< Waamuzi 21 >

1 Wana wa Israeli walikuwa wameapa kwa kiapo kule Mispa: “Hapana mtu yeyote atakayemwoza binti yake kwa Wabenyamini.”
Sasa watu wa Israeli walikuwa wameahidi huko Mispa, “Hakuna hata mmoja wetu atakayempa binti yake kuolewa na Mbenyamini.”
2 Watu wakaenda Betheli, wakaketi mbele za Mungu mpaka jioni, wakapaza sauti zao, wakalia sana.
Ndipo watu wakaenda Betheli, wakakaa huko mbele ya Mungu hata jioni; wakalia kwa sauti kubwa.
3 Wakasema, “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, kwa nini jambo hili limewapata Waisraeli? Kwa nini kabila moja la Israeli limekosekana?”
Walipiga kelele, “Kwa nini, Bwana, Mungu wa Israeli, amefanya jambo hili kwa Waisraeli, kwamba moja ya makabila yetu linapotea leo?”
4 Kesho yake asubuhi na mapema watu wakajenga madhabahu na kuleta sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
Siku iliyofuata watu waliamka mapema na wakajenga madhabahu huko na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
5 Ndipo Waisraeli wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikufika katika mkutano kumkaribia Bwana?” Kwa kuwa walikuwa wameweka kiapo kikuu kuwa yeyote asiyefika mbele za Bwana huko Mispa, kwa hakika angeuawa.
Watu wa Israeli wakasema, “Ni nani kati ya kabila zote za Israeli hawakuja katika mkutano wa Bwana?” Kwa kuwa walikuwa wamefanya ahadi muhimu juu ya mtu yeyote ambaye hakuja kwa Bwana huko Mispa. Wakasema, “Hakika yeye atauawa.”
6 Basi Waisraeli wakaghairi kwa ajili ya ndugu zao Wabenyamini, wakasema, “Leo kabila moja limekatiliwa mbali na Israeli.
Watu wa Israeli walikuwa na huruma kwa ndugu yao Benyamini. Wakasema, “Leo hii kabila moja limekatiliwa mbali kutoka Israeli.
7 Sasa tutawezaje kuwapa mabinti zetu wawe wake zao kwa hao waliobaki maadamu tumeapa kwa Bwana kuwa hatutawapa binti zetu kuwa wake zao?”
Ni nani atakayewapa wale walioachwa wake, kwa kuwa tumeahidi kwa Bwana kwamba hatuwezi kuwaruhusu yeyote kati yao aoe binti zetu?”
8 Ndipo wakasema, “Ni kabila lipi la Israeli ambalo halikufika mbele za Bwana huko Mispa?” Wakagundua kuwa hakuna hata mmoja aliyetoka Yabeshi-Gileadi aliyefika kambini kwa ajili ya kusanyiko la mkutano.
Wakasema, “Ni nani kati ya kabila za Israeli hawakuja kwa Bwana huko Mispa? Ilionekana kuwa hakuna mtu aliyekuja kwenye mkusanyiko kutoka Jabeshi-Gileadi.
9 Walipohesabu waliona hakuna mtu yeyote wa Yabeshi-Gileadi aliyekuwepo.
Kwa maana watu walipokuwa wamepangwa kwa utaratibu, tazama, hakuna hata mmoja wa wenyeji wa Yabeshi Gileadi.
10 Ndipo mkutano wakatuma askari 12,000 na wakawaamuru kwenda Yabeshi-Gileadi na kuwaua wale wote waishio huko, walikuwepo wake na watoto.
Mkutano huo uliwatuma watu kumi na wawili wa watu wao wenye ujasiri kwa maagizo ya kwenda Jabeshi-gileadi na kuwaangamiza, na kuwaua, hata wanawake na watoto.
11 Wakasema, “Hilo ndilo mtakalofanya. Ueni kila mtu mume na mke ambaye si bikira.”
“Fanya hivi unapaswa kuua kila mume na kila mwanamke aliyelala na mwanaume.”
12 Wakakuta kati ya watu walioishi Yabeshi-Gileadi wanawali mia nne ambao hawajakutana kimwili na mwanaume, nao wakawachukua kwenye kambi huko Shilo katika nchi ya Kanaani.
Watu wale walikuta watu kati ya hao waliokaa Yabeshi-gileadi, wanawake mia nne ambao hawakulala na mwanaume, wakawapeleka kwenye kambi huko Shilo, huko Kanaani.
13 Ndipo mkutano ukatuma ujumbe wa amani kwa Wabenyamini huko katika mwamba wa Rimoni.
Mkutano wote ukatuma ujumbe na kuwaambia watu wa Benyamini waliokuwa kwenye mwamba wa Rimoni kwamba walikuwa wanawapa amani.
14 Basi Wabenyamini wakarudi nyumbani mwao, wakapewa wale wanawali wa Yabeshi-Gileadi waliowaponya. Lakini hawakuwatosha wanaume wote.
Wabenyamini walirudi wakati huo na walipewa wanawake wa Yabeshi Gileadi, lakini hapakuwa na wanawake wa kutosha kwa wote.
15 Waisraeli wakasikitika kwa ajili ya Wabenyamini, kwa kuwa Bwana ameweka ufa katika makabila ya Israeli.
Watu waliomboleza kwa kile kilichotokea Benyamini, kwa kuwa Bwana alifanya mgawanyiko kati ya makabila ya Israeli.
16 Viongozi wa kusanyiko wakasema, “Kwa kuwa wanawake wa Wabenyamini wameangamizwa, tufanyeje ili kuwapatia wake wale wanaume waliosalia?
Kisha wakuu wa mkutano wakasema, “Tutafanyaje ili Wabenyamini wapate wake, kwa kuwa wanawake wa Benyamini wameuawa?”
17 Wale waliopona wa Wabenyamini ni lazima tuwape wake, ili wawe na warithi, ili kabila lolote katika Israeli lisifutike.
Wakasema, 'Lazima kuwe na urithi kwa Wabenyamini waliosalia, ili kabila lisiharibiwe kutoka Israeli.
18 Hatuwezi kuwapa binti zetu kuwa wake, kwa kuwa sisi Waisraeli tumeapa kiapo hiki: ‘Alaaniwe mtu yeyote ampaye Mbenyamini mke.’”
Hatuwezi kuwapa wake kutoka kwa binti zetu, kwa kuwa wana wa Israeli walikuwa wametoa ahadi, 'Na alaaniwe mtu atakayempa Benyamini mke.'”
19 Ndipo waliposema, “Tazama iko sikukuu ya kila mwaka ya Bwana katika Shilo, kaskazini ya Betheli na mashariki mwa ile barabara itokayo Betheli kwenda Shekemu, upande wa kusini wa Lebona.”
Wakasema, “Mnajua kuwa kuna sikukuu kwa Bwana kila mwaka huko Shilo ( ambayo ni kaskazini ya Betheli, mashariki ya barabara inayopanda kutoka Betheli hadi Shekemu, na kusini mwa Lebona).
20 Hivyo wakawaelekeza Wabenyamini wakisema, “Nendeni mkajifiche kwenye mashamba ya mizabibu,
Wakawaagiza wana wa Benyamini, wakisema, “Nendeni, mjifiche kwa siri, na kusubiri katika mashamba ya mizabibu.
21 nanyi mwangalie. Wasichana wa Shilo watakapojiunga kwenye kucheza, ninyi tokeni kwenye hayo mashamba ya mizabibu na kila mmoja akamate mwanamke mmoja toka miongoni mwa hao wasichana wa Shilo na mwende nao katika nchi ya Benyamini.
Tazama wakati ambapo wasichana kutoka Shilo watatoka kucheza, Tokeni nje ya mizabibu na kila mmoja wenu anapaswa kunyakua mke kutoka kwa wasichana wa Shilo, kisha kurudi kwenye nchi ya Benyamini.
22 Baba zao au ndugu zao waume watakapotulalamikia, tutawaambia, ‘Kuweni wakarimu kwetu, nanyi mturuhusu tuwe nao kwa kuwa hatukuweza kumpa kila mtu mke tulipopigana. Lakini ninyi pia hamna hatia, kwa kuwa hamkuwapa wao binti zenu kuwa wake.’”
Wakati baba zao au ndugu zao watakapokuja kutupinga, tutawaambia, 'Tupeni neema! Waache wabaki kwa sababu hatukupata wake kwa kila mtu wakati wa vita. Na ninyi hamna hatia juu ya ahadi, kwa sababu hamkuwapa wao binti zenu.'”
23 Basi hivyo ndivyo Wabenyamini walivyofanya. Wakati wasichana walipokuwa wakicheza, kila mtu akamkamata msichana mmoja akamchukua akaenda naye ili awe mke wake. Kisha wakarudi katika urithi wao na kuijenga upya miji na kuishi humo.
Watu wa Benyamini walifanya hivyo. Walichukua idadi ya wake waliowahitaji kutoka kwa wasichana waliokuwa wakicheza, nao wakawachukua ili wawe wake zao. Wakaenda na kurudi mahali pa urithi wao; wakajenga tena miji, na wakaishi ndani yao.
24 Wakati huo Waisraeli wakaondoka sehemu ile na kwenda nyumbani kwao, kwenye makabila yao na kwa jamaa zao, kila mmoja kwenye urithi wake mwenyewe.
Kisha watu wa Israeli wakatoka mahali hapo na kwenda nyumbani, kila mmoja kwa kabila lake na ukoo, na kila mmoja kwa urithi wake mwenyewe.
25 Katika siku hizo kulikuwa hakuna mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya kile alichoona ni sawa machoni pake mwenyewe.
Siku hizo hapakuwa na mfalme huko Israeli. Kila mtu alifanya yaliyo sawa machoni pake mwenyewe.

< Waamuzi 21 >