< Waamuzi 1 >

1 Baada ya kifo cha Yoshua, Waisraeli wakamuuliza Bwana, “Ni nani atakayetangulia kupanda mbele yetu kwa ajili ya kupigana na Wakanaani?”
Baada ya kifo cha Yoshua, wana wa Israeli walimuuliza Yahweh wakisema, “Ni nani atawashambulia kwanza Wakanaani kwa ajili yetu, ili kupigana nao?
2 Bwana akajibu, “Yuda ndiye atakayetangulia; nimewapa hiyo nchi mikononi mwao.”
Yahweh akasema, “Yuda atawashambulia. Tazama, nimewapa kumiliki nchi hii.
3 Ndipo watu wa Yuda wakawaambia Wasimeoni ndugu zao, “Pandeni pamoja nasi katika nchi tuliyopewa, ili tupate kupigana na Wakanaani. Sisi pia tutakwenda pamoja nanyi katika sehemu yenu mliyopewa.” Basi Wasimeoni wakaenda pamoja nao.
Watu wa Yuda wakawaambia wana wa Simeoni, ndugu zao, “Njoo pamoja nasi katika eneo letu ambalo tumepewa ili kwa pamoja tupigane na Wakanaani. Na sisi pia tutakwenda nanyi katika eneo mlilopewa.” Basi kabila la Simeoni wakaenda pamoja nao.
4 Yuda aliposhambulia, Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, nao wakawaua watu 10,000 huko Bezeki.
Watu wa Yuda wakashinda, na Bwana akawapa ushindi juu ya Wakanaani na Waperizi. Wakawaua watu elfu kumi huko Bezeki.
5 Huko ndiko walipomkuta huyo Adoni-Bezeki, nao wakapigana naye na kuwafanya Wakanaani na Waperizi wakimbie.
Wakamkuta Adoni Bezeki huko Bezeki, nao wakapigana naye na kuwashinda Wakanaani na Waperizi.
6 Adoni-Bezeki pia alikimbia, nao wakamfuata na kumkamata, wakamkata vidole vyake gumba vya mikono na vya miguu.
Lakini Adoni Bezeki akamkimbilia, wakamfuata na kumshika, nao wakavikata vidole gumba na vidole vyake vikubwa.
7 Ndipo Adoni-Bezeki akasema, “Nimewatendea wafalme sabini kama nilivyotendewa na kuwalisha makombo ya chakula chini ya meza yangu. Sasa Mungu amenilipa haya, kama yale niliyowatendea.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.
Adoni Bezek akasema, “Wafalme sabini, ambao na vidole gumba vyako na vidole vikubwa vilivyokatwa, walikusanya chakula chao chini ya meza yangu. Kama nilivyofanya, hata hivyo Mungu amefanya kwangu.” Wakamleta Yerusalemu, naye akafa huko.
8 Watu wa Yuda wakashambulia pia Yerusalemu na kuiteka. Wakaupiga mji kwa upanga na kuuchoma kwa moto.
Watu wa Yuda wakapigana dhidi ya jiji la Yerusalemu na kulichukua. Walishambulia kwa makali ya upanga na wakauwasha mji kwa moto.
9 Baada ya hayo, watu wa Yuda wakateremka kupigana na Wakanaani walioishi katika nchi ya vilima, yaani, Negebu na nchi chini ya vilima vya magharibi.
Baada ya hayo, watu wa Yuda walikwenda kupigana na Wakanaani waliokaa mlimani, Negebu, na magharibi mwa milima.
10 Yuda wakakabiliana na Wakanaani walioishi Hebroni (ambayo hapo kwanza iliitwa Kiriath-Arba) na kuwashinda Sheshai, Ahimani na Talmai.
Yuda akaenda dhidi ya Wakanaani waliokaa Hebroni (jina la Hebroni hapo awali ilikuwa Kiriath-arba), nao wakamshinda Sheshai, Ahimani na Talmai.
11 Kutoka huko wakasonga mbele kukabiliana na watu walioishi Debiri (ambao hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi.)
Kutoka huko watu wa Yuda walipigana na wenyeji wa Debiri (jina la Debiri hapo awali ilikuwa Kiriath-seferi).
12 Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.”
Kalebu akasema, Yeyote atakayeivamia Kiriath-seferi na kuichukua, nitampa Aksa, binti yangu, awe mkewe.
13 Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, akawashinda, kwa hiyo Kalebu akamtoa binti yake Aksa akaolewa naye.
Otinieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu, akaiteka Debiri, naye Kalebu akampa Aksa, binti yake, awe mkewe.
14 Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”
Ndipo Aksa alifika kwa Othnieli, naye akamsihi amuombe baba yake ampe shamba. Alipokuwa akishuka katika punda wake, Kalebu akamwuliza, “Nikufanyie nini?”
15 Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Ndipo Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.
Akamwambia, Nibariki. Kwa kuwa umenipa nchi ya Negebu, nipe pia chemchemi za maji. Kwa hiyo Kalebu akampa chemchemi za juu na chemchemi za chini.
16 Wazao wa yule Mkeni, baba mkwe wa Mose, wakapanda pamoja na watu wa Yuda kutoka Mji wa Mitende, wakaenda kuishi miongoni mwa watu wa jangwa ya Yuda huko Negebu karibu na mji wa Aradi.
Kizazi cha Mkeeni shemeji yake na Musa, walikwenda kutoka mji wa Mitende pamoja na watu wa Yuda, mpaka jangwa la Yuda, ambalo liko Negevu, kuishi na watu wa Yuda karibu na Arad.
17 Basi watu wa Yuda wakaenda na Wasimeoni ndugu zao kushambulia Wakanaani waishio Sefathi, nao wakauangamiza huo mji kabisa. Kwa hiyo huo mji ukaitwa Horma
Nao watu wa Yuda wakaenda pamoja na wana wa Simeoni ndugu zao, wakawaangamiza Wakanaani waliokaa Zefathi, wakaiharibu kabisa. Mji uliitwa Horma.
18 Watu wa Yuda wakatwaa pia Gaza, Ashkeloni na Ekroni, kila mji na vijiji vyake vinavyouzunguka.
Watu wa Yuda pia waliiteka Gaza na nchi iliyoizunguka, Ashkeloni na nchi iliyoizunguka, na Ekron na nchi iliyoizunguka.
19 Bwana alikuwa pamoja na watu wa Yuda. Wakaimiliki nchi ya vilima, lakini hawakuweza kuwafukuza watu waliokaa katika hiyo tambarare, kwa sababu walikuwa na magari ya chuma.
Yahweh alikuwa pamoja na watu wa Yuda na wakaimiliki nchi ya milima, lakini hawakuweza kuwatoa wenyeji wa kwenye bonde kwa sababu walikuwa na magari ya chuma.
20 Kama vile Mose alivyoahidi, Kalebu alipewa Hebroni, naye akawafukuza wana watatu wa Anaki.
Hebroni alipewa Kalebu (kama Musa alivyosema), naye akawafukuza kutoka huko wana watatu wa Anaki.
21 Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wanaishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.
Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa Yerusalemu. Basi Wayebusi wakakaa na watu wa Benyamini huko Yerusalemu hata leo.
22 Basi nyumba ya Yosefu wakashambulia Betheli, naye Bwana alikuwa pamoja nao.
Nyumba ya Yusufu ilijiandaa kuishambulia Betheli, na Yahweh alikuwa pamoja nao.
23 Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo kwanza uliitwa Luzu),
Walipeleka watu kuipeleleza Betheli (jiji lililoitwa Luzu).
24 wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuonyeshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.”
Wapelelezi waliona mtu akitoka nje ya jiji, wakamwambia, “Tafadhali tuonyeshe jinsi ya kuingia ndani ya jiji, na tutakutendea mema.”
25 Hivyo akawaonyesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote.
Aliwaonyesha njia ya kuingia kwenye mji. Waliuteka mji kwa makali ya upanga, lakini wakamuacha mtu huyo na ndugu zake wote waondoke.
26 Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambao ndio jina lake hadi leo.
Na mtu huyo akaenda nchi ya Wahiti, akajenga mji, akauita Luzu, ambalo jina lake hata leo.
27 Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na vijiji vyake, au watu wa Taanaki na vijiji vyake, au watu wa Dori na vijiji vyake, au watu wa Ibleamu na vijiji vyake, au watu wa Megido na vijiji vyake, lakini Wakanaani waliazimu kuishi katika nchi ile.
Watu wa Manase hawakuwafukuza watu waliokuwa katika miji ya Bethsheani na vijiji vyake, au Taanaki na vijiji vyake, au wale waliokaa Dori na vijiji vyake, wala wale waliokaa Ibleamu na vijiji vyake, wala walioshi Megido na vijiji vyake, kwa sababu Wakanaani walikuwa wameamua kuishi katika nchi hiyo.
28 Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa.
Israeli ipokuwa na nguvu, waliwalazimisha Wakanaani wawatumikie kwa kazi ngumu, lakini hawakuwafukuza kabisa.
29 Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi humo miongoni mwao.
Efraimu hakuwafukuza Wakanaani waliokaa Gezeri; kwa hiyo Wakanaani wakakaa kati yao.
30 Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, wala walioishi Nahaloli, ambao walibaki miongoni mwao; bali waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.
Zebuloni hakuwafukuza watu wa Kitroni, wala watu waliokuwa Nahaloli; na Wakanaani wakaendelea kuishi pamoja nao; lakini Zabuloni akawalazimisha Wakanaani wawatumikie kwa kazi ngumu.
31 Wala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu
Asheri hakuwafukuza watu wanaoishi Aka, au watu wanaoishi Sidoni, au wale wanaoishi Alabu, Akzib, Helba, Afeka, au Rehobu.
32 na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi.
Kwa hiyo kabila ya Asheri iliishi kati ya Wakanaani (waliokaa katika nchi hiyo), kwa sababu hawakuwafukuza.
33 Wala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa.
Na kabila la Naftali halikuwafukuza watu waliokuwa wakiishi Bethshemeshi, wala waliokuwa wakiishi Bethanathi. Kwa hiyo kabila la Naftali liliishi kati ya Wakanaani (watu waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo). Hata hivyo, wenyeji wa Bethshemeshi na Bethanathi walilazimishwa kufanya kazi ngumu kwa Naphthali.
34 Waamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, kwa maana hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare.
Waamori waliwalazimisha kabila la Dani kuishi katika nchi ya kilima, hawakuwaruhusu kuja bondeni.
35 Waamori pia wakaendelea kukaa katika Mlima Heresi, katika Aiyaloni na Shaalbimu, lakini mkono wa nyumba ya Yosefu ukawalemea, nao wakashindwa hata wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa.
Basi Waamori waliishi katika mlima wa Heresi, huko Aiyaloni, na Shaalbimu, lakini nguvu za kijeshi za nyumba ya Yusufu ziliwashinda, nao wakalazimishwa kuwatumikia kwa kazi ngumu.
36 Mpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.
Mpaka wa Waamori ulikuwa kutoka kilima cha Akrabimu huko Sela hadi nchi ya vilima.

< Waamuzi 1 >