mtakapoingia kwenye hema ya kukutania msije mkafa. Hii itakuwa amri ya kudumu katika vizazi vyote vya watu wenu,
10 Ni lazima mtenganishe kilicho kitakatifu na kile kilicho cha kawaida, kati ya yaliyo najisi na yaliyo safi,
ili kupaambanua kati ya mambo matakatifu na mambo ya kawaida, na kati ya najisi na safi,
11 na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo Bwana aliwapa kupitia Mose.”
ili kwamba mweze kuwafundisha watu wa Israeli amri zote ambazo Yahweh ameziamru kwa kinywa cha Musa.
12 Mose akamwambia Aroni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana.
Musa akazungumza na Aroni na wanawe wawili waliosalia; Eliazari naIthamari, Twaeni sadaka ya nafaka inayobaki kutokana na sadaka ifanywayo kwa Yahweh kwa moto, nanyi ileni kando ya madhabahu bila hamiara, kwa kuwa ni takatifu sana.
13 Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa Bwana kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa.
lazima mtaila mahali patatifu kwa sababu huo ni mgao wako wewe na mgao wa wanao wa matoleo yaliyofanywa kwa Yahweh kwa moto, kwa kuwa hivi ndivyo limeamriwa niwaambie.
14 Lakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila mahali safi pa kawaida ya ibada; mmepewa wewe na watoto wako kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli.
Kile kidari kitikiswacho na lile paja ambalo hutolewa kwa Yahweh, yapasa mzile mahali palipo safi panapokubalika kwa Mungu. Wewe mwenyewe, wanao na binti zako waliopamoja nawe mtakula sehemu hizo, kwa kuwa zimetolewa kuwa mgao wako na mgao wa wanao kutokana na dhabihu ya sadaka ya ushirika wa watu wa Israeli.
15 Paja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za Bwana kama sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako la kawaida na wanao, kama Bwana alivyoagiza.”
Lile paja lililotolewa na kidari kilichotikiswa, ni lazima ziletwe pamoja na sadaka ya mafuta iliyofanywa kwa moto, ili kutikiswa mbele za Yahweh. Nazo zitakuwa zako wewe na wanao kuwa mgao wenu daima, kama Yahweh alivyoamru.
16 Mose alipouliza kuhusu mbuzi atolewaye kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kukuta kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliobaki, akawauliza,
Kisha Musa akauliza kuhusu yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye akagundua kwamba alikuwa ametekezwa kwa moto. Kwa hiyo akawakasirikia Eliazari na Ithamari, wana wa Aroni waliosalia; akawaambia,
17 “Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za Bwana.
“Kwa nini hamjaila sadaka ya dhambi katika eneo la hema, kwa kuwa ni takatifu sana, na kwa kuwa Yahweh amishaitoa kwenu ili kuchukua uovu wa kusanyiko, ili kufanya upatanisho kwa aijli yao mbele zake?
18 Kwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.”
Tazama, damu yake haikuletwa ndani ya hema, kwa hiyo iliwapasa kwa hakika kuwa mekwisha ila kwenye eneo la hema, kama nilivyoagiza?
19 Aroni akamjibu Mose, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za Bwana, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, Bwana angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?”
Kisha Aroni akamjibu Musa, “Tazama, leo walitoa sadaka yao ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa mbele za Yahweh, na jambo hili vilevile limetendeka kwangu leo. Ikiwa nimeshakula sadaka ya dhambi leo, Je! Isingekuwa imeshapendeza mbele za Yahweh?”
20 Mose aliposikia haya, akaridhika.
Naye Musa aliposikia hivyo, akaridhika.